HUU NDIO WARAKA WA LEMA ALIOMUANDIKIA RAIS KIKWETE, SOMA HAPA

Mh Rais nakusalimu. Kauli yako iliyonukuliwa na vyombo mbambali mbali vya habari wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wako wa NEC (CCM ) ni...

Mh Rais nakusalimu.
Kauli yako iliyonukuliwa na vyombo mbambali mbali vya habari wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wako wa NEC (CCM ) ni kauli hatari na yenye laana kubwa sana ya damu za Watu wengi katika Taifa letu . Ninaona wakati mgumu mwingine ambao Taifa letu linaingia kwa sababu ya kauli yako ambayo sasa imetangaza mauaji rasmi yatakayoongozwa na Viongozi mbali mbali wa CCM Nchi nzima huku Polisi wakiendelea kusimamia kama kawaida yao .

Mh Rais , Kwa mujibu wa maneno yako umethibitishia Umma wa Watanzania kuwa mmejadiliana kwenye kamati Kuu na kukubaliana kuwa sasa yale mambo mliyokuwa mnayafanya kwa kificho sasa yamethibitishwa na Kamati Kuu ya Chama chako na kutangazwa na wewe mwenyewe kuwa, kuumiza, kuua, kutesa na kudhalisha sasa imekuwa sera rasmi ya CCM na umeithibitisha kauli hiyo mbele ya Wajumbe wa Baraza Kuu la CCM ( NEC)

Mh Rais , kwa kauli hii naomba nikuambie kuwa umeamua kumalizia kipindi chako kwa mikono iliyojaa Damu na Roho za Watu . Nafasi uliyonayo ni kubwa sana sio jambo jepesi kuona makosa makubwa au madogo na kutubu , wapambe ni wengi ambao kwa kumsifu Mfalme hata kwa ujinga maisha yao na ya watoto wao yataendelea kuwa bora , lakini nakuhakikishia kwa kauli hii iko siku utajuta na kulaani ni kwanini ulitoa kauli mbaya na yenye hatia kama hii kwa Kiongozi mkubwa wa Nchi kama wewe . Vijana wa CCM sasa wamejipanga kuua na kuchinja hadharani kama ambavyo umeagiza wafanye na Polisi watakuwa Kimya kabisa kama ambavyo siku zote wamekuwa lakini mara hii watasaidia wazi wazi kabisa unyama wote utakaofanywa kwani wao pia wamesikia Amri yako na wewe ndio Mkuu wa Nchi hii .

Mh Rais , mambo mengi yanachangia kuvurugika kwa Amani lakini moja kubwa ni pale Polisi na Mahakama zitakaposhindwa kutenda wajibu wake katika kutenda haki haswa pale uonevu unapokuwa dhahiri . Naweza kutambua matendo yote mabaya yanayotokea wakati wa Uchaguzi kuwa yamesababishwa na Upendeleo wa Jeshi la Polisi kwa Wanachama wa CCM pindi wanapofanya uhalifu dhidi ya wenzao wa Vyama Vingine vya Siasa . Mwaka jana 2013 wakati wa uchaguzi wa marudio wa Madiwani wa kata nne Arusha Mjini watu zaidi ya 16 waliumizwa vibaya na Green Guard na matukio yote yaliripotiwa lakini mpaka leo hakuna Mtu aliyefikishwa mahakamani kujibu mashitaka , lakini unakumbuka na unajua kuwa mkutano wetu wa kufunga Kampeni hizo za Udiwani ulipigwa BOMU na Watu Wanne waliuuwa na Zaidi ya 100 kuumizwa vibaya na wengine wamebaki na Vilema hata leo na tumekuomba uunde tume ya Kimahakama ili tukuletee Wauaji wa watesaji wa tukio hilo lakini mpaka leo umegoma na badala yake zimekuwepo jitihada nyingi zinazofanywa na Jeshi la Polisi kubambikia Watu kesi nikiwemo mimi na kutesa watu kwa kiwango ambacho hakielezeki .

Mh Rais , Watu wameteswa na wanaendelea kuteswa sana katika Nchi hii na kazi hiyo inafanywa na Polisi na ccm na hapa ndipo mashaka katika jamii yanatokea na Jamii kuona ulinzi wao huko mikononi mwao na sio mikononi mwa Polisi na sheria za Nchi . Sasa umetangaza Watu wapigwe na wachinjwe hadharani , jambo ambalo nina uhakika nalo ni kwamba umeamua kuangamiza Nchi uliyoapa kuitetetea na ulioagiza wapigwe sina uhakika kama watakua wamelala chini wakati wanapigwa au wamefumba macho wakati wanateswa na kama itakuwa kinyume maana yake kutatokea Ugomvi ambao madhara yake mimi kwa sasa sielewi ila wewe MKUU uliyotoa amri utakuwa unajua .

Mh Rais , Wewe wewe ndiye Amri Jeshi Mkuu umeshindwa kuamrisha Polisi walinde Raia na mali zao na sasa umeamua Watu wachinjane ? kwa kauli hii unasubiri nini Ikulu ? Hata hivyo Nguvu ulizonazo sio Imara sana kama Nguvu alizonazo Mwenyezi Mungu . Mateso na Damu iliyomwagika katika Taifa hili kwa uzembe wa utawala wako hakika utalipa kama sio wewe Watoto wako na Wajukuu zako elewa kuwa hakuna dhambi itakayopita bila kulipwa . Kauli yako hii inaleta hofu kubwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015 lakini hatutaogopa kufanya kampeni kwa sababu Rais ameruhusu tupigwe na tuchinjwe , tutasonga mbele kutafuta haki tunayoamini kama ambavyo pamoja na matangazo mengi ya malaria kuua lakini hatujawahi kutembea huku tumevaa chandarua .

Mh Rais wewe sio Mungu , hata hivyo unamkumbuka Jean Kambanda aliyekuwa Waziri Mkuu wa Rwanda mwaka 1994 alishatakiwa kwa kutoa kauli kama yako na kugawa mapanga kwa Vijana wa Nterahamwe na kusababisha mauaji makubwa sana Rwanda na tarehe 18/7/1997 alikamatwa Nairobi na baadae alishitakiwa na kufungwa Maisha kwenye mahakama ya ICTR Arusha na hii ilikuwa tarehe 4 sept 1998 , sikufundishi uoga hata kidogo ila ni muhimu kujadili historia muhimu kulingana na wakati .

 Mh Rais thamani yako haitatokana na kusababisha CCM iwe madarakani tena bali Haki kuwa madarakani katika kipindi ulichotawala ni hekima ngumu kuielewa lakini ni lazima tuiseme . Tunaenda Kalenga kupigwa na kuchinjwa kwa sababu tu umewapa Watu wako ujasiri wa kufanya hivyo lakini elewa kuwa kila tukio litakalosababishwa na kauli zako ni tukio ambalo utalipa gharama zake . Makala zangu kama hizi uwezi kuzipenda sana Mh Rais , Wapambe watakuambia huyu kijana ni muhuni na maneno mengi ya kejeli lakini elewa kwamba anayekupenda ni anayekuambia ukweli , kwani ukweli thamani yake ni kubwa mno hata kama una madhara ya muda .

Mh Rais , Ninapata hofu ninapoandika waraka huu kwani kama ni kwazo basi unaweza kuamua kufanya chochote dhidi yangu lakini napata faraja kuwa kifo kipo tu hata kama utafuti haki na ukweli kwani Bibi yangu kule Machame hakufa kwa kuwa aliandika waraka bali ni umri tu ulimuondoa . Mh Rais ukweli nakuambia usipofuta kauli yako yenye lengo baya kwa Nchi yetu basi nimemuomba Mungu afanye jambo muhimu dhidi yako na jambo hilo muhimu liko wazi kuwa kama wewe ni chanzo cha Taifa kuharibika kwani nini anaendelea kukupa pumzi ? Hapa nitaonekana muhuni tena lakini Mh Rais wema wako ni katika haki na sio sifa .

Mwisho , Mh Rais , Mamlaka yana tabia ya kudanganya akili nikuombe Rais wangu usikubali mamlaka ikudanganye hata kidogo , futa kauli yako , watakaokuona mjinga wao ndio wajinga . Najua Polisi na Jeshi wanakutii wewe lakini Dhambi na hila iko mbali na MUNGU .

Godbless Lema (Mb)

Related

OTHER NEWS 6379038877857728342

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item