BUNGE LA KATIBA KUAHIRISHWA APRILI 28
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, jana alikutana na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikirstu, kuzungumzia msugua...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/04/bunge-la-katiba-kuahirishwa-aprili-28.html
Asubuhi alikutana na kiongozi wa Kanisa
Katoliki, Muadhama Kadinali Pengo katika kanisa la la Mt.Joseph jijini Dar es
Salaam na baadae akakutana na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban
Simba katika ofisi za Bakwata.
Mazungumzo yao yalijikita zaidi katika
mchakato wa bunge la katiba unaosuasua kutokana na misimamo ya kisiasa na
kuwaomba viongozi hao kuuombea mchakato huo ukwamuke.
Akizungumza na Sheikh Shaaban bin Simba,
Sitta, alisema katiba mpya ni kwa manufaa ya wanachi wote kwa ajili ya
kuwaletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Alisema viongozi wa dini ni watu muhimu
kwakuwa wanabeba wafuasi wengi katika jamii na kuwepo kwao kunasaidia katika
maendeleo ya nchi hususani kujenge amani na kuwahamasisha wananchi kuwa
wavumilivu, watulivu,waelewa na wenye kupenda amani.
“Namuomba Mhe.Mufti Shaaban bin Simba pamoja
viongozi wengine wa dini wazidi kutuombea ili tuweze kufikia muafaka katika
kupata katiba mpya na bora yenye kuleta mabadiliko katika nchi yetu,” alisema.
Aidha alisema Watanzania wanataka katiba
itakayojenga taasisi imara zitakazosimamia mambo muhimu na kuondokana na
uhalifu ikiwemo janga la dawa za kulevya ambalo limekuwa likiisumbua nchi.
Aliwaomba wajumbe wa kamati 12 za bunge la
katiba, wasome kwa makiini ibara ya sura ya 1 na ya 6 ambazo ni muhimu katika
kujenga nchi, ili waweze kutoka na mawazo mazuri na yakinifu kwa manufaa ya nchi na watu wake.
“Katiba itunge sheria ambazo ni imara zenye
kufuata kanuni na taratibu dhabiti ili kuleta mabadiliko katika kuiongoza nchi
na kuweza kuwasaidia wananchi wake,” alisema.
Aidha, alisema bunge hilo linatarajia kuahirishwa
Aprili 28 kwa ajili ya kupisha bunge la bajeti na kwa kuwa siku 70 hazitoshi kumaliza bunge hilo amemuomba
Rais kuwaongezea muda hivyo wanatarajia kurudi tena mwezi wa Ogasti kuendelea
na mijadala ya katiba mpya.
Akizungumza na Kadinali Pengo, Sitta alimuomba kuliombea bunge ili kufikia muafaka na kutoka na katiba mpya na bora yenye kuleta mabadiliko.