TAMKO LA RAIS NA AMIRI JESHI MKUU JAKAYA MRISHO KIWETE KUHUSU TUKIO LA KUSHAMBULIWA NA KUUWAWA KWA WANAJESHI SABA WA JWTZ WALIOKUWA WAKILINDA AMANI DARFUR SUDAN.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuz...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/07/tamko-la-rais-na-amiri-jeshi-mkuu.html
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kushambuliwa
na kuuawa kwa vijana saba hodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur, Sudan.
Kwa hakika, Rais amesikitishwa
sana na kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania
wamejeruhiwa na waasi wa Sudan na ametuma salamu za rambirambi za moyoni
mwake kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.
Aidha, Rais Kikwete anaungana na
Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za
wafiwa kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia
anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo
waweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani
chini ya Umoja wa Mataifa.
Katika salamu zake za rambirambi
kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunynge na
familia za wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya
kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya
vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana
ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta
amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza
maisha yao kwa kushambuliwa na waassi.”
Rais Kikwete ameongeza kumwambia
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya
Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana
wetu hao tokea walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika
tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007,
wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na
kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa
kujivunia kazi yao.”
Amesisitiza Mheshimiwa Rais
Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi
za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma
salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na
wapigaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao. “
“Aidha, kupitia kwako, natuma
salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu
zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza.
Wajue kuwa uchungu wao ni uchungu
wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi
Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. Vile
vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za
marehemu. Amina”.
Kwa walioumia, Rais Kikwete
amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia na Watanzania wenzangu
katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo tukiwaombea kwa
Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa
amani chini ya Umoja wa Mataifa.”
Vijana hao waliopoteza maisha yao
na walioumia, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao
walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika Darfur
kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi kiasi
cha kilomita 20 kutoka Khorabeche saa tatu asubuhi jana, Jumamosi, Julai
13, 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
14 Julai, 2013