UN YALAANI MASHAMBULIZI MOGADISHU
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi dhidi ya ofisi za umoja wa mataiofa mjini Mogadishu Somalia. Ban...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/06/un-yalaani-mashambulizi-mogadishu.html
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi dhidi ya ofisi za umoja wa mataiofa mjini Mogadishu Somalia.
Ban amesema kupitia kwa msemaji wake kuwa shambulizi hilo lilikuwa kitendo cha unyama, na ambacho kilisababisha vifo vya watu 15.
Kwa Mujibu wa msemaji wake Ban,pia alisisitiza kuwa Umoja wa mataifa hautaogopa kutokana na mashambulizi hayo kuendelea na kazi zake nchini Somalia.
Washambuliaji walishambulia ofisi hizo kwa kulipua gari lililokuwa limeegeshwa karibu na lango kuu la ofisi zenyewe na kisha kuanza kukabiliana na maafisa wa usalama kwa kufyatuliana risasi ndani ya ofisi hizo.
Kwingineko mjumbe maalum wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (SRCC) nchini Somalia, Balozi Mahamat Saleh Annadif ameshutumu vikali shambulio la kigaidi lililofanywa leo na magaidi wa Al-Shabaab katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu.
"Tunalaani vikali shambulio hili la kinyama katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu. Mashambulio haya yasiyofanikiwa yanayoendeshwa na Al-Shabaab yanalenga tu kuvuruga jitihada zinazochukuliwa na wananchi wa Somalia baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya ishirini na magaidi hao hawawezi kuzuia jitihada zetu za pamoja kuendelea kuwasaidia wananchi wa Somalia kuijenga nchi yao" amesema Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (SRCC), Balozi Mahamat Saleh Annadif.
Balozi Mahamet Annadif amepongeza hatua ya haraka iliyochukuliwa na majeshi maalum ya AMISOM na majeshi ya usalama ya Somalia na amesisitiza kuwa AMISOM haitaacha kuchukua hatua za kuimarisha usalama nchini Somalia.
"Umoja wa Afrika na AMISOM kwa sasa wako pamoja na wananchi wa Somalia," amesema Balozi Annadif, wakati akituma salaam za rambirambi kwa wale waliowapoteza wapendwa wao katika shambulio hilo na kuwaombea kupona haraka watu wote waliojeruhiwa.
Takriban watu 12 wakiwemo ria wa kigeni wameuawa katika shambulizi baya lililofanywa dhidi ya ofisi ya umoja wa mataifa mjini Mogadishu Somalia
Ufyatulianaji risasi uliodumu kwa zaidi ya saa moja ulishuhudiwa ndani ya ofisi za shirika la maendeleo la umoja wa mataifa UNDP.
Mpiga picha aliyeshuhudia kisa hicho, aliambia BBC kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga alijilipua ndani ya gari moja liliokuwa karibu na lango kuu la ofisi hizo na kuwa aliona washambuliaji wanne wakiingia ndani ya ofisi yenyewe.
Kundi la Al Shabaab limesema kuwa ndilo lilifanya shambulizi hilo.
Somalia haijakuwa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 20, na kipindi hicho chote nchi hiyo ilikuwa eneo la vita.
Lakini sasa serikali inapata msaada kutoka kwa umoja wa mataifa na imeweza kudhibiti miji mingi ya nchi hiyo na hata kufurusha wapiganaji wa al-Shabaab.
Hata hivyo waziri mkuu Abdi Farah Shirdon Saaid, amesema kuwa Al Shabaab haiwezi kushinda vita dhidi ya serikali inayojaribu kuleta utulivu na amani nchini kote
Ofisi kuu ya shirika la UNDP, iko karibu na eneo lenye ulinzi mkali karibu na uwanja wa ndege Kusini mwa Mogadishu.
Baadhi ya wale waliouawa na wafanyakazi wa UN, majengo pia yameharibiwa na watu wamelazimika kukimbilia usalama wao.
SOURCE: BBC
SOURCE: BBC