RIPOTI YA CAG KUZIGUZA CHADEMA, CCM
Dar es Salaam. Bunge la Bajeti linaanza vikao vyake mjini Dodoma na moja ya kazi zake zitakazovuta hisia za wengi ni Ripoti ya Mwaka...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/05/ripoti-ya-cag-kuziguza-chadema-ccm.html
Dar es Salaam.
Bunge la Bajeti linaanza vikao vyake mjini Dodoma na moja ya kazi zake zitakazovuta hisia za wengi ni Ripoti ya Mwaka 2012/13 ya Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali itakayowasilishwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Bunge la Bajeti linaanza vikao vyake mjini Dodoma na moja ya kazi zake zitakazovuta hisia za wengi ni Ripoti ya Mwaka 2012/13 ya Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali itakayowasilishwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Pia, ripoti hiyo itakayowasilishwa keshokutwa
baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, kwa mara ya
kwanza itahusisha hesabu za vyama vya siasa nchini ambavyo kwa muda
mrefu vimekuwa vikidaiwa kutofanya ukaguzi wa hesabu zake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe alithibitisha kuwasilishwa kwa ripoti hiyo
keshokutwa na kuongeza kuwa kila mbunge atapatiwa nakala yake. “Baadaye
mchana, CAG atafanya mkutano na waandishi wa habari kufafanua yaliyomo
katika ripoti hiyo. Katika mkutano huo nitakuwepo mimi na mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC),” alisema Zitto.
Mwaka 2012, Ripoti ya PAC iliyowasilishwa na CAG
ndiyo iliyokuwa chanzo cha kung’olewa kwa mawaziri wanane kwa tuhuma
mbalimbali. Ripoti hiyo iliibua ufujaji wa fedha na uingiaji wa mikataba
kiholela iliyofanywa na mawaziri hao na hivyo Bunge kushinikiza
wajiuzulu.
Mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ya 2012 ya
CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni William Ngeleja (aliyekuwa
Nishati na Madini), Omar Nundu (Uchukuzi) na Naibu wake Athuman
Mfutakamba. Wengine ni Mustafa Mkulo (Fedha), Ezekiel Maige (Maliasili
na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na naibu wake, Dk
Lucy Nkya pamoja na Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara).
Vyama vya siasa
Ripoti hiyo pia itakuwa mwiba mchungu kwa vyama
vya siasa ambavyo mwaka jana kwa nyakati tofauti Zitto alivinanga kuwa
hesabu zake hazikaguliwi.
Zitto alifikia hatua ya kusimamisha ruzuku ya kila
mwezi kwa vyama hivyo hadi vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa
fedha za umma tangu mwaka 2009 kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Katika
maelezo yake, Zitto alisema tangu mwaka 2009 vyama tisa vya siasa
vinavyopewa ruzuku na Serikali vilipata jumla ya Sh67.7 bilioni, lakini
havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa Msajili kama
inavyopaswa kisheria.
Madai hayo ya Zitto yaliibua malumbano makali kati
yake na viongozi wa vyama hivyo, kikiwamo Chadema, CUF na CCM ambavyo
vilidai kuwa vimekaguliwa na wakaguzi binafsi na kuwasilisha hesabu hizo
katika Ofisi ya CAG.
Sakata hilo liliingiliwa kati na Msajili wa Vyama
vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliposema kuwa hatazuia ruzuku ya vyama
vya siasa kutokana na mkanganyiko wa ukaguzi uliojitokeza na kwamba
kufanya hivyo itakuwa ni kukiuka sheria.
Uamuzi huo pia uliafikiwa na Kamati ya PAC ambayo
awali, ilimwagiza Msajili huyo kusimamisha ruzuku hiyo hadi hapo vyama
hivyo vitakapokuwa vimekaguliwa hesabu zao.
Mwananchi.