MKUTANO WA TFF WAPITISHA MAREKEBISHO YA KATIBA, WAKATI HUO HUO TAIFA STARS IKITOKA PATUPU MBELE YA UGANDA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Julai 13, 2013 MKUTANO TFF WAPITISHA MAREKEBISHO YA KATIBA Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/07/mkutano-wa-tff-wapitisha-marekebisho-ya.html
Julai 13, 2013
MKUTANO TFF WAPITISHA MAREKEBISHO YA KATIBA
Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu (TFF) uliofanyika leo (Julai 13 mwaka huu) umepitisha
marekebisho ya Katiba yake, hivyo mchakato wa uchaguzi unatarajia kuanza
wakati wowote.
Wajumbe zaidi ya 100 walihudhuria
Mkutano huo uliofanyika ukumbi wa NSSF Waterfron, Dar es Salaam na
kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera aliyewataka
wajumbe kuhakikisha kiwango cha mpira wa miguu nchini kinakuwa.
Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti
wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga umefanya marekebisho ya Katiba kutokana
na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). James
Johnson kutoka Idara ya Wanachama ndiye aliyeiwakilisha FIFA katika
mkutano huo.
Aprili mwaka huu FIFA ilisimamisha
mchakato wa uchaguzi wa TFF, na kuagiza kwanza yafanyike marekebisho ya
Katiba ili kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili
ambavyo ndivyo watashughulikia matatizo ya kimaadili kwa familia ya
mpira wa miguu nchini.
Mbali ya kamati hizo, mabadiliko hayo
pia yametengeneza ngazi mbili za kushughulikia masuala ya kinidhamu
ambazo ni; Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Rufani ya Nidhamu.
Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais
Tenga itakutana kesho (Julai 14 mwaka huu) kwa ajili ya kuteua wajumbe
watakaounda Kamati hizo ili kuruhusu kuanza mchakato wa uchaguzi ambao
FIFA iliusimamisha hadi vitakapoundwa vyombo hivyo.
TAIFA STARS YAPOTEZA MECHI NYUMBANI
Taifa Stars imeshindwa kuutumia vizuri
uwanja wa nyumbani baada ya leo (Julai 13 mwaka huu) kufungwa bao 1-0 na
Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika
mwakani nchini Afrika Kusini.
Denis Iguma ndiye aliyefunga bao hilo
pekee kwa Uganda dakika moja baada ya mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka
Burundi kupuliza filimbi kuanzisha kipindi cha pili cha mechi hiyo
iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa
Stars, Kim Poulsen amesema mpira wa miguu ni mchezo wa kufunga mabao
ambapo timu ilipata nafasi nzuri katika dakika ya kwanza tu lakini
ilishindwa kuibadili kuwa bao.
“Uganda walitengeneza nafasi moja tu
katika kipindi cha kwanza wakati sisi tulikuwa nazo kadhaa. Kipindi cha
pili tuliwapa nafasi wakafunga bao lao. Lakini kwa kifupi kama wao
wameweza kufunga hapa (Dar es Salaam), hata sisi tunaweza kufunga
Kampala,” amesema Kim akizungumzia nafasi ya timu yake kusonga mbele.
Timu hizo zitarudiana jijini Kampala
kati ya Julai 26 na 27 mwaka huu ambapo mshindi ndiye atakayepata tiketi
ya kwenda kwenye fainali za tatu za CHAN zitakazofanyika Afrika Kusini.
Stars ilicheza fainali za kwanza za CHAN zilizofanyika mwaka 2009
nchini Ivory Coast.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)