DIWANI WA CCM MKOANI AFARIKI KWA AJALI YA PIKIPIKI YAKE SHINYANGA
SHINYANGA, Tanzania DIWANI wa Kata ya Nyida wilayani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Shindiko Masele(40) amekufa...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/12/diwani-wa-ccm-mkoani-afariki-kwa-ajali.html
SHINYANGA, Tanzania
DIWANI
wa Kata ya Nyida wilayani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM), Shindiko Masele(40) amekufa papo hapo baada ya kupinduka na
pikipiki aliyokuwa akiendesha.
Akizungumza
na waandishi wa habari Mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya ya Shinyanga, Sosteness Ngassa alisema diwani huyo alipata ajali
hiyo juzi saa 2.30 usiku wakati alipojaribu kumkwepa mwendesha baiskeli
na kusababisha pikipiki yake kupoteza mwelekeo na ikagonga mti uliokuwa
kando ya barabara.
Ngassa
alisema baada ya pikipiki hiyo kugonga mti diwani huyo alianguka chini
na kufa papo hapo huku abiria aliyekuwa amebebwa aliyetambuliwa kwa jina
la Silasi Ngoni alijeruhiwa kidogo kwa kupata michubuko ambapo hata
hivyo alikimbizwa katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga
alikotibiwa na kuruhusiwa.
Makamu
mwenyekiti huyo alisema kifo hcho kilichotokea ghafla kimewasikitisha
na kwamba halmashauri yake imepoteza mmoja wa viongozi muhimu na
ameacha pengo ambalo halitokuwa kuwa rahisi kuzibika kwa siku za hivi
karibuni.
Alisema
hivi sasa wanaendelea na maandalizi ya shughuli za mazishi ambapo mwili
wa marehemu ulikuwa umehifadhiwa katika hospitali ya serikali mkoani
Shinyanga na kwamba iwapo mipango itakwenda kama ilivyopangwa mazishi
yake yalitarajiwa kufanyika leo mchana kijijini kwake Nyida.
Kwa
upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi alisema
amepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha diwani huyo na kwamba
alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika suala zima la
uhimizaji wa maendeleo katika kata yake na usimamiaji wa utekelezaji wa
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.
“Nimeshitushwa
na taarifa za kifo cha diwani wetu wa kata ya Nyida, kwa kweli
inasikitisha sana, maana ametutoka ghafla, ameacha pengo ndani ya
halmashauri yetu na katika kata yake, alikuwa mstari wa mbele katika
suala zima la uhimizaji wa maendeleo katika eneo lake ni wazi
tutamkumbuka daima,” alisema Nyamubi.
Marehemu
Masele alizaliwa mwaka 1973 wilayani Shinyanga na ameacha mjane mmoja
na watoto watatu a ambapo wakati akipata ajali hiyo alikuwa akitokea
Kata ya Isaka wilayani Kahama akirejea kijijini kwake Nyida.