Shirika la "Tanzania Sisi kwa Sisi Foundation (TSSF)" LAFUTIWA USAJILI kwa tuhuma ya kujihusisha na kuhamasisha ushoga nchini
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imelifutia usajili Shirika la Tanzania Sisi kwa Sisi Foundation (TSSF), kwa tuhuma ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/04/shirika-la-tanzania-sisi-kwa-sisi.html
WIZARA
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imelifutia usajili Shirika la
Tanzania Sisi kwa Sisi Foundation (TSSF), kwa tuhuma ya kujihusisha na
kuhamasisha ushoga nchini.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali wizarani, ilieleza kuwa shirika hilo limefutiwa usajili
kuanzia Aprili 4, mwaka huu.
Ilieleza kuwa kufungiwa huko, kunatokana na kukiuka masharti ya Sheria
ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002 na sheria mbalimbali za
nchi.
“Taarifa inatolewa kwa umma kuwa shirika la Tanzania Sisi kwa Sisi
Foundation (TSSF) lililosajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali mwaka 2011, limefutiwa usajili kuanzia tarehe 04.04.2014
kutokana na kukiuka masharti ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
ya mwaka 2002 na sheria mbalimbali za nchi.Kwa taarifa hii, utendaji
kazi wa shirika hili unasitishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali Namba 24 ya mwaka 2002 na utendaji kazi wake baada
ya taarifa hii, utakuwa ni kinyume cha sheria,” ilieleza taarifa hizo ya
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Mmoja wa viongozi wa wizara hiyo, alieleza kuwa shirika hilo limefungiwa
kutokana na vitendo vya ushoga, lakini hana taarifa zaidi na kutaka
watendaji waulizwe.
Baada ya taarifa hiyo, mtu mmoja ambaye namba zake zinaonekana katika
mtandao wa kijamii wa shirika hilo, ukielekeza wanaume wanaojihusisha na
vitendo vya kishoga kumuandikia taarifa kwa ajili ya semina,
alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, kwamba wamefutiwa leseni alisema hawana
taarifa.
Akizungumza na habari leo, mtu huyo aliyesema ofisi zao ziko Ilala
jijini Dar es Salaam, aliyekataa kutaja jina lake, alisema hawajapewa
barua ya kusitisha huduma zao, hivyo wataendelea na huduma zao mpaka
wapewe taarifa.
Mtu huyo ambaye awali alijitambulisha kwa jina la Dk John, ambaye namba
zake zinaonekana katika maelezo ya taasisi hiyo katika mitandao, alisema
hana taarifa zozote na yuko nje ya nchi.
Alisema namba hiyo ni kwa ajili ya huduma za wateja. Alisema hajaliona tangazo wala hana taarifa.
Hivi karibuni katika mitandao ya jamii, watu kadhaa walililalamikia
shirika hilo, lililosajiliwa na serikali kujihusisha kudai haki, wakidai
linahamasisha ushoga nchini. Mtandao wa kijamii wa shirika hilo, una
tangazo linalowaalika wanaume wanaojihusisha na vitendo hivyo.
"Je, wewe ni mwanaume unayejihusisha katika mapenzi ya jinsia moja?TSSF
inakualika katika semina fupi, itakayofanyika kesho Ijumaa ya tarehe 21
Februari 2014 kuanzia saa 4 asubuhi.
“Mada zitakazoongelewa ni: Magonjwa ya ngono yanayowaathiri kuchu; Namna
ya kujilinda na magonjwa hayo, Kujiepusha na magonjwa hayo na tiba. Kwa
maelezo ya jinsi ya kuhudhuria tupigie katika 0752648253 au tutumie
meseji.