“Kifo cha mtoto huyo, ndicho kilichozaa tatizo
hili la ukatili dhidi yangu na kunisababishia ulemavu, kwa kuwa huyo
mwanaume wangu na huyo mwanamke aliyezaa nae, walidai kwamba mimi ndiyo
nilimtupia majini marehemu mtoto wao ili afe,”anasema mama huyo.
Mchali, anasema mara baada ya msiba wa mtoto kumalizika,
mwanamume wake huyo alihamia kwa mke mdogo lakini akawa anarejea
nyumbani na kumtukana huku akitishia kufanya lolote analofikiri linafaa.
Anasema baada ya mateso na vitisho kuzidi aliamua
kuondoka kwa mumewe huyo toka mwezi Aprili mwaka huu na kuamua kurudi
kwa wazazi wake huku akiwaacha watoto wake kwenye nyumba waliyokuwa
wakiishi.
Anasema alilazimika kuwaacha watoto kutokana na
agizo la mumewe, aliyekataa asiwachukue, hivyo akaanza maisha mengine ya
upweke bila watoto huku akiendesha maisha yake kwa biashara ya kuuza
samaki.
Anasema mwanzoni mwa mwezi huu, aliugua malaria na
kukaa nyumbani bila kwenda kwenye biashara zake. Agosti saba mwaka huu,
alipata nafuu na kuamua kwenda kumsalimia kaka yake, anayeishi mbali
kidogo na nyumbani kwao na ndipo yakamkuta yaliyomkuta.
Anaeleza kuwa alikaa kwa kaka yake hadi muda wa
futari wakafuturu na kushangaa simu yake ikiita, kuangalia ni namba ya
mpenzi wake huyo. Alipoipokea, aliulizwa aliko, yeye alimweleza yuko kwa
kaka yake na kumtaka amfuate mnadani akale nyama kitendo ambacho
anasema alipingana nacho.
Anasema baadaye aliamua kurudi nyumbani na
kusindikizwa na wifi yake hadi karibu na nyumba yao ikiwa ni saa mbili
usiku.Walipoagana, ghafla akashangaa kusikia sauti ya mumewe ikimuita,
alipogeuka alimwona, kisha akamuuliza alikotoka na kumwambia alikuwa
kwa kaka yake.
Anasema mara baada ya kumjibu mwanamume huyo
alianza kumpiga na hatimaye alianguka chini na mumewe akatoa panga na
kuanza kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili wake.
Hakika hujafa hujaumbika. Mchali amecharangwa kwa
mapanga kuanzia chini ya goti mguu wa kushoto hadi kwenye makalio,
amekatwa sehemu zaidi ya saba mwilini.
Anasema kwa namna anavyoona ni kama alidhamiria
kumuua akisema kuwa mara nyingi akiwa na huo upanga alikuwa analenga
kumtenganisha shingo. Alichofanya mama huyo ni kuweka mikono shingoni
kuzuia panga, kitendo kilichosababisha mkono wake wa kushoto kukatwa
kabisa.
Hawezi kukaa
Mwandishi wa makala haya baadaye alimwomba mwanamke huyo angalau
akae chini, kwani muda mwingi wa mahojiano alikuwa amelala, ndipo
alipojibiwa kwamba hawezi kukaa kwa vile kuna nyama kubwa kwenye makalio
ambayo imeshindikana kushonwa.
Mama huyo anasema wakati mumewe akimcharanga
mapanga, mama yake mzazi aliendelea kupiga ngolo (yowe) kuomba msaada,
kaka yake alikwenda lakini akashindwa kutoa msaada kwa kuwa shemeji yake
huyo alikuwa akimkimbiza na panga.
Anasema kelele za mama yake zilisaidia kuokoa
maisha yake, kwa kuwa majirani walijitokeza, hivyo mwanamume huyo
akaanza kuwakimbiza akitaka kuwadhuru kitendo ambacho mama huyo aliona
ndiyo nafasi pekee kukimbilia ndani.
Matibabu
Mchali, anasema baadaye ndugu zake, walitafuta
usafiri na kufanikiwa kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC
ambako alilazwa kwa siku nne na kurejea nyumbani kutokana na ushauri wa
daktari anayemhudumia.
Kwa mujibu wa mama huyo, daktari anayemtibu
alimtaka Mchali akubali kutibiwa majeraha akiwa nyumbani ili kuepuka
maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na kuepuka gharama za matibabu.
“Sina uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu
kwa kuwa siwezi kutembea, nalazimika kukodi gari na kwa wiki naoshwa
mara tatu. Nisaidieni ndugu zangu, ndoa yangu imenifikisha hapa,”
anasema.
Mchali na hali ya ukatili mkoani Manyara
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa
anasema mtuhumiwa bado hajakamatwa kwa vile hajulikani aliko, huku
akiahidi kuendelea kulifanyia kazi suala hilo.
Akielezea zaidi ukatili mkoani Manyara, anasema
upo, japo ni mdogo ikilinganishwa na mikoa mingine. Anaamini kuwa bado
changamoto ni kubwa kwa wanawake ambao wengi wao wamekuwa
wakinyanyasika.
Sababu kubwa za kunyanyasika kwa wanawake ni
mfumodume. Akasisitiza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea
kuelimisha jamii madhara ya ukatili na kusema jitihada hizo zinapaswa
kuigwa na wananchi na asasi nyingine kuhakikisha ukatili wa kijinsia
unatokomezwa.
Msimamo wa wanaharakati
Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Kwieco, inayojihusisha na
utoaji wa msaada wa kisheria na haki za binadamu mkoani
Kilimanjaro,Wakili Elizabeth Minde, anasema hali ni mbaya hasa kwa
wanandoa wa kike, kwani wengi ndani ya ndoa hawana nguvu.
Taifa lilipofikia
Hali ya ukatili dhidi ya wanawake nchini bado ni
kubwa kutokana na takwimu zinazoonyesha asilimia 39 ya wanawake wenye
umri kati ya mika 15 hadi 49 wanafanyiwa vitendo vya ukatili.
Waziri anena
Naibu waziri wa maendeleo ya jamii jinsia na
watoto, Ummy Mwalimu alikiri ukatili dhidi ya wanawake kuongezeka na
kusema vitendo kama kupigwa na kubakwa ni matukio yanayoongoza zaidi na
yanafanywa na wanaume, huku akisisitiza kuendelea kuangalia namna ya
kufanya ili wanawake nchini waendelee kufurahia maisha.
Safari ya ndoa
Kwa mujibu wa Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga
anayefanya shughuli zake za ushauri Mkoani Mbeya, ndoa inaweza
kufananishwa na safari ndefu yenye matukio yasiyotazamiwa, mengine yenye
kupendeza na mengine yenye kuumiza.
Anasema mafanikio katika ndoa hayapimwi kwa panda
shuka za safari bali yanapimwa kwa jinsi wenza wanavyoshughulikia hali
hizo Ndio kusema ni suala la msingi kwa walio kwenye ndoa kujifunza
namna ya kupambana na changamoto zinapotokea, siyo kutesana au
kukimbiana.
Ushauri zaidi
Mshauri maarufu wa ndoa nchini Uingereza, Hussain
Zahid anasema katika makala ya kitabu chake cha ‘My marriage’ yaani ndoa
yangu kuwa msingi wa kuwa na ndoa nzuri ni kupata muda wa kuzungumza
baina ya wanandoa wenyewe ili kuondoa tofauti zao.
“Kila mtu ajione analo deni la kumpenda na
kumfanyia mema mwenza wake. Kila mtu ajifunze kauli nzuri na matendo
mazuri kwa mwenzi wake…kwamba kabla ya kufanya lolote, tafakari,
ungefurahi kufanyiwa hilo unalotaka kulifanya,” anaonya.
Staili mpya ya maisha kwa baadhi ya wanawake
Tafiti zinaonyesha kwamba kutokana na uwepo kwa mikwaruzo mingi
katika mapenzi, kuna wanawake hawataki tena kuolewa. Kama lengo ni
kupata mtoto au watoto, huwa tayari kuzaa na yeyote hata kama ni mume wa
mtu, kisha jukumu la kulea kwa asilimia kubwa hufanya wao au kwa
kushirikiana na hao waliozaa nao.
Hata hivyo wataalamu mbalimbali wa masuala ya
ndoa, wanashauri watu kuacha tabia hiyo ya kuzaa tu, badala yake wapende
kuzaa wakiwa kwenye ndoa kwa sababu mtoto ambaye hana mzazi mmoja,
huathiriwa sana na matatizo ya kisaikolojia.
Mfano wa utafiti
Kulingana na utafiti uliotolewa hivi karibuni na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Marekani, uko uwezekano mkubwa wa watoto wenye
kulelewa na mzazi mmoja kuwa na tabia mbaya zaidi ya watoto wenye
wazazi wote.
“Kama ni suala la kuiga tabia na matendo mabaya,
watoto ambao wana mzazi mmoja wanaharibika mara tano zaidi ya watoto
ambao wana wazazi wote wawili,” inasema sehemu ya utafiti huo.
Utafiti unaongeza kuwa hata wanapofika kwenye umri
wa ujana, vijana ambao wana mzazi mmoja, wanaharibika zaidi ya wale
ambao wana wazazi wote; Wana uwezekano wa kuharibika mara tatu zaidi ya
vijana ambao wanaishi na wazazi wote wawili.
Si wote huharibika
Hata hivyo utafiti unasisitiza kuwa si watoto wote
wenye mzazi mmoja huwa na tabia mbaya, bali kinachosemwa ni kwamba kwa
asilimia kubwa watoto wa aina hiyo huharibika zaidi ya wale ambao
wanalelewa na wazazi wote wawili. Wanaoathirika zaidi ni wale ambao
wazazi wao wametalakiana, hasa kwa sababu mara nyingi hata nguvu za
kulea watoto hupungua kutokana na wazazi au mzazi husika kuwa na msongo
wa mawazo.
Matendo mabaya kama vile ya mzazi mmoja kuteswa na
mwingine au mtoto kuona mama au baba yake akimshtaki mwenzi wake,
huchangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kumuathiri mtoto kitabia.Tabia
kama za kupigana au mateso mengine kabla ya wanandoa kuachana, huchangia
kuharibu maisha ya mtoto kwa kuona labda kupigana ndio njia nzuri ya
kupambana na mtu anayekukwaza au mwingine kutishwa na uhusiano kwamba
unaweza kusababisha mateso.
Sababu ya migogoro na tiba yake
Mtafiti maarufu wa masuala ya ndoa kutoka Urusi,
Korotayev, A, katika chapisho lake alilolipa jina “Division of Labor by
Gender’ yaani mgawanyiko wa majukumu katika jinsia, anasema msingi wa
kuwa na uhusiano mbaya katika ndoa nyingi ni kutokuwa na fursa ya kukaa
pamoja na kukubali kuondoa kasoro.
“Hakuna mtu ambaye yuko safi kwa asilimia 100.
Umekaa tumboni mwa mama yako na kuna wakati mnagombana, iwe mtu ambaye
mmekutana tu mitaani?”anahoji Korotayev, huku akiwasisitiza watu walio
kwenye ndoa kubuni mbinu za kupendana na kufanya mikakati mingine ya
maisha badala ya kuendekeza ugomvi, kufikiria kuachana au kutafuta
wapenzi wengine.
MWANANCHI