MWIZI MTANDAO WA SIMU AKAMATWA

MTANDAO mpya wa wizi wa fedha zinazotumwa kupitia kwenye simu za viganjani unaowahusisha wafanyabiashara na baadhi ya watumishi wa kampuni...

MTANDAO mpya wa wizi wa fedha zinazotumwa kupitia kwenye simu za viganjani unaowahusisha wafanyabiashara na baadhi ya watumishi wa kampuni za simu umebainika. Tayari mfanyabiashara mmoja anayejihusisha na uuzaji wa ‘line’ za simu za mkononi aliyetambuliwa kwa jina moja la Fikri, amekwishakamatwa na kuwataja washirika wenzake katika wizi huo kuwa ni wafanyakazi wa kampuni za simu za mkononi.

Fikri alikamatwa jana akiuza namba maalumu ya simu ya mkononi ya kampuni moja kwa mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Brockwely Mchana, ambaye ni muhanga wa matukio hayo.

Mchana akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya Fikri kukamatwa, alisema amepata kununua kadi maalumu za simu mara kadhaa kwa mfanyabiashara huyo ambazo baada ya kuzitumia kutuma fedha zilikufa na hata aliporipoti kwenye kampuni husika ili kurejeshewa namba yake, kiasi cha fedha kilichokuwa kwenye kadi hiyo hakukikuta.

Alisema amekwishanunua kadi za simu mara mbili kwa Fikri ambazo baada ya kuzitumia kutuma pesa zilikufa na pesa yake kupotea.

Pia alieleza kuwa hata mkewe naye alikwishapoteza pesa alizozitaja kuwa ni zaidi ya shilingi milioni kumi ambazo alikuwa akizihamisha kutoka kwenye simu yake kuziingiza kwenye akaunti yake ya benki.

Alisema kuwa mtandao wa wizi wa fedha kupitia simu ya kiganjani ni mkubwa na sasa unaendeshwa kwa kutumia namba maalumu za kadi.

“Nikisema Special number namaanisha unakuwa na namba za mitandao yote zinazofanana kwa mfano namba zangu za simu za mitandao yote zinakuwa zinafanana, kwa hiyo hawa jamaa wanajifanya kuendesha huduma hiyo lakini wanakuwa na lengo lao maalumu.

“Mimi wameniibia pesa zangu zaidi ya mara mbili, niliweka laki nne wakanitapeli hata mke wangu wameishawahi kumuibia zaidi ya milioni kumi ambapo aliingiza fedha katika akaunti yake ya simu ya kiganjani na kuzituma katika akaunti yake ya benki lakini alipoingiza tu fedha hizo line yake ilikufa na hata alipokwenda kupedwa mpya fedha zake hazikupatani,” alisema Mchana.

Alipoulizwa Fikri ambaye gazeti hili lilimkuta amewekwa chini ya ulinzi eneo la Sinza Mori katika ofisi za Kampuni ya Zinol Tanzania Ltd, namna ambavyo amekuwa akitekeleza wizi huo, alisema hakujua kama kadi za simu alizokuwa akipewa na washirika wake wa kibiashara zilikuwa za wizi.

Alisema kwa muda mrefu amekuwa akifanya biashara ya kuuza kadi za simu zenye namba maalumu na anao washirika wake wa kibiashara katika kampuni mbalimbali za simu ambao wamekuwa wakimpatia kadi hizo na kusisitiza kuwa hakujua iwapo zilikuwa zimetengeshwa kwa ajili ya kutumika kuibia wateja.

“Sikufahamu kama hawa rafiki zangu ni matapeli, mimi wananituma tu kupeleka ‘line’ kwa wateja na hata leo hii sikujua kama nimeingia kwenye mtego wa kukamatwa kwa sababu wateja hawa walinipigia simu wakihitaji ‘specil namba,” alisema Fikri.

Source: Mtanzania

Related

OTHER NEWS 383466850452343669

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item