CHADEMA YAKUSANYA SAINI ZA WANANCHI KUKATAA MAISHA MAGUMU

  Wabunge watano wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliofukuzwa bungeni wiki iliyopita na kupewa adhabu ya siku tano ya kuto...

 
Wabunge watano wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliofukuzwa bungeni wiki iliyopita na kupewa adhabu ya siku tano ya kutohudhuria vikao vya Bunge la bajeti, wameanza kukusanya orodha ya wananchi katika mikoa minne, wakiomba ridhaa yao kuunga mkono hoja binafsi itakayowasilishwa bungeni baada ya Aprili 30, mwaka huu.
 
Hoja hiyo inalitaka Bunge liilazimishe serikali kupunguza athari za ongezeko la kupaa kwa gharama za maisha na kudhibiti mfumuko wa bei.
 
Mbunge wa jimbo la Ubungo, John Mnyika, ambaye ameungana na wabunge hao katika ziara hiyo maalumu ya kukishitaki kiti cha Spika wa Bunge, Anna Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, alisema Chadema inakusanya sahihi za wananchi katika mikoa ya Iringa, Njombe, Dodoma na Mbeya ili kupata ridhaa ya umma itakayotimiza matakwa ya kikanuni kwa mujibu wa sheria za Bunge.
 
Mnyika alikuwa alitangaza dhamira hiyo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mwembetogwa,  Manispaa ya Iringa muda mfupi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Willibrod Slaa, kuzungumzia madai ya Chadema kuhusishwa na vitendo vya ugaidi. “Wananchi wangu naomba mjiandikishe kwenye hizo karatasi zinazopita huko kwenu na kuweka sahihi zenu kwa sababu tunataka ridhaa ya umma inayopendekeza Bunge liisimamie (liilazimishe) serikali ipunguze athari za ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi na kudhibiti mfumuko wa bei nchini…Hakuna anayependa kuona anakosa makazi, sukari inapanda bei, chakula bei juu halafu serikali hii hii inakaa kimya,” alisema Mnyika.
 
Kwa mujibu wa Mbunge huyo hoja yake ambayo amedai kuwa ataiwasilisha bungeni baada ya Aprili 30 mwaka huu, inatokana na kanuni ya 34 ya kanuni za kudumu za Bunge.
 
Hadi mkutano huo unaahirishwa jana jioni, zaidi ya watu 300 walikuwa wamejiorodhesha kukubaliana na hoja hiyo.
 
Dk. Slaa alisema licha ya Chama chake kuhusishwa na propaganda chafu za masuala ya ugaidi, yeye mwenyewe yupo tayari kutekwa, kuteswa, kuuawa na hata kungolewa macho na meno, lakini hatoacha kuzungumzia mambo yanayohusu maslahi mustakabali wa taifa.
 
“Nilitaja mafisadi 11 pale Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, lakini hadi leo sijakamatwa wala kesi kufunguliwa, kwa maana hiyo kama nilikuwa nimesema uongo leo hii ungekuta ninaoezea jela. Lazima wajue (CCM na serikali yake) kwamba Chadema hatuogopi kwa sababu tulianza na Mungu na tutamaliza na Mungu na kwa maana hiyo niko tayari kutekwa, kuteswa, kung’olewa macho, kucha na kuuawa, lakini si kuzibwa mdomo nisizungumzie mustakabali wa nchi,”  alisema.
 
Aliwaagiza  wabunge wote wa Chadema kuhakikisha kuwa kila hotuba ya Mawaziri vivuli wa chama hicho na michango yote ya wabunge wake itakayosomwa bungeni hivi sasa wanaidurufu na kuisambaza kwenye kila kata na ngazi zote za vijiji ili wananchi wajue nini viongozi wao wanachokifanya ndani ya bunge hilo.
 
Hata hivyo,hali ya usalama katika uwanja huo jana ilionekana kuimarika zaidi kutokana na makachero wa Polisi kutanda kila kona huku Dk. Slaa akiimarishiwa ulinzi kwa askari waliovaa sare kandokando ya jukwaa kuu.
 
Wakati huo huo, Dk. Slaa leo anaongoza timu ya wabunge tisa wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara unaofanyika jijini Mbeya wenye lengo la kuwaeleza wananchi sababu za baadhi ya wabunge wa Chadema kufukuzwa bungeni.
 
Katibu Mwenezi wa Chadema wilaya ya Mbeya Mjini, Christopher Mwamsiku, alisema ugeni huo mkubwa unaingia Mbeya kwa lengo moja kubwa la kukijenga chama na kutoa ufafanuzi wa kina wa sababu za kufukuzwa bungeni kwa wabunge wao, akiwamo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Mr. II Sugu.
 
“Wageni wetu tunawapokea kesho (leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Ruandanzovwe, mkutano ambao utaongozwa na Katibu wa Chadema Taifa, Dk. Slaa.
CHANZO: NIPASHE
 

Related

OTHER NEWS 3395538398017601836

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item