ASKOFU WA KATOLIKI AELEZA NJIA MPYA KUZUIA KATIBA

Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi. MAKAMU   wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Ask...

Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi.

MAKAMU wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, amesema maoni yaliyotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) juu ya Bunge Maalumu la Katiba, hayajatekelezwa na hivyo watapita kwa Watanzania na waumini wao kuwaeleza nini cha kufanya.
Jukwaa hilo lilikutana Agosti 27 hadi 28, mwaka huu na kujadili hatima ya Bunge hilo na kutoa mapendekezo sita, moja ikiwa ni kusitishwa kwake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Niwemugizi  ambaye pia ni mjumbe wa TCF, alisema: “Tunaona Bunge bado linaendelea na Serikali iliyopo madarakani inaendelea na mipango yake, haiheshimu wala haitekelezi ushauri unaotolewa.
“Sauti nyingi haziridhiki na yale yanayotendwa na Bunge Maalumu la Katiba, hawajui ni kiasi gani Watanzania wameshapevuka na wanatambua haki zao.”
Alisema wamejipanga kurudi kwa Watanzania kuwafahamisha na kuwafundisha ili watambue haki na wajibu wao hali itakayowasaidia kujua njia sahihi ya kufanya.
“Wanaweza kutudharau kwamba sisi hatuna chochote, kwakuwa hawajali tuliyopendekeza, tutarudi kwa watu wetu tunaowaongoza, kitakachotokea hatujui.
“Sisi tunaamini kurudi kwa Watanzania ni sehemu pia ya injili kwa sababu kuna injili ya jamii, na tutawafundisha watambue haki na wajibu wao na namna sahihi ya kufanya,” alisema.
Askofu huyo alisema wanachotaka Watanzania ni kuona mambo yakienda vizuri, hivyo kama viongozi wanakataa ushauri unaotolewa, Watanzania wataamua cha kufanya.
Kuhusu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, askofu huyo alisema amejidhalilisha kwa kauli zake za kejeli ndani ya Bunge hilo.
“Mkishakuwa na viongozi wenye dharau na kejeli, hapo nchi imekwisha kabisa. Sitta amejidhalilisha kwa kauli zake, hasa ukizingatia kuwa na yeye anatajwa kutaka kugombea urais, sifa zake zinazidi kupungua,” alisema.
Jukwaa hilo linaundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Jumuiya ya Kikristo (CCT) na Makanisa ya Kisabato (SDA).
Tamko la jukwaa hilo lililotolewa Agosti 28, mwaka huu, lilisema mjadala wa Bunge hilo umeondoa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wao.
“Wamewezesha maoni na maslahi ya chama tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora,” inasema sehemu ya tamko hilo.
Kutokana na hali hiyo, jukwaa hilo lilitoa mapendekezo sita likitaka yafanyiwe kazi.
MAPENDEKEZO YA JUKWAA
1. Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.
2. Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.
3. Mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano mwafaka, Uchaguzi Mkuu na wa Serikali za Mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.
4. Baada ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.
5. Wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.
Tamko lilisema: “Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako, hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba mpya.
“Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya taifa letu.
“Ifahamike kuwa Wananchi wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe wananchi wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu chama hicho kimeyapuuza na kimekataa maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.
“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa.
“Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao. (Rejea Warumi 1: 28-32)
“Ikumbukwe kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba ni waraka halali na rasmi na ndiyo mawazo ya Watanzania na tunahimiza kuwa Katiba ni ya wananchi na inahitaji maridhiano na siyo ubabe.”
CHANZO: MTANZANIA

Related

TUJUZANE 5407329383359433876

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item