WABUNGE WAANDAA MKAKATI MPYA WA KUMNG'OA WAZIRI MKUU PINDA

Dodoma/Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge wameanzisha mkakati wa kumwondoa madarakani, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kile wanachoda...

Dodoma/Dar es Salaam.
Baadhi ya wabunge wameanzisha mkakati wa kumwondoa madarakani, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kile wanachodai kuwa hawaridhishwi na utendaji wake serikalini.
Hiyo ni dalili kwamba kung’oka kwa mawaziri wanne kutokana na matokeo ya ripoti ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili hakujamnusuru Pinda, kwani baadhi ya wabunge wanaendelea na msimamo kwamba naye ajiuzulu kwa kushindwa kuwasimamia wenzake.
Mawaziri waliong’oka baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao kutokana na ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete inatafsiriwa na wengi kama njia ya kuwapoza wabunge na kumwokoa Pinda ambaye ikiwa atang’oka itamaanisha kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili jana zinasema wabunge 26 wametia saini fomu maalumu ya kutaka Bunge litumie mamlaka yake ya kikatiba kumng’oa Pinda kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alisema hili jana kuwa ukusanyaji saini za wabunge aliouanzisha Ijumaa jioni unakwenda vizuri.
“Kung’oka kwa mawaziri wale wanne inatosha kuthibitisha kuwa Pinda amepoteza uhalali wa kuwa Waziri Mkuu kutokana na kushindwa kuwasimamia walio chini yake,” alisema Machali.
“Rais tunaweza kumuacha, lakini Pinda ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali. Kama wapo mawaziri wameboronga ni wazi na yeye anaingia moja kwa moja katika hilo kapu,” alisema na kuongeza:
“Kama kweli tunataka taifa lisonge mbele kutoka hapa tulipo ni lazima tumuondoe Pinda…….. amekuwa mpole mno, mzito kufanya uamuzi na analea matatizo.”
Hata hivyo, alisema wabunge waliosaini fomu hiyo, wote wanatoka kambi ya upinzani na kusema wabunge wengi wa CCM aliowafuata kuwaomba watie saini wanaogopa au wanasita kufanya hivyo.
 “Nataka niwaambie wabunge wa CCM hebu tusimame katika masilahi ya umma… Serikali inapofanya vibaya wanaoumia ni wananchi wetu bila kujali ni mwanachama wa chama gani,” alisema.
Pinda tayari amesema wazi kwamba yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake iwapo Rais Kikwete ataamua kumuondoa na kwamba hata Rais asipochukua hatua hiyo ni ruksa kwa wabunge kutumia mamlaka yao ya kikatiba ya kumuondoa kwa njia ya kura ya kutokuwa na imani naye.

Wabunge wengine
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ambaye alikuwa mwiba kwa Pinda bungeni alisema: “Haya ni mambo ya ajabu sana, tutaendelea kubadilisha glasi lakini mvinyo ni uleule”.
Alisema uwajibikaji wa Serikali unaanzia kwa Waziri Mkuu na kusema anamuomba Rais atafakari ombi lake la kumfuta kazi Pinda.
“Tufike mahali tuambiane ukweli bila kumung’unya maneno kama kweli tunataka kuisaidia nchi yetu na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo inapendwa na kuaminiwa na Watanzania,” alisema Lugola.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa  alisema anavyomuona Pinda na kutafsiri utendaji wake, anadhani kuwa viatu vya uwaziri mkuu vinampwaya.
“Haiwezekani mara mbili ndani ya Bunge mawaziri wang’oke halafu wewe ubaki… wanapoboronga katika utendaji wao lazima pia umguse kiranja wao (Pinda) na hili bado tutalia nalo,” alisema Msigwa na kuongeza:
“Tulitarajia Waziri Mkuu awe wa kwanza kutafakari na kujipima kama kweli anastahili kubaki hasa baada ya madudu yale ambayo yameichafua Serikali mbele ya umma.”
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema wakati umefika kwa Waziri Mkuu, Pinda kukaa pembeni na kumwachia Rais Kikwete aunde safu nyingine.
“Pinda ni mtu wangu. Tunaheshimiana na sina chuki naye. Kwanza yeye ni mmoja wa watu ninaotuhumiwa kuwapa jimbo apite bila kupingwa na kuniletea matatizo kwenye chama changu.
“Hivyo sina chuki naye maana pia anatoka kanda yetu. Hata hivyo, hali ya sasa ya nchi inahitaji kupumua. Ampe nafasi Rais aunde Serikali upya.”

Alisema kuna tatizo kubwa la uongozi ndani ya nchi na kuwa mambo hayaendi licha ya juhudi mbalimbali pamoja na Bajeti ya Serikali kuongezeka kila kukicha.
“Huduma hazifiki kwa wananchi. Serikali ni kama haipo, nchi imevimba na inahitaji kupumua. Mwaka 1990 Rais Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi,) alikumbwa na hali kama hii na Warioba alijiuzulu ili kumpa nafasi kuunda upya Serikali. Alimrudisha Warioba lakini mawaziri wengi waliondoka,” alisema Zitto.
Aprili mwaka jana katika mazingira yanayofanana na ya mkutano wa 14 wa Bunge uliomalizika Jumamosi, wabunge 74 wakiwamo wa CCM walitia saini fomu ya kutaka kumng’oa Pinda.
Hata hivyo, aliepuka zahama hiyo, baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri mwezi mmoja baadaye na kuwaondoa mawaziri sita na manaibu waziri wawili waliokuwa wakishinikizwa kuachia ngazi.
Mawaziri hao walikuwa William Ngeleja (Nishati na Madini), Mustafa Mkulo (Fedha), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omar Nungu (Mawasiliano), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii). Manaibu walikuwa Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).

Credit: Mwananchi

Related

OTHER NEWS 1060807097049016301

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item