VIGOGO 200 WAHOJIWA MABILIONI YA USWISI

Suala la baadhi ya Watanzania kuhifadhi mabilioni ya fedha nchini Uswisi limechukua sura mpya, baada ya tume maalumu kuwahoji vigogo 200 w...


Suala la baadhi ya Watanzania kuhifadhi mabilioni ya fedha nchini Uswisi limechukua sura mpya, baada ya tume maalumu kuwahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa tume hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema tayari imeshafanya kazi hiyo kwa miezi miwili sasa.
Tume hiyo maalumu iliyoundwa na Serikali kwa Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana, inatarajiwa kukamilisha uchunguzi huo wakati wowote kuanzia sasa na kuwasilisha ripoti hiyo katika kikao kijacho cha Bunge. Jaji Werema alipoulizwa na Mwananchi Jumpili maendeleo ya uchunguzi huo, alisema kuwa kazi hiyo bado inaendelea.
“Uchunguzi huo unaendelea,” alisema Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.”
Mwanasheria huyo wa Serikali alikataa kutaja baadhi ya majina ya watu ambao tume yake imewahoji mpaka sasa.
Alisema anashangazwa na swali la namna hiyo, kwa maelezo kwamba ni jambo ambalo liko wazi kuwa ni kinyume na maadili kuwataja watuhumiwa wakati huu uchunguzi ukiwa bado unaendelea.
Uchunguzi huo unafanyika baada ya Benki ya Taifa ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa mwezi Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida la kimataifa la uchunguzi la The Indian Ocean Newsletter toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini.
Werema anaripotiwa akiri kuwa uchunguzi huo umefikia ‘hatua ya kutia matumaini’ na wanaendelea na kazi hiyo kwa uangalifu ili kuwa na uhakika wa taarifa wanazozitafuta.
Alisema kwamba taarifa ya awali inatarajiwa kutolewa hivi karibuni na tayari idadi kubwa ya wahusika wakiwamo wabunge wameshahojiwa.
Werema alisema wanaendelea na uchunguzi kuwabaini zaidi ya Watanzania 200, waliotajwa kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Mbali na Werema, tume hiyo inaundwa na viongozi kadhaa wa taasisi nyeti kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Tume hiyo inawahusisha pia Mkuu wa Sheria wa BoT, Mustapha Ismail na maofisa kutoka idara ya upelelezi na ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa jarida hilo la kimataifa, miongoni mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na majenerali wastaafu wanaotuhumiwa kutorosha zaidi ya Dola 133 milioni mwaka 2005, kupitia Mfuko wa Ulipaji Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika wamehojiwa kutokana na taaluma zao, familia zao, akaunti zao za benki zilizoko nchini na nje ya nchi pamoja na nchi walizotembelea mara kwa mara kwa miaka mitatu iliyopita.
Lengo la kuwahoji inaelezwa ni kutaka kujua iwapo walifuata njia zinazotakiwa katika kufungua akaunti hizo nje ya nchi na iwapo fedha zilizohifadhiwa huko zilipatikana kihalali.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa Bungeni kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Bunge liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja ambacho kinaishia Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo bungeni.

Related

OTHER NEWS 9214772169651694443

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item