Majaji EACJ waruhusu Spika Eala kung’olewa
Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Dk Magreth Zziwa Arusha. Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Dk Magreth Zziwa a...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/05/majaji-eacj-waruhusu-spika-eala.html
Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Dk Magreth Zziwa
Arusha.
Spika wa Bunge la
Afrika Mashariki (Eala), Dk Magreth Zziwa amekalia kuti kavu kutokana na
uwezekano wa kung’olewa madarakani baada ya Mahakama ya Afrika
Mashariki (EACJ), kuruhusu bunge hilo kuendelea na shughuli zake
kulingana na kanuni na taratibu zake.
Jopo la majaji watatu wa EACJ, wakiongozwa na Jaji
Mfawidhi Jean-Bosco Butasi lilitupilia mbali maombi ya zuio la muda
kuhusu Kanuni za Bunge zinazohusu suala la kumwondoa madarakani spika
lililowasilishwa na Taasisi ya Mbidde Foundation Ltd ya nchini Uganda na
Spika Zziwa mwenyewe.
Wabunge wa Eala wanataka kumng’oa Spika Zziwa kwa
madai ya kupendelea makundi na dharau miongoni mwa wabunge, matumizi
mabaya ya madaraka na kushindwa kumudu majukumu yake.
Mwanzoni mwa Aprili, bunge la Eala lilivunjika
baada ya kuibuka malumbano kati ya makundi mawili yanayosigana, moja
likitaka kumng’oa Spika na jingine likimtetea.
Zziwa ni Spika wa tatu wa bunge la Eala na wa
kwanza mwanamke kukalia kiti hicho. Spika wa kwanza alikuwa Abdulrahama
Kinana wa Tanzania aliyefuatiwa na Abdirahin Haithar Abdi kutoka Kenya.
Katika uamuzi wao wenye kurasa 16, Jaji Butasi na
wenzake, Jaji Isaac Lenaola na Jaji Monica Mugenyi walisema baada ya
kupitia hoja za pande zote mbili za wadai na wadaiwa, mahakama
imejiridhisha kuwa wadai wa kwanza na wa pili, hawatapata madhara
makubwa iwapo zuio la muda lisipotolewa.
Madai ya msingi yaliyopo mbele ya mahakama katika
maombi yao ya msingi, taasisi ya Mbidde Foundation Ltd na Spika Zziwa
wanaiomba mahakama kutoa ufafanuzi kuhusu uhalali wa kanuni na taratibu
za uendeshaji wa Bunge la Eala wakijielekeza katika kanuni ya tisa
inayoelekeza jinsi ya kumwondoa madarakani Spika wakidai zinakiuka
baadhi ya vifungu vya katiba ya kuanzishwa EAC.
Mdaiwa wa kwanza katika shauri hilo ni Katibu Mkuu
wa EAC, Dk Richard Sezibera anayewakilishwa na Mawakili Wilbert Kaahwa
na Stephen Agaba, wakati Mwanasheria Mkuu wa Uganda, ambaye ni mdaiwa wa
pili akiwakilishwa na jopo la mawakili watatu, Christine Kaahwa, Oburu
Odoi na Madete Geofrey.
Wabunge wa Eala wameanza utaratibu wa kumwondoa
madarakani Spika kwa kuwasilisha hoja iliyosainiwa na wabunge zaidi ya
wanne kutoka kila nchi mwanachama.