NI VIGUMU KUIFUTA CHADEMA : WASIRA
*Akiri kuwa kazi hiyo si nyepesi Kukifuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) si rahisi; amethibitisha Waziri wa Nchi, Ofis...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/ni-vigumu-kuifuta-chadema-wasira.html
*Akiri kuwa kazi hiyo si nyepesi
Kukifuta
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) si rahisi; amethibitisha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Kauli ya Wasira imekuja huku wahafidhina ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wakishinikiza Chadema ifutwe kwenye Daftari la Msajili wa Vyama
vya Siasa nchini, kwa madai kuwa inakusudia kuifanya nchi isitawalike.
Hivi
karibuni Chadema ilisema itaimarisha kikosi chake cha Red Brigade ili
ichukue dhima ya kuwalinda viongozi wake baada ya Polisi kushindwa
kufanya hivyo.
Wasira
ambaye amewahi kuwa mbunge kupitia pande zote mbili - CCM na upinzani -
anasema badala ya kuwaza kuifuta Chadema, ni vema wananchi wakashiriki
maombi ili Mungu awape (Chadema) mawazo yatakayoafikiana na hali halisi
ya kisiasa na maendeleo nchini.
Anasema
kitendo cha chama hicho kutangaza hadharani kuanzisha ‘jeshi’ la
kuwahami viongozi wake, ni uvunjaji wa wazi wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Mwishoni
mwa mwaka jana, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alisema ana
mamlaka ya kukifuta chama chochote kinachohatarisha amani, hata kama
kina wabunge. Kauli yake iliilenga Chadema.
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 147 (1)
inatamka, “Ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi
chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la
aina yoyote.
(2)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda na
kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na
usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania.
(3)
Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote
cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa
katika ibara ya 5 ya Katiba hii.
(4)
Kwa madhumuni ya ibara hii, "mwanajeshi" maana yake ni askari
aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi,
Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa.”
Katika mahojiano na JAMHURI,
Wasira amewataka viongozi na wafuasi wa Chadema wakae, watafakari vema
msimamo wa Watanzania juu ya mustakabali wa amani hapa nchini.
“Sidhani
kama Watanzania wataunga mkono Chadema ifanye inayotaka kufanya,
nawashauri wasome alama za nyakati, wasome mood (hisia) ya Watanzania
waone kama wanachotaka kukifanya kinaingia katika akili au hisia za
kawaida,” amesema.
Waziri huyo amesema Chadema hawawezi kuunda jeshi na wakati huo huo wakawa wanataka kuiondoa CCM madarakani.
“Huwezi
kuunda jeshi eti kwa sababu huamini Polisi, JWTZ na majeshi mengine
yaliyopo kikatiba. Huwezi kutaka kuingia madarakani, hapo hapo unataka
kuwang’oa Polisi na JWTZ halafu uunde Red Brigade. Nadhani hapo wameenda
mbali. Hawa ni wa kuwaombea kwa Mungu wapate mawazo yanayoafikiana na
hali halisi,” amesema.
Anasema
kuanzishwa kwa Red Brigade kwa kigezo kuwa CCM ina Green Guard, si
sahihi kwa kuwa Green Guard ni tawi ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM).
“Wao
wana BAVICHA. Hakuna anayewazuia kuwa na vijana ndani ya Bavicha kama
ilivyo kwa UVCCM. Lakini kuwa na military training (mafunzo ya kijeshi)
hairuhusiwi, ni illegal (haramu) kwa mujibu wa Katiba na sheria za
nchi,” amesema.
Alipoulizwa
Serikali itachukua hatua gani hasa baada ya Chadema kutangaza kuwa
inaendelea na mpango wake wa kuwapa mafunzo ya kijeshi vijana wake,
Wasira akasema, “Ngoja wasonge na polisi wasonge, wataonana mahali.”
Ingawa hakufafanua kauli hiyo, yaelekea alimaanisha kuwa watakutana na
mkono wa dola.
Tamko la Chadema
Kamati
Kuu ya Chadema ilikutana katika kikao cha dharura kuanzia tarehe 6-7
Julai mwaka katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam kujadili mambo
mbalimbali yakiwamo ya ulinzi na usalama wa viongozi na wanachama wake.
Taarifa
iliyotolewa baadaye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ilisema
Kamati Kuu imesikitishwa na vitendo vya fujo walivyofanyiwa viongozi,
wagombea pamoja na wanachama katika sehemu mbalimbali palipofanyika
uchaguzi.
“Kamati
Kuu imesikitshwa na kulaani vitendo hivyo vikiwamo vya watu kukatwa
mapanga, kuchomwa visu na kubakwa kwa akina mama na vijana wahuni
walioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi. Kamati Kuu imelaani vitendo hivyo
vya kinyama vilivyofanywa mbele ya Jeshi la Polisi na wakuu wa wilaya.
“Ili
kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya
wagombea, wanachama na viongozi wa Chadema, Kamati Kuu imeagiza kwamba
kitengo cha ulinzi cha chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa
kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade nchi nzima wanapewa mafunzo
maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika makambi maalum katika mikoa
yote.
“Kamati
Kuu imejadili maandalizi ya Uchaguzi wa Madiwani katika kata nne (4)
katika Jiji la Arusha. Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa juu
mipango inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa
wa Arusha, Magesa Mulongo, na viongozi wengine wa CCM mkoani Arusha,
katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa kuwatisha wapiga kura kwa kutumia
polisi na vijana wa Green Guard siku ya uchaguzi.”
Msimamo wa Polisi
Punde
baada ya Chadema kutoa taarifa hiyo, Jeshi la Polisi, kupitia Msemaji
wake, Advera Senso, lilitoa taarifa ya kuionya Chadema.
“Kitendo
cha chama chochote cha siasa ikiwamo Chadema kuanzisha kikundi cha
kujihami ni kinyume cha sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua
za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Jeshi la Polisi nchini limeanza
uchunguzi na litachukua hatua kulingana na ushahidi utakaopatikana.
“Jeshi la Polisi litamshughulikia mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha sheria bila kujali wadhifa wake,” ilisema taarifa hiyo.
Source: Jamhuri Newspaper