HIZI NDIZO MBINU MPYA ZA MAWASILIANO KUHUSU MAENEO YA KUUZA NA KUNUNUA MADAWA YA KULEVYA.
LICHA ya vita dhidi ya dawa za kulevya nchini kupigiwa chapuo na wanasiasa, akiwamo Rais Jakaya Kikwete sambamba na kuwapo kwa Tume ya ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/hizi-ndizo-mbinu-mpya-za-mawasiliano.html
LICHA ya vita
dhidi ya dawa za kulevya nchini kupigiwa chapuo na wanasiasa, akiwamo Rais
Jakaya Kikwete sambamba na kuwapo kwa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya,
wauzaji na wateja wa biashara hiyo wamebuni mbinu mpya ya mawasiliano kuhusu
maeneo ya kuuza na kununua dawa hizo, uchunguzi umebaini.
Uchunguzi huo
wa muda mrefu i Jijini Dar es Salaam, na hususan maeneo ya Kinondoni na
Magomeni umebaini kuwapo kwa ishara maalumu za kuwatambulisha wanunuzi wa dawa za kulevya kwamba sehemu fulani ndipo dawa hizo huuzwa.
Kwa mujibu wa
uchunguzi huo, kila unapoona jozi ya viatu imetundikwa katika nyaya za umeme
barabarani basi, mita chache tu kuna biashara ya kuuza na kununua dawa za
kulevya kwa kuzingatia mahitaji yako.
Mwandishi wetu
amefika katika baadhi ya maeneo hayo na kununua baadhi ya dawa hizo ikiwa ni
sehemu ya kuhakiki uchunguzi wetu kwa mujibu wa matakwa ya kitaaluma na
kujiridhisha kwa namna gani vyombo husika, licha ya kuwapo kwa sheria za
kupinga biashara hiyo, vimekuwa vikizidiwa maarifa.
Kuning’iniza
jozi za viatu
Uchunguzi
wa Raia Mwema, umebaini kuwa mtandao wa wauzaji dawa za kulevya ambao
ndio wauzaji wadogo wadogo wamekuwa wakitambuana kwa jina maalumu la “mapusha”
na kwamba vijana hao ni miongoni mwa wakazi wa maeneo husika na wengine
wakiheshimika katika mitaa wanayoishi.
Lakini licha
ya kuwa na jina maalumu la kimtandao, wahusika hao wamekuwa wakitumia mbinu
hiyo ya kutundika jozi ya viatu katika nyaya za umeme kama zinavyoonekana
katika picha iliyopigwa na timu ya waandishi wetu iliyohusika na uchunguzi
wetu.
Ni aina
maalumu ya viatu
Si kila aina
ya viatu inaweza kutundikwa kama utambulisho wa kuwapo kwa “maduka” ya dawa za
kulevya katika maeneo husika.
Aina hiyo
maalumu ya viatu inaitwa “All Star”. Ni viatu vilivyoko katika muundo maalumu
mithili ya “buti”. Katika baadhi ya maeneo, timu ya waandishi wetu ikielekezwa
na ishara hizo za viatu imefika na kununua dawa hizo.
Uchunguzi wetu
umebaini kuwa katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam mbinu hiyo ya
kuning’iniza jozi ya viatu imekuwa ikitumiwa mno katika maeneo ya Tandale,
Kinondoni-Mkwajuni, Msasani, Kinondoni B katika mitaa ya Wibu, Togo na Ufipa
jirani na Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ana kwa ana na
watumiaji ‘unga’
Katika vijiwe
hivyo, mwandishi wetu akiigiza kama mmoja wa watumiaji sugu wa dawa hizo haramu
za kulevya, alipenya na kuzungumza na baadhi ya watumiaji halisi wa dawa hizo.
Mmoja wa
watumiaji hao aliyekutana na mwandishi wetu katika ‘kijiwe’ cha Mtaa wa Wibu,
Kinondoni ambaye baada ya mazungumzo ‘kukolea’ kati yake na mwandishi wetu,
ilibidi mwandishi ajitambulishe rasmi, alikiri kuwa katika kila eneo zinapouzwa
dawa hizo viatu vimekuwa vikining’inizwa juu ya nyaya za umeme.
Mtumiaji huyo
wa dawa za kulevya ambaye katika habari hii hatutataja jina lake, alimweleza
mwandishi wetu; “Sina uhakika sana na mbinu hiyo ya kutundika ‘All Star’ (jozi
za viatu) juu ya nyaya za umeme kuwa ni alama ya kuuzwa mdude (dawa za
kulevya), lakini naweza kukubaliana na maneno yako kwani maeneo yote kunakouzwa
‘mdude huwaga’ nakuta alama hiyo.
“Zamani
tulikuwa tunaiga Wamarekani kutundika ‘All Star’ katika nyaya za umeme, kwa
sasa hata sijui kuna uhusiano gani na biashara hii. Ila naweza kukuthibitishia
kuwa ni kweli kila kunapouzwa ‘mdude’ huwa kuna viatu aina ile vinaning’inia
kwenye nyaya.”
Mwandishi wetu
pia alizungumza na kijana mwingine ambaye naye ni muuzaji mdogo wa dawa hizo na
hapa, kwa sababu maalumu tutamwita jina lisilo halisi la Kijiko Issa.
Mwandishi wetu
alikutana na kijana huyo anayeishi mtaa wa Togo, Kinondoni B jijini Dar es
Salaam.
Kijiko
alitambulishwa kwa mwandishi wetu na Baraka kuwa yeye ndiye pusha (muuzaji) wa
dawa za kulevya. Pusha (muuzaji) huyo katika mazungumzo yake na mwandishi wetu,
hakuwa tayari kuthibitisha kuwa utundikaji jozi za viatu katika nyaya za umeme
ni ishara ya kuuza ‘unga’ eneo hilo.
Lakini baada
ya mazungumzo marefu na mwandishi wetu, Kijiko alisema; “Mimi naona tu maeneo
mengi ninapokwenda kununua ‘busta’ (kifuko cha dawa za kulevya chenye uwezo wa
kuzalisha kete 200 mpaka 250), huwa nakuta ‘All Star’ zimetundikwa juu ya umeme
lakini kiukweli sijui maana yake nini.
“Kwa mfano
mtaa wa Ufipa karibu na ofisi za CHADEMA kuna dogo ‘anabana mzigo’ (anauza
dawa) pale au ukienda Bonde la Mkwajuni pembeni ya barabara utakuta viatu vingi
vipo juu ya umeme pale pia kuna jamaa wanabana mzigo.”
Maelezo ya
mamlaka ya udhibiti
Timu yetu
haikuishia hapo bali ilikwenda katika ofisi za Kikosi cha Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini na kukutana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, ambaye ni
mkuu wa kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya nchini, Godfrey Nzowa.
Kamanda Nzowa
alimweleza mwandishi wetu kuwa, anazo taarifa za kila mbinu mpya inayotumiwa na
wauzaji wakubwa na wadogo wa dawa za kulevya nchini.
Kwa mujibu wa
Kamanda Nzowa, wanayo timu maalumu ya askari katika kila eneo linalosifika kwa
biashara hiyo.
“Hiyo mbinu
nimeisikia kutoka kwa vijana (askari) wangu, lakini nasi pia hatuna uhakika
nayo kwani bado ni mpya ila tunashukuru kwa utafiti wenu nasi tutaufanyia kazi
utafiti huo,” alisema Nzowa.
Sheria
inalenga vigogo wa ‘unga’
Hata hivyo,
katika maelezo yake, Kamanda Nzowa alisema ingawa kikosi chake kinashiriki
kikamilifu kudhibiti kila kundi la wauzaji wa dawa hizo, sheria inalenga zaidi
kudhibiti waingizaji wa dawa hizo nchini kuliko wasambazaji.
“Sisi
tunafuata sheria ya kudhibiti dawa za kulevya sura ya 95 (The drugs and
prevention of illicit traffic in drugs) ambayo inaegemea sana katika
waingizaji kuliko watumiaji na wasambazaji, ingawa upande huo nao hatuufumbii
macho,” alisema Kamanda Nzowa.
Kilo moja
huathiri watu milioni moja
Lakini Kamanda
Nzowa alizungumzia pia kiwango cha madhara, yaani kwa namna gani kiwango kidogo
tu cha dawa za kulevya kinavyokuwa na uwezo wa kuathiri idadi kubwa ya
watumiaji.
Akifafanua
Kamanda Nzowa, alisema mtumiaji huweza kutumia kiwango cha kati ya gramu 0.01
na 0.11 ambayo ni kete moja na kwamba, kilo moja ya dawa za kulevya huweza
kuathiri takriban watu (watumiaji) milioni moja.
Alisema ingawa
lengo la kikosi chake ni kuangamiza matumizi ya dawa za kulevya nchini lakini
changamoto katika kufikia mafanikio ni nyingi na zimekuwa zikiongezeka kila
siku.
Alizitaja
baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kukosa bajeti ya kutosha kutoka
serikalini. Lakini wakati bajeti ikiwa ndogo, vigogo wauza dawa za kulevya
wamekuwa na uwezo mkubwa kifedha. via JF