SERIKALI KUTAJA BEI ELEKEZI ADA ZA SHULE ZA MSINGI

KILIO cha siku nyingi cha wazazi kuhusu ada za shule za msingi na sekondari, kimesikika na hivi karibuni Serikali itakuja na jibu la k...

KILIO cha siku nyingi cha wazazi kuhusu ada za shule za msingi na sekondari, kimesikika na hivi karibuni Serikali itakuja na jibu la kudhibiti ada hizo. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, amesema hayo jana wakati alipozindua mfumo wa ada elekezi kwa vyuo vya elimu ya juu nchini. Amesema kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kuja na bei elekezi ya ada kwa ajili ya shule za msingi na sekondari.

Akizungumzia mfumo huo utakavyoanza kufanya kazi katika vyuo vya elimu ya juu, Dk Kawambwa alisema utasaidia wanafunzi, wazazi na wafadhili kujua ada halisi kwa kozi husika za wanafunzi. Mfumo huo pia unatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji mikopo kwa wanafunzi unaofanywa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

“Kuzinduliwa kwa mfumo wa gharama halisi ya mafunzo ya elimu ya juu, kutatufanya mimi na Mchome (Profesa Sifuni), kulala usingizi, kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kuja na mfumo kwa ajili ya shule za msingi na sekondari,” alisema.

Mfumo wa gharama halisi ya masomo kwa mwanafunzi wa elimu ya juu, unajumuisha gharama zote za kuendesha kozi husika kwa mwaka. Gharama hizo zitakokotolewa kwa kuzingatia gharama za mishahara ya wafanyakazi wote wa chuo husika, gharama zingine za kozi na huduma nyingine.

Aidha, kuanza kutumika kwa mfumo huo, kutasababisha gharama kwenye baadhi ya vyuo kupungua au kuongezeka kidogo, kulingana na aina ya chuo, gharama za uendeshaji, aina ya kozi na idadi ya wanafunzi.

Kwa mfano katika vyuo vya Serikali ambavyo baadhi ya gharama zinabebwa na Serikali, wanafunzi watakuwa na nafuu zaidi, kwa kuwa sehemu hiyo ya gharama inayolipwa na Serikali, itatolewa katika sehemu ya ada.

Dk Kawambwa alisema kutokana na mchakato huo kuwa na wigo mpana wa ushirikishwaji wa wadau, ana imani kuwa utatekelezwa kikamilifu na wadau hao.

“Ni imani yangu kuwa mfumo utatumika kama mwongozo kwa Serikali na taasisi za elimu ya juu nchini katika kubuni na kuamua gharama za kuendesha programu na kuweka ada moja.

“Hii itapunguza au kuondoa kabisa malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu gharama za elimu ya juu hapa nchini.”

Aidha, Kawambwa alisema Serikali inaelewa changamoto za kifedha zinazokabili taasisi za elimu ya juu na kuzitaka taasisi hizo kutafuta vyanzo vingine vya fedha, badala ya kutegemea Serikali na ada.

Dk Kawambwa pia alizitaka taasisi za elimu ya juu, kuwa makini katika matumizi katika shughuli za kila siku ikiwa ni pamoja na kutumia rasilimali kwa mambo ambayo yanaleta faida na kuwa na utawala mzuri wa fedha.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Magishi Mgasa, alisema mfumo huo ambao mchakato umefanywa na wataalamu wazawa, umepitia hatua mbalimbali na kushirikisha wadau wa elimu ya juu katika kila kozi.

“Baada ya kukamilika kwa mfumo huu, ni lazima taasisi za elimu ya juu zitapitia upya suala zima la ada katika kozi husika,” alisema. Alisema kwa sasa TCU ina kazi ya kutoa elimu kwa taasisi za elimu ya juu, ili watumie mfumo huo kikamilifu katika taasisi zao na kupitia upya ada katika mwaka ujao wa fedha.

Aidha, Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam, Profesa Uswege Minga, alisema kuanzishwa kwa mfumo huo kunaziondoa kwenye giza taasisi za elimu ya juu husa zile za binafsi kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya kutoza ada kubwa. “Ninamini katika kupitia mchakato huu mmezingatia utoaji wa elimu bora,” alisema.
 
HABARILEO

Related

ELIMU 2105380932511468212

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item