KESI YA KIKATIBA: PINGAMIZI LA AG DHIDI YA KUBENEA, WANASHERIA LATUPWA

DAR ES SALAAM Mahakama   Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana imetupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu ...


DAR ES SALAAM

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana imetupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya kesi ya kikatiba inayohoji uhalali wa Bunge Maalumu la Katiba iliyofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Said Kubenea.
Aidha, mahakama hiyo hiyo ilitupilia mbali pingamzi kama hilo lililowasilishwa na AG dhidi ya kesi ya kikatiba ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na hivyo kutoa kibali kwa chama hicho kufungua kesi ya kupinga vikao vya bunge hilo pamoja na mwenendo wa bunge hilo. Katika kesi ya Kubenea, Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Augustino Mwarija, wengine ni Aloysis Mujulizi na Dk Fauz lilitupilia mbali pingamizi la AG jana baada ya kukataa hoja zake na kupanga kesi hiyo ianze kusikilizwa leo asubuhi.

Kubenea alifungua kesi hiyo kupitia Wakili wake Peter Kibatala, akiomba Mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba, kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.
Aidha, anaiomba Mahakama itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa AG aliwasilisha pingamizi la awali akiomba Mahakama itupilie mbali kesi hiyo kwa kuwa imefunguliwa isivyostahili, hivyo haina mamlaka ya kuisikiliza.
Kesi ya TLS Jopo hilo lilitoa kibali kwa TLS kufungua kesi hiyo baada ya kutupilia mbali pingamizi la AG na kusikiliza ombi la wanasheria hao waliokuwa wakitaka Mahakama iwape kibali cha kufungua kesi.
Hata hivyo, jopo hilo lilikataa ombi la TLS la kutaka Mahakama imuamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wawasilishe bungeni muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Katiba.
Jopo hilo lilisema hakuna ushahidi kwamba waleta maombi waliwaomba wanasheria hao kuwasilisha muswada huo wakakataa.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata waliomba Mahakama isitoe kibali kwa kuwa ombi hilo halina msingi kisheria.
Aidha, alidai Mahakama haina mamlaka ya kutoa kibali hicho kwa kuwa ombi la TLS linahusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lakini sheria waliyoitumia kuwasilisha ombi hilo inatumika Tanzania bara pekee. Waliongeza kuwa kifungu cha sheria ya mabadiliko ya Katiba wanachoomba kirekebishwe kinahusu pande zote mbili na hawana uhakika kama wanasheria wa Zanzibar wamehusishwa, hivyo Mahakama haiwezi kutoa uamuzi unaozihusu pande zote mbili wakati upande mmoja haupo.
CHANZO: HABARI LEO

Related

OTHER NEWS 5419470528417062646

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item