UFAHAMU UGONJWA WA UTI NA ATHARI ZAKE KWA BINADAMU

Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI) ni moja kati ya magonjwa ambayo hayapewi msisitizo wa kutosha katika jamii licha ya kuwa wengi hu...


Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI) ni moja kati ya magonjwa ambayo hayapewi msisitizo wa kutosha katika jamii licha ya kuwa wengi huathirika kwa ugonjwa huu bila kujua chanzo, tiba na kinga yake. 

Ugonjwa huu huanza kuathiri mirija inayopitisha mkojo, baadaye huenea katika kibofu na figo. Mgonjwa anaweza kupata ugonjwa sugu wa figo na kupoteza maisha kama ugonjwa huu hautatibiwa mapema. 

Wataalamu wa afya wanasema UTI husababishwa na vimelea ambao huingia kupitia mirija inayosafirisha mkojo na kuutoa nje. Vimelea hawa wanashambulia kibofu na baadaye huendelea mpaka kwenye figo. Hii ndiyo hatua kubwa ya ugonjwa ambayo inaweza kusababisha kifo au tatizo la kudumu. 

Hawa ni vimelea wa jamii ya bakteria walio wanajulikana kwa jina la escherichia coli (E.coli). 

Bakteria hawa wanapatikana katika utumbo mpana lakini husafiri kupitia njia ya haja kubwa kwenda katika njia ya mkojo na kusababisha maambukizi katika kibofu na figo. 

UTI inavyoenea 

Dk Veronika Kaniki kutoka hospitali ya Sekou Toure, anabainisha tabia na mazingira yanayoweza kusababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuwa ni kushiriki ngono mara kwa mara na watu tofauti bila kutumia kinga. 

Anasema hii inamfanya mtu kuchukua bakteria wa UTI kutoka kwa mwenzi wake ambaye tayari ana maambukizi hayo. 

Dk Kaniki anaongeza kuwa kujitawaza kutoka nyuma kuja mbele baada ya haja kubwa kunapelekea maambukizi hasa kwa wanawake. 

Hii ni kwa sababu vimelea hao hupatikana kwa wingi katika utumbo mpana. 

Hivyo, kitendo cha kujisafisha kwa njia hiyo, anasema huwasafirisha bakteria hao kutoka sehemu ya haja kubwa kuja katika njia ya haja ndogo.

Anasema mazingira haya husababisha UTI kwa wanawake kwa sababu njia ya haja kubwa na ndogo zipo karibu sana. 

“Mama wajawazito pia wako hatarini zaidi kwa sababu mimba kukandamiza kibofu na kusababisha kukosekana kwa uwazi katika njia ya mkojo ambayo kitaalamu inajulikana kama incomplete emptying,” anafafanua Dk Kaniki. 

Mtaalamu wa magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Fransis Fredrick anasema takwimu zinaonyesha kuwa kwa kila wanawake watano, mmoja amewahi kupata ugonjwa huo. 

Hali hiyo anaielezea kuwa huweza kuwa ni ya kujirudia mara kwa mara kwa baadhi ya wanawake, hasa kinamama wajawazito na watu wenye umri mkubwa. 

Mbali na wanawake kupata maambukizi zaidi, Dk Fredrick anaeleza kuwa watoto wa jinsi zote pia wako hatarini. 

Anasema ni vema mazingira ya chooni na bafuni yawe safi ili kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi haya. 

Dk Fredrick anabainisha kuwa maambukizi katika njia ya mkojo yanaweza kusababishwa na bacteria, fangasi au virusi. Anasema matibabu yake hutolewa kulingana na aina ya vimelea waliosababisha maambukizi hayo. 

Kisukari huathiri zaidi 

Maambukizi haya yanaweza pia kuwaathiri watu wenye kisukari kirahisi zaidi kwa sababu ya sukari nyingi iliyopo katika mkojo. 

Sukari hiyo huchochea kuzaliana kwa bacteria wanaosababisha maambukizi. 

Kwa mujibu wa ripoti iliyofanywa na Chama cha Kisukari cha Marekani (ADA), asilimia 9.4 ya watu wanaokutwa na kisukari wanaugua pia UTI wakati asilimia 5.7 ni wenye maambukizi lakini hawana kisukari. 

Wenye kisukari wanaathirika zaidi kwa sababu pia bakteria kuzaliana kwa wingi na baadhi ya mishipa inaharibika na kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa sukari nyingi iliyopo kwenye damu ya mgonjwa wa kisukari inaua seli nyeupe za damu, hivyo mwili unakosa kinga ya kupambana na bakteria hatarishi walioingia mwilini. 

Athari, dalili, tiba 

Dk Kaniki anafafanua kuwa endapo mtu hatatibiwa mapema au kumaliza dozi, ugonjwa huu unaweza kuwa sugu na kusababisha kuharibika kwa figo na kibofu. 

Anasema maambukizi yanayotokea chini ya kibofu huathiri kibofu na mirija inayotoa mkojo nje. 

Maambukizi yanayotokea katika figo ni hatua ya juu na athari zake ni kubwa zaidi kuliko athari zitokeazo katika mirija na kibofu. 

Alibainisha athari nyingine kuwa mwanamke mjamzito anaweza kuzaa mtoto kabla ya wakati au mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu. 

Anasema wagonjwa wanashauriwa kupata tiba mapema na kumaliza dozi na kwamba watoto wadogo na wazee pia wanaweza kupata maambukizi hayo kirahisi. 

Ripoti ya ADA inabainisha dalili za awali kwa mtu mwenye maambukizi katika njia ya mkojo ni maumivu wakati wa kukojoa, kuhisi kukojoa laini ukienda chooni mkojo unatoka kidogo sana, kukojoa mkojo wenye damu na maumivu ya tumbo na mgongo. 

Dalili kwa maambukizi yaliyokomaa, zinaelezwa kuwa ni homa kali, kutetemeka, kutapika, kuharisha na maumivu ya mgongo. 

Hata hivyo, kinga ya ugonjwa huu inaelezwa kuwa ni kuzingatia kanuni za usafi hasa baada ya haja kubwa na kujisafisha kuanzia sehemu ya mbele kwenda nyuma ili kutoruhusu vimelea kuingia katika njia ya mkojo kwa urahisi. 

Inashauriwa kumwona daktari baada ya kuona dalili hizi na kutumia kikamilifu dawa itakayopendekezwa na daktari. 

Ni muhimu kwa mgonjwa kumaliza dawa ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa huo mara kwa mara na kusababisha madhara au usugu.


 MWANANCHI

Related

TUJUZANE 2801544113123165898

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item