JAJI MUTUNGI: SINA MAMLAKA NA UKAWA

Jaji Francis Mutungi   Na Waandishi wetu Msajili  wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema kwamba Umoja wa Katiba ya Wa...

Jaji Francis Mutungi
 
Na Waandishi wetu
Msajili  wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema kwamba Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) siyo chama cha siasa, hivyo hauko chini ya ofisi yake.Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo wakati kukiwa na kauli za kuitaka ofisi yake ichukua hatua dhidi ya Ukawa kwa madai kuwa inajihusisha na siasa bila kuwa na usajili.

Miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali aliyetoa kauli hiyo ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyemtaka msajili huyo kuchunguza kama Ukawa imesajiliwa kama chama cha siasa au shirika lisilo la kiserikali.

Balozi Iddi akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Zanzibar, alisema msajili akibaini kuwa Ukawa haijasajiliwa kufanya shughuli za kisiasa, ifutwe.

Jaji Mutungi aliliambia NIPASHE jana kwamba, Ukawa siyo chama cha siasa na kama kingekuwa chama wangepeleka maombi ya kusajiliwa katika ofisi yake, lakini yeye hajapokea maombi yoyote yaliyopelekwa na umoja huo wakiomba kusajili kama chama cha siasa. 

“Hatujaletewa maombi, lakini mimi kama msajili wa vyama vya siasa naona kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kuhusiana na suala la jinsi hii. Hicho siyo chama cha siasa,” alisema Jaji Mutungi.

Aidha, alipohojiwa iwapo katiba inaruhusu ushirika au umoja wa vyama vya siasa kama ilivyo kwa Ukawa, alisema, haizuii isipokuwa kama umoja huo unavuka mipaka na kufanya kazi za vyama vya siasa ambavyo vinapaswa kusajiliwa na yeye kabla havijaruhusiwa kuingia kwenye siasa, atapaswa kuingilia kati na kuwaita viongozi wahusika ili kuhojiwa.

KAULI YA MBATIA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye chama chake kinaunda Ukawa sambamba na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF), alisema Msajili wa Vyama vya Siasa au kiongozi yeyote akiwamo Balozi Iddi, hawana mamlaka ya kuhoji uhali wa uwapo wa ushirikiano baina ya vyama kama ilivyo kwa Ukawa.

Mbatia alisema hakuna sheria wala sera inayovizuia vyama vya siasa kushirikiana na kwamba wanachokifanya wao kupitia Ukawa ni kuwaunganisha wananchi na kutetea haki yao ya kupata katiba wanayoitaka.

“Sisi tunafanya mambo yetu waziwazi, tunahubiri umoja na maridhiano kwa wananchi. Tulipokuwa Dodoma tulikuwa tukiendesha vikao vyetu wazi wazi katika ukumbi wa Pius Msekwa na kila mtu alikuwa anasikia, lakini wao (Tanzania Kwanza) walikuwa wanaendesha vikao vyao kwa siri,” alisema na kuongeza:

“Wao wanahubiri chuki, kugawa umoja wa kitaifa Zanzibar, wanahubiri jeshi kushika hatamu za uongozi na hapo ndipo wanapothibitisha udhaifu tuliousema.”
Aliongeza kuwa Balozi Iddi kwa nafasi yake hapaswi kuzungumzia suala kama hilo kwa kuhoji uhalali wa Ukawa na kumtaka msajili wa vyama vya siasa achunguze uhalali wake iwapo umesajiliwa.

JUSSA ANENA KUHUSU URAIA
Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, amemtaka Balozi Iddi kuthibitisha kwa kutumia vielelezo halali kuhusiana na kauli yake aliyoitoa juzi katika mkutano wa hadhara kuwa yeye (Jussa) si Mzanzibari.

Jussa alisema jana kuwa anayetaka uhalali wa uraia wake aende Idara ya Uhamiaji ajiridhishe na ikiwa hataridhishwa na vielelezo hivyo, amtafutie uraia na kumpeleka nchi anayostahili kuishi. Juzi Balozi Iddi alisema Jussa hana imani na Wazanzibari na amejivisha koti la Zanzibar wakati siyo Mzanzibari.

Alisema anayo mengi ya kueleza kuhusu Jussa, lakini kutokana na muda kutotosha atamzungumzia katika mkutano mwingine.

 “Hayo ni maneno ya wanasiasa wasio na hoja hoja za kusema, atazusha kila jambo,” alisema Jussa.  Alisema  Balozi Seif hapaswi kutoa kauli kama hizo zenye tuhuma nzito kutokana na nafasi aliyonayo.

 Kuhusu kauli ya Balozi Iddi ya kutaka Ukawa ifutwe, Jussa alisema msajili wa vyama vya siasa hana uwezo wa kuifuta Ukawa kwani siyo chama cha siasa bali ni umoja wa vyama vya upinzani.

 “Vyama vya siasa ndivyo vinavyosajiliwa, siyo umoja hata nchini India upo umoja wa vyama vya siasa (UPA) ambao ni kama Ukawa,” alisema Jussa.
“Nasema wataendelea kuweweseka, lakini Ukawa bado utaendelea na shughuli zake na hautarudi nyuma,” alisema Jussa.

ZEC YAZUNGUMZA
NIPASHE ilipoiuliza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa inakuwaje mtu ambaye si raia anaruhusiwa kugombea ubunge au uwakilishi, Kaimu Mkurugenzi wa ZEC, Idrisa Jecha, alisema ofisi yake haina mamlaka  ya kuthibitisha uraia wa Mzanzibari.

 Hata hivyo, Jecha alisema vigezo inavyoviangalia kabla ya kumpitisha mgombea ni kukubalika katika chama chake na kujaza fomu ya maaelezo na kuambatanisha nakala ya kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi.

Jecha mbaye pia ni AOfisa Habari wa ZEC, alisema kama ni vigezo hivyo, Jussa alivitimiza wakati anagombea uwakilishi wa jimbo lake kupitia CUF mwaka 2010. 

Chanzo : Nipashe

Related

OTHER NEWS 5859941920571054365

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item