KOSA LA NDUGAI
HUKU akijitapa kuwa ndiye mlinzi wa kanuni za Bunge, na akiwalaumu wabunge, hasa wa upinzani, kwa kukiuka kanuni hizo, Naibu Spika wa...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/09/kosa-la-ndugai.html
HUKU
akijitapa kuwa ndiye mlinzi wa kanuni za Bunge, na akiwalaumu wabunge,
hasa wa upinzani, kwa kukiuka kanuni hizo, Naibu Spika wa Bunge, Job
Ndugai, amebainika kuwa alivunja kanuni nyingi za Bunge siku ilipozuka
zogo bungeni.
Kwanza, alivunja kanuni inayomtaka ampe fursa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuzungumza.
Pili, alivunja kanuni inayomruhusu kumchukulia hatua mbunge aliyedharau kiti cha spika.
Tatu, alivunja kanuni inayomtaka kuahirisha Bunge kabla ya kuruhusu askari kuingia bungeni unapotokea mzozo.
Kanuni ya 5
(1) inasema: “Katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa katika ibara
ya 84 ya katiba, spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni
hazikutoa mwongozo basi spika atafanya kazi kwa kuzingatia katiba,
sheria nyingine za nchi kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya
maspika wa mabunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye
utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.”
Mbowe hakupewa fursa hiyo.
Kwa
utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola ambao unatumiwa na Bunge letu,
Mbowe ni sawa na Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali
bungeni. Tofauti yao ni moja tu, kwamba waziri mkuu ana dola, na yeye
hana.
Kwa
kuzingatia utamaduni huo, viongozi hawa wanaposimama wakati wowote, kiti
cha spika kitamwomba mbunge anayezungumza aketi chini kisha mmoja kati
yao ambaye atakuwa alisimama atapewa nafasi ya kutoa hoja yake.
Kanuni ya 74 - (1) ndiyo ilipaswa kutumiwa na Ndugai kumshughulikia Mbowe kama alidharau kiti, lakini pia hakuitumia.
Inasomeka:
“Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya spika
na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge ikiwa: (a) kwa maneno au vitendo, mbunge huyo anaonyesha dharau
kwa mamlaka ya spika; au (b) mbunge huyo anafanya kitendo chochote cha
makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza
shughuli hiyo.
Kama Ndugai
angezingatia kanuni za kudumu zinazoliongoza Bunge ili kudhibiti fujo
kama hizo bungeni, alitakiwa kutumia kanuni ya 76 - (1) badala ya
kuwaingiza ukumbini watu wasiopaswa ili kuwadhalilisha baadhi ya wabunge
wa upinzani akiwemo kiongozi wao, Mbowe.
Kanuni hiyo
inasema: “Kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo ikitokea ndani ya
ukumbi wa Bunge na spika ataona kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza
kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha
kikao kwa muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na mpambe wa
Bunge.”
Wadadisi wa
masuala ya kisiasa wanautafsiri uamuzi wa Ndugai kama mbinu ovu
iliyokuwa imeandaliwa mapema ili kuwasonga wapinzani wasiweze kuujadili
muswada wa sheria wa kurekebisha sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka
2013.
Ni wazi kuwa
kasoro nyingi zilizopenyezwa katika muswada huo zisingeweza kuafikiwa
na wapinzani ili kuipa nafasi CCM kudhibiti mchakato wa katiba mpya
unaoendelea.
Katika vuta
ni kuvute hiyo, wapinzani waliitaka serikali kuuondoa muswada huo kisha
kuufanyia marekebisho, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wakiwemo
Wazanzibari.
Serikali na
kiti cha spika hawakuwa tayari kutekeleza masharti hayo, hatua iliyoibua
mvutano wa kikanuni hadi kufikia wabunge kupiga kura ya kuamua ama
mjadala uendelee au usitishwe.
Kura za
wabunge waliotaka mjadala huo uendelee zilikuwa nyingi kutokana na CCM
kuwa na wabunge wengi. Lakini baada ya uamuzi huo, Mbowe alisimama
kuomba ufafanuzi wa kikanuni, akakataliwa.
Licha ya Ndugai kumdhalilisha Mbowe, hakufahamu alitaka kusema nini, hatua iliyoibua hamaki kwa wapinzani.
Mbowe
alitaka kuomba kiti kiwatake viongozi wa serikali, Mwanasheria Mkuu,
Jaji Fredrick Werema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi waweke mezani ushahidi wa vielelezo
vya taarifa walizokuwa wamezitoa.
Kwa mujibu
wa Mbowe, taarifa hizo hazikuwa na uthibitisho wa vielelezo, na kwamba
vile vile zilikuwa na upotoshwaji mwingi, lakini Ndugai hakumpa nafasi
hiyo, badala yake alimtaka aketi chini.
Kiongozi
huyo, hakuketi bali alisisitiza kuwa ana hoja asikilizwe, jambo
lililomfanya Ndugai kuwaita askari ili wamtoe nje bila kujali kama
wengine hawapaswi kuingia ukumbini wakati Bunge linaendelea kwa mujibu
wa kanuni.
Baada ya
askari hao kuitwa na kuingia ndani, wabunge wa upinzani ukimwondoa
Augustino Mrema wa TLP (Vunjo), walimzunguka Mbowe wakipinga asitoke nje
kwa kuzingatia kuwa Ndugai alikuwa amekiuka kanuni.
SOURCE: Chadema Social Media