UFAFANUZI ZAIDI KUHUSU MATANGAZO YA KAZI KUTOKA SEKRETARIETI YA AJIRA
Waombaji wa fursa za ajira Serikalini kupitia Sekretarieti ya Ajira wametakiwa kuweka kumbukumbu sahihi za matangazo ya kazi wanazozio...
Hayo yamesemwa na Bw. Lucas Mrumapili ambae ni Naibu Katibu wa Idara ya Ajira katika Sekretarieti ya Ajira wakati akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya wasailiwa waliofika ofisini kwake ili kujua majina ya kuitwa kwenye usaili wa nafasi za kazi za PPRA utafanyika lini.
Mrumapili amesema kwa tangazo la tarehe 30 Desemba, 2013 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 13 Januari, 2014 kuwa mchakato wake bado unaendelea kutokana na kuhitaji uchambuzi wa kina kwa kila kada maana baadhi ya waombaji kazi wa tangazo hilo kujirudia zaidi ya mara mbili.
Aliongeza kuwa kwa tangazo la kazi la tarehe 23 Januari ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 6 Februari, 2014 kuwa usaili wake nao utafanyika mwisho mwa mwezi Aprili mwaka huu. Aidha, aliwataka waombaji wa nafasi iliyokuwa imetangazwa kwa ajili ya TACAIDS kuwa nafasi hiyo mchakato wake ulisitishwa kutokana na nafasi hiyo kujazwa kwa kibali cha ajira mbadala, hivyo ofisi yake inaomba radhi kwa usumbufu ulijitokeza kwa waombaji wa nafasi hiyo.
Pia amefafanua kuwa kwa waombaji wa tangazo la tarehe 17 Februari, 2014 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 3 Machi, 2014 mchakato wake nao uko katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuitwa kwenye usaili.
Mwisho amewataka waombaji wote wa fursa za ajira Serikalini kufuatilia taarifa zinazowekwa katika mtandao wa Sekretariti ya Ajira ili kupata ufafanuzi sahihi kadri unavyotolewa kila mara, kuliko kutegemea taarifa za kusikia kutoka kwa baadhi ya watu ambazo wakati mwingine huwa za kupotosha.
Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kwa barua pepe; gcu@ajira.go.tz na Facebook-page ya “Sekretarieti Ajira”
au simu 255-687624975
15 Aprili, 2014