KOMBORA LA MWAKYEMBE LAPIGA VIGOGO SABA

WAZIRI WA UCHUKUZI DR. HARRISON MWAKYEMBE Ni wanaotuhumiwa kutafuna Sh bilioni 2 za TPA.   KASI ya utendaji kazi ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. ...

WAZIRI WA UCHUKUZI DR. HARRISON MWAKYEMBE

Ni wanaotuhumiwa kutafuna Sh bilioni 2 za TPA.

 KASI ya utendaji kazi ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na juhudi zake za kuisafisha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), imeingia mkoani Mwanza. Katika kasi hiyo, Waziri Mwekyembe amesimamisha kazi kupisha uchunguzi wafanyakazi saba wa mamlaka hiyo mkoani Mwanza, kutokana na tuhuma za ubadhirifu.

Machi mwaka huu, Waziri Mwakyembe aliiagiza Bodi ya Mamlaka ya TPA,kuwasimamisha na kufanya uchunguzi, baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika bandari ya Mwanza Kusini.

Katika ziara hiyo, alibaini kuwapo na ubadhirifu wa Sh bilioni 2.2, zinazodaiwa kutumiwa vibaya na watendaji hao.

Wafanyakazi waliosimamishwa na vyeo vyao kwenye mabano ni Ludovick Ngowi (Mkuu wa Bandari), Khasim Mori (Afisa Ugavi Manunuzi) na Lucas Magomora (Fundi na Msimamizi wa Vibarua).

Wengine waliotajwa kwa jina moja moja na nyadhifa zao kwenye mabano ni Msechu (Mkaguzi wa Mkuu wa Ndani), Singano (Mkuu wa Usalama na Ulinzi) na Komba (Mwenyekiti wa Vyama vya Wafanyakazi wa Tawi la Bandari).

Waziri Mwakyembe katika ziara hiyo, aliambatana na naibu wake, Dk. Charles Tizeba.

Baada ya kufika jijini Mwanza, ghafla waliomba taarifa ya fedha ya mwaka 2011/12 na kuelezwa kuwa makusanyo ya mwaka huo yalikuwa Sh milioni 969.9, lakini cha kushangaza matumizi yalikuwa Sh bilioni 2.2.
Utata mwingine, uliogubika taarifa hiyo ni pale ilipoonyesha kampuni iliyopewa tenda ya kukusanya ushuru bandarini, ikizidisha muda wa kufanya kazi hiyo tofauti na mkataba ulivyosainiwa.

“Kampuni ya kukusanya mapato ya mizigo, inadaiwa kuwa ni ya baadhi ya watumishi ambao waliianzisha na kusajiliwa kisha kuipitisha kwenye zabuni na inadaiwa kuikosesha mapato na kuisababishia hasara mamlaka,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema wanazo taarifa za watumishi kumiliki majumba na kujilimbikizia magari ya kifahari na mali nyingine kwa manufaa yao binafsi.

Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imeanza kupambana na watumishi wanaotumia madaraka yao kuikosesha mapato.

Waziri Mwakyembe, alisema wakati mapato yakionekana kuwa kiduchu na matumizi kuwa makubwa zaidi, ushuru ulikuwa ukilipwa kwa kiasi kikubwa cha zaidi ya Sh milioni 80 hadi 100 kwa mwezi na mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya Mohamed Bakhressa wa jijini Dar es Salaam, ambaye husafirisha bidhaa zake nchi jirani na mikoa ya kanda ya Ziwa, hivyo fedha nyingine ziliishia mikononi mwao.

Hadi Waziri Mwakyembe anaagiza watumishi hao wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi, tayari taarifa ya nusu mwaka wa fedha ilikuwa inaonyesha kukusanywa kiasi cha Sh milioni 711.9,lakini matumizi yakiwa zaidi ya kiasi hicho ambapo ilibainika kutumia zaidi ya bilioni moja.

Habari kutoka ndani ya bandari, zimesema baadhi ya watumishi wa Bandari wamekuwa wakishirikiana na wale wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC) kuwasafirisha wafanyabiashara wa nguo, viatu, vyombo, mitumba ya redio, spea za magari na pikipiki, vipodozi na vingine kwenda na kurudi kutoka nchini Uganda.

Wafanyabiashara hao, pamoja na mizigo yao hufichwa kwenye vyumba vya wafanyakazi wa meli kwa makubaliano fulani na kisha hupakua mizigo yao, baada ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuondoka sehemu za kazi.

Kwa mujibu wa habari hizo, baadhi ya wafanyakazi hao wanamiliki maduka ya bidhaa hizo jijini Mwanza na meli zinazotumiwa kusafirisha mizigo yao kinyemela zimetajwa kuwa MV Kabalega ya Uganda, MV Wimbi, MV Umoja na MV Serengeti za Marine na zile za watu binafsi (majina tunayo.)

Ngowi na Mori, walipohojiwa kuhusu tuhuma hizo walidai hawana makosa yoyote na hawezi kuzungumzia suala hilo kwa waandishi, bali watajieleza kwenye tume ambayo itakwenda kufanya uchunguzi.

Walipoulizwa kama wamepokea barua za kusimamishwa kazi, walikiri kuzipokea.

“Mimi sina kosa, nadhani nimeonewa tu maana ni mgeni, siwezi kuzungumzia suala hili kwenu waandishi, tunasubiri tume inayokuja kutuhoji na kuchunguza suala hili,” alisema Ngowi.

SOURCE: Mtanzania

Related

OTHER NEWS 8690238682572455648

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item