RAIS GOODLUCK JONATHAN WA NIGERIA AAHIDI WASICHANA WALIOTEKWA NYARA KUWA WATAPATIKANA
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amezungumza wazi kwa mara ya kwanza kuhusu kutekwa kwa waschana takriban 200 wa shule kaskazini ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/05/rais-goodluck-jonathan-wa-nigeria.html
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amezungumza wazi
kwa mara ya kwanza kuhusu kutekwa kwa waschana takriban 200 wa shule
kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Katika taarifa yake ya kwanza hadharani tangu
wasichana 200 kutekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa
Waislamu wenye itikadi kali wa Boko Haram, Rais Goodluck Jonathan,
amesema kuwa kila juhudi zinapaswa kufanywa kuwakomboa wasichana hao.
Tangazo la Rais lilitolewa kufuatia
shinikizo zilizotolewa na familia, makundi ya wanawake na watu wengine
ambao wameitaka Serikali kufanya bidii zaidi kuhakikisha kuwa wasichana
hao wanakombolewa.
Rais alisema kuwa maafisa wa usalama wamekuwa
wakitafuta kila mahali wakitumia ndege na helikopta lakini akakiri kuwa
hawajafaulu kutambua walikofichwa wasichana hao.
Alisema kuwa Serikali yake imelazimika kuomba
msaada katika kuwatafuta wasichana hao kutoka Serikali za Marekani,
Uingereza na Uchina.
Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana na kundi
hilo la wapiganaji tangu mwaka 2009, lakini mashambulizi na milipuko ya
mabomu yameendelea kusikika kila mahali bila kukoma.
Hivi majuzi kumekuwa na milipuko katika mji mkuu
wa Abuja katika muda wa majuma matatu ambapo karibu watu 90 waliuawa na
wengine wengi kujeruhiwa.
Mnamo Jumatano Kongamo la Dunia juu ya Uchumi wa
Afrika utafanyika mjini Abuja na swala la usalama limewatia maafisa wa
usalama tumbo joto, ambapo imetangazwa kuwa siku hiyo shule zote na
afisi za Serikali zitafungwa ili kuimarisha usalama eneo hilo la
mkutano.