MEMBE, TULIKAANGWA, TULIULIZWA MASWALI MAGUMU URAIS 2015

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amesema aliulizwa maswali mazito na Kamati Ndogo ya Maadili ...

Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amesema aliulizwa maswali mazito na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula kuhusu mbio za urais 2015.
Akizungumza jana mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, Membe alisema kamati hiyo inauliza maswali magumu kuhusu wanayoyafanya pamoja yanayofanywa na mashabiki wao.
“Kamati inauliza maswali mazito na magumu yanayohusiana na uvunjaji wa maadili ya uongozi wa chama chetu… Kamati ya maadili imejipanga vizuri sana wala msidanganyike, wanauliza maswali mazito,” alisema Membe.
Membe aliongeza kusema aliulizwa mambo makubwa matatu, kubwa likiwa ni kuibuka ghafla kwa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila wakati chama hicho kinapokaribia kwenye uchaguzi wa Rais.
“Kuna mambo makubwa matatu ambayo kamati ya maadili imeyauliza. Kubwa kabisa ni uzukaji ghafla wa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila wakati wanapodhani mtu fulani anafaa kuwa kiongozi.”
Alisema na kuongeza: “Suala la pili nililoulizwa ni tunafanyaje kukifanya chama chetu kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani kwenye uchaguzi?”
Suala la tatu ambalo wajumbe wa kamati hiyo wanauliza ni suala la fedha, kama msingi wa ushindi na kuhoji inakuwaje mtu atumie mamilioni au mabilioni ya shilingi kununua uongozi?
Membe alisema hayo ndiyo maeneo matatu ambayo kamati hiyo ya maadili imekuwa ikiyauliza na kusema kuna uwezekano mkubwa wa wanachama zaidi kuitwa kuhojiwa.
Alisema alitumia fursa hiyo kukishauri chama mambo kadha wa kadha ikiwamo CCM kufanya mchakato wa kumteua mgombea au wagombea urais mwaka huu ili waweze kujulikana kabla ya Desemba.
Kamati hiyo ya ndogo ya Maadili ya CCM iliyoanza kikao chake Alhamisi iliyopita, imewahoji makada sita wa chama hicho ambao wamekuwa wakitajwa kuanza kutangaza nia za kuwania kupendekezwa kupeperusha bendera yake kwenye kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Tayari kamati hiyo imeshawahoji Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa wanakivuruga chama kwa kuonyesha nia ya kuwania urais kabla ya muda ulioruhusiwa na chama hicho.
Pia kikao hicho kimewahoji Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Membe aliyeingia kwenye kikao hicho, saa 3.15 asubuhi na kutoka saa 5.00 asubuhi, alisema anaona kuna haja sasa kwa CCM kufanya uteuzi wa mgombea au wagomba ili kutoa nafasi kwa watu hao kujitangaza na kujipambanua kuwania urais.
“Nadhani sasa chama kinabidi kichague mgombea anayefaa kuwa kiongozi au nani wanafaa kuwa viongozi ili ifanyike midahalo wananchi wajue tunapokwenda mwaka 2015 mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ni nani? Inatakiwa afahamike mapema,” alisema na kuongeza:
 “Lazima tufike hapo, tukiacha kila mwanachama aombe, kila binadamu anayejiona anavaa nguo ya kijani na ana hela aombe uongozi tutakiangusha chama chetu. Kwa hiyo nadhani mwelekeo sasa ni wa kushauri na watu kama sisi tunashauri kwamba ni vizuri chama sasa kikajipanga kiwe na candidate (mgombea) kwa ajili ya 2015.
“Yaani kiwe na watu ambao wapitishwe ili tunapofika kwa mfano Desemba, CCM kinajua nani anachukua bendera kwenye uchaguzi wa mwakani ili chama chetu kiwe kimoja kisimegukemeguke.”
Membe ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, alisema iwe ni mwiko kwa mtu yoyote ndani ya chama hicho kutumia fedha, kama nguzo ya ushindi wake.
Alisema uongozi wa taifa hauwezi kununuliwa kwa fedha na kwamba jambo hilo ndilo Kamati ya Maadili imekuwa ikikemea na yeye anajiunga nayo kulikemea.
Membe alisema Kamati ya Maadili inauliza maswali magumu kwa watu wanaosemwa kuwa viongozi na ndiyo inayosikiliza ushauri ili CCM iende kwenye uchaguzi mwakani ikiwa imara na yenye mshikamano.
Alisema kama CCM itazingatia ushauri wake huo, inaweza kushinda kwa miaka 60 ijayo.

MWANANCHI.

Related

OTHER NEWS 9137273634211228280

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item