SAKALA LA KUTEKWA KWA DK ULIMBOKA, AFUTIWA KESI YA KUMTEKA LAKINI ASHTAKIWA KWA KUDANGANYA KUMTEKA.

DAR ES SALAAM.   MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia mashtaka raia wa Kenya, Joshua Mulundi kuhusu kumteka na kumjeruhi Mw...



DAR ES SALAAM. 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia mashtaka raia wa Kenya, Joshua Mulundi kuhusu kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka na sasa atakabiliwa na mashtaka ya kuidanganya polisi kuhusika kumteka daktari huyo.
Hakimu Warialwande Lema aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alifikia hatua hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), kuwasilisha hati ya kumfutia mashtaka hayo.
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Beatha Kitau kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika.

Akiwasilisha hati hiyo mahakamani, Wakili Kitau alisema DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa, chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka. Kutokana na uamuzi huo wa DPP, Hakimu Lema alimfutia mashtaka Mulundi na kumwachia huru.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, alikamatwa na kufunguliwa kesi nyingine ya kutoa taarifa za uongo kwa Jeshi la Polisi.
Katika kesi hiyo mpya inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka, alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai, 2012, katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Wakili Kweka alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa akiwa kituoni hapo alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa polisi kuwa yeye na wenzake ndiyo waliokodiwa ili kumteka na kumdhuru Dk Ulimboka wakati akijua kuwa si kweli.

Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo.
Wakili Kweka alisema upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili waweze kuandaa maelezo ya awali ya kesi hiyo. Pia aliweka pingamizi la dhamana dhidi ya mshtakiwa akidai hana makazi ya kudumu kwa kuwa si raia pia kwa ajili ya usalama wake kulingana na mazingira ya tukio hilo.
Kauli hiyo ya Wakili Kweka ilimfanya mshtakiwa huyo alipuke na kudai kuwa wanamfungulia kesi za uongo ambazo hahusiki na kudai kwamba wamepanga kumpoteza.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba unisamehe, kwa kile nitakachokifanya, kwani nikirudi mahabusu mimi itaniumiza,” alidai mshtakiwa huyo na kusisitiza kuwa hahusiki na kwamba bado ni kijana mdogo.
Baada ya mshtakiwa huyo kulalamika hivyo, Hakimu Katemana aliutaka upande wa mashtaka uwasilishe hati ya kuzuia dhamana ambayo hata hivyo, hawakuwa nayo licha ya kuwaongezea saa mbili kuandaa. 
MWANANCHI

Related

OTHER NEWS 8378719457294179276

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item