HIZI NDIZO MBINU ZA KUISHI KAMA HAUNA PESA MFUKONI !!!!.

Na James Mwang'amba WAZUNGU wana msemo wao unaosema, ‘Life is unpredictable’ wakimaanisha kwamba maisha hayatabiriki. Wapo ambao w...

Na James Mwang'amba
WAZUNGU wana msemo wao unaosema, ‘Life is unpredictable’ wakimaanisha kwamba maisha hayatabiriki. Wapo ambao walikuwa na hali nzuri sana kifedha huko nyuma lakini leo hii ukiwaona huwezi kuamini. 
Wanaishi maisha magumu sana tena kwa msaada wa watu wengine. Hayo ndio maisha! Leo hii ukiwa juu usijipe asilimia mia moja kwamba siku zote utakuwa juu. Upo uwezekano mkubwa kabisa wa siku moja kuwa chini na waliokuwa chini wakapanda.
Kwa mantiki hiyo basi tunapolizungumzia suala la kuishiwa linamgusa kila mtu bila kujali tajiri wala maskini. Kimsingi kuishiwa ni hali ya kukosa pesa kwa ajili ya matumizi yetu ya kila siku.
Hali hii ni ya kawaida katika maisha ya binadamu. Hii inamaanisha kwamba unaweza ukawa unafanya kazi na kuwa na kipato kizuri tu, lakini katika mazingira fulani ukajikuta pesa ambayo ulikuwa nayo imekwisha.
Yawezekana ukawa umepata matatizo yanayohitaji fedha nyingi ukazitumia katika kutatulia matatizo hayo au unaweza kujikuta umeishiwa baada ya mshahara kuchelewa na ukajikuta kwamba huna kitu kabisa.

Wakati huohuo unahitaji chakula, matibabu, usafiri na mahitaji mengine ya msingi yanayohitaji pesa. Ufanyeje sasa ili uweze kuendelea kuishi ?.
Katika kukabiliana na tatizo kama hili hapo ndipo umuhimu wa suala la kuishi vizuri na watu linapoonekana.
Nasema hivyo kwa sababu, katika mazingira hayo hakuna njia nyingine zaidi ya kuomba msaada kutoka kwa watu walio karibu yako. Sasa kama uhusiano wako na watu wanaokuzunguka sio mzuri unatarajia nani atakusaidia ?.

Kwa ufupi hakuna na kama atajitokeza msamaria mwema wa kukusaidia basi atakuwa ni mtu ambaye hakufahamu tabia zako na uhusiano wako na watu kwa jumla. 

Wapo watu ambao hujisahau kabisa wanapokuwa na vijisenti na kuwa na maringo, dharau na tabia nyingine zinazochukiza bila kujua kwamba ipo siku pesa hizo zitakwisha. Lakini mtu huyo huyo atakapokuja kuishiwa utamuonea huruma kwani si ajabu hata akapatwa na homa. 

Unapojikuta umeishiwa kwanza chukulia kwamba ni hali ya kawaida na amini kwamba unaweza kuendelea kuishi licha ya kuwa katika hali hiyo.

KOPA

Naamini kabisa utakuwa na marafiki, ndugu na jamaa ambao kwa namna moja wanaweza kukuelewa utakapowaeleza kwamba umeishiwa hivyo unaomba wakukopeshe pesa.
Katika hili wengi hujipoteza uaminifu, wanakuwa wagumu sana kulipa madeni yao. 
Ni vizuri unapokopa pesa kwa mtu ukakumbuka kulipa katika wakati muafaka. Hicho ndicho kitakufanya siku nyingine kuweza kupata msaada huo.
Wapo baadhi ya watu ni wazuri sana kukopa tena wanakuwa wapole sana wakati wanafanya hivyo lakini wanakuwa wagumu na wakali wanapotakiwa kulipa deni. 
Hivi unapofanya hivyo unatarajia siku nyingine utakapoishiwa ukakope wapi?
Kwa kifupi unapoona kwamba umeshiwa unayo nafasi ya kukopa pesa kutoka wale ambao unaamini wanaweza kukusaidia. Lakini cha msingi katika hili ni kujijengea uaminifu. 

Bila kuwa muaminifu hakuna atakayekuwa tayari kukukopesha na hapo ndipo unaweza kuiona dunia ni chungu.

OMBA MSAADA
Unapoishiwa unaweza kuendelea kuishi kwa kuomba msaada kwa watu walio karibu yako. Yaani badala ya kuomba ukopeshwe unaweza kuomba usaidiwe. Kusaidiana ni jambo la msingi sana kwani leo kwangu kesho kwako. Kwa hiyo kwa kumsaidia mwenzako leo unajiwekea mazingira mazuri ya kuja kusaidiwa pale utakapohitaji msaada.

Katika maisha ya sasa ni rahisi sana kuomba ukopeshwe ukakopeshwa kuliko kuomba kusaidiwa. Kwa mfano unaweza kumfuata mtu leo hii ukamwambia akukopeshe laki moja. 

Mtu huyo anaweza kukupa akijua kwamba ni kama vile unamhifadhia kwani siku moja utamrudishia. Lakini mtu huyo huyo akimfuata na kumwambia akusaidie kiasi hicho hicho cha fedha ni vigumu sana kukupatia labda uwe na uhusiano naye wa karibu sana.

Related

TUJUZANE 8869575221576318335

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item