MWANDISHI UINGEREZA AJA KUONA VITA DHIDI YA UJANGILI
Dar es Salaam. Serikali imeanza juhudi za kujinasua kwenye lawama kwamba haifanyi juhudi za kutosha kupambana na ujangili kwa ku...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/03/mwandishi-uingereza-aja-kuona-vita.html
Dar es Salaam.
Serikali imeanza juhudi za
kujinasua kwenye lawama kwamba haifanyi juhudi za kutosha kupambana na
ujangili kwa kuwaalika waandishi wa habari wa kimataifa ili kujionea
kazi inayofanyika.
Tayari mwandishi wa Habari wa Uingereza
aliyeandika habari katika Gazeti la Daily Mail, Martin Fletcher kuwa
Tanzania haifanyi jitihada zozote kukabiliana na ujangili amewasili
nchini.
Mwandishi huyo aliandika habari kwenye gazeti hilo
toleo la Februari 8 na 9, mwaka huu kwamba Serikali ya Tanzania
imeshindwa kutimiza wajibu wake katika kuwalinda faru na tembo ambao
wako hatarini kutoweka.
Mwandishi huyo jana alitembelea ghala la meno ya
tembo yaliyohifadhiwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii kumwonyesha
juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika kupambana na ujangili nchini.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuona ghala hilo, Fletcher alisema ni
jambo jema kwa kuwa ameona sehemu ya hazina hiyo.
“Nimeona kwa sehemu kubwa hifadhi iliyopo, bado
ninaendelea kufuata utaratibu kwa kuwa nimealikwa, siwezi kusema lolote
kwa sasa,” alisema Fletcher. Kwa mujibu wa ratiba, leo atapelekwa katika
Mbuga ya Selous ambako atajionea ‘utajiri wa wanyama kwenye mbuga
hiyo’.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
alikutana na mwandishi huyo lakini akakanusha kuwa Serikali imemwalika,
akisema hiyo ilikuwa ni sehemu ya mpango wake akitaka kujionea mambo
yanayotendeka nchini kuhusu suala la ujangili.
Alisema mbali na mwandishi huyo, wengine wa
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na CNN ya Marekani nao wameomba
kufanya hivyo.
Habari zilizoandikwa na mwandishi huyo ziliwapa
wakati mgumu Rais Jakaya Kikwete na Waziri Nyalandu kwa kuwa
zilichapishwa wakati Rais akihudhuria mkutano kuhusu ulinzi wa wanyama
walio hatarini kutoweka.
MWANANCHI
MWANANCHI