SHEIKH PONDA AWEKWA CHINI YA ULINZI MUHIMBILI
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa amelazwa kwenye chumba maalumu katika taasisi ya mifupa...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/sheikh-ponda-awekwa-chini-ya-ulinzi.html
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda
Issa Ponda yupo chini ya ulinzi huku akitibiwa majeraha katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili.
Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka
Morogoro baada ya juzi kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa
bomu saa 12:25 jioni alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda
katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa
mhadhara katika kongamano mjini hapo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Ponda zilisema
kwamba baada ya kupata taarifa za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh
walifunga safari kwenda Morogoro na kumrejesha Dar es Salaam usiku
huohuo. Kabla ya kurudishwa Dar es Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda
alipelekwa katika Zahanati ya Islamic Foundation.
Mmoja wa wanafamilia alidokeza kwamba Sheikh Ponda
alifichwa na alikuwa chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wake na hakuna
aliyeruhusiwa kumsogelea.
Muhimbili
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye jana
zilisema kuwa alifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya
kupatiwa matibabu.
Sheikh Ponda alifikishwa Muhimbili jana saa 7:18
mchana na alipelekwa kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura na baadaye
alitolewa na kupelekwa kwenye chumba cha x-ray kwa ajili ya vipimo.
Baadaye alipelekwa chumba cha upasuaji.
Eneo kubwa la hospitali hiyo lilikuwa na idadi
kubwa ya askari na mmoja wa askari waliokuwa doria hospitalini hapo
alisema walitawanywa kwenye hospitali mbalimbali za Dar es Salaam baada
ya kupata taarifa kuwa angeletwa kwa matibabu.
“Nakuambia tuko hapa tangu saa kumi na moja
asubuhi, tumetawanywa hospitali mbalimbali baada ya kupata taarifa kuwa
analetwa Dar. Bahati nzuri kaletwa hapa Muhimbili... tunasubiri apate
matibabu na tutamtia mbaroni,” alisema askari huyo.
Taarifa ya polisi
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana
katika taarifa yake kuwa Sheikh Ponda yuko Hospitali ya Muhimbili
akitibiwa baada ya kupata majeraha yaliyotokana na purukushani na polisi
wakati wafuasi wake walipokuwa wanataka kumtorosha.
“Kutokana na tukio hilo, timu inayoshirikisha wajumbe kutoka
Jukwaa la Haki Jinai likiongozwa na Kamishna wa Polisi Isaya Mungulu
imeanza uchunguzi wa tukio hilo na Polisi inawataka wananchi kuwa
watulivu wakati wanashughulikia suala hilo kisheria.”
Polisi Morogoro wapigwa chenga
Wakati akiwa Muhimbili, Polisi mkoani Morogoro, lilisema bado linamtafuta Sheikh Ponda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine
Shilogile alisema jana kuwa kwa taarifa zilizopo, bado Sheikh Ponda
amefichwa mkoani Morogoro na kwamba anaendelea kutafutwa.
“Tamko la Serikali mpaka sasa hatujathibitisha
kwamba Sheikh Ponda amejeruhiwa na risasi na tunamtaka mtu yeyote awe
yeye au ndugu yake aje kuthibitisha kwamba amepigwa risasi,” alisema.
Alikanusha madai kwamba jeshi hilo limehusika
kumpiga risasi akisema hakuna ushahidi kwa kuwa hajaonekana ili
kuonyesha kuwa amepata majeraha sehemu yoyote ya mwili wake.
“Siku zote risasi haifichiki, kama amepigwa angejitokeza ili kupewa kibali cha matibabu,” alisema Shilogile.
Alisema polisi inawashikilia watu wawili na
inawatafuta viongozi watano wa Umoja wa Waadhiri wa Kiislamu Mkoa wa
Morogoro walioandaa kongamano hilo.
Kamanda Shilogile alisema waandaaji wa kongamano
hilo walipewa kibali na polisi kufanya kongamano kwa masharti ya
kutokutoa matamshi ya uchochezi ikiwa ni pamoja na Sheikh Ponda
kutokuhudhuria.
Alisema hata hivyo, katika kongamano hilo
lililofanyika eneo la Kiwanja cha Ndege kulikuwapo na wageni zaidi ya
watano waliohutubia. Kamanda Shilogile alisema ilipofika saa 12.50 jioni
ndipo Sheikh Ponda alipofika na baadaye kupewa dakika tano kuzungumza
na alieleza kuwa yeye si mzungumzaji kwa siku hiyo na badala yake
angezungumza leo katika Viwanja vya Msikiti wa Jabal Hirra.
Alisema baada ya hapo mkutano ulifungwa na wafuasi
wake wakaanza kusukuma gari alilokuwa amepanda katika Barabara ya
Tumbaku karibu na Kituo cha Mafuta cha El Saedy. Alisema kuwa, polisi
walimfuata kutaka kumtia mbaroni lakini wafuasi wake walianza kurusha
mawe na ndipo askari hao walipofyatua juu risasi tatu za baridi ili
kuwatawanya.
Hata hivyo, alisema polisi walizidiwa nguvu na
wafuasi hao ambao walifanikiwa kumtorosha Sheikh huyo kwa
pikipiki.Alisema kuwa baadaye zilizagaa taarifa kuwa amepigwa risasi ya
begani na kupelekwa Hospitali ya Mkoa kisha kutoroshwa kusikojulikana.
Wavamia hospitali
Katika hatua nyingine, watu wanaosadikiwa ni
wafuasi wa Sheikh Ponda wamevamia Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na
kufanya uharibifu kwa kuvunja vioo katika wodi namba sita ya watoto
wakishinikiza kuonyeshwa Sheikh huyo alipo.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa na watoto wao katika
wodi hiyo, Kibua Michael na Cecilia Clemence kwa nyakati tofauti
walisema kwamba wafuasi hao walikusanyana nje ya hospitali hiyo na
kurusha mawe na kusababisha taharuki kwa baadhi ya wagonjwa.
Sheikh Kundecha atoa sharti
Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, imeitaka
Serikali kuunda tume huru ya uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh
Ponda na majibu yake ndiyo yatakayoamua uhusiano baina ya Waislamu
nchini na Serikali iliyopo madarakani.
Akitoa tamko la Jumuiya hiyo katika Msikiti wa
Mtambani, Kinondoni, Dar es Salaam jana, Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh
Yusufu Mussa Kundecha alisema pamoja na mambo mengine, pia wanataka
kuona askari polisi aliyemdhuru Sheikh Ponda anachukuliwa hatua za
kisheria.
Alisema kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda ni
mtiririko wa vitendo vya uonevu na unyanyasaji na aliishangaa Serikali
kumtafuta Sheikh huyo kupitia vyombo vya habari wakati inafahamu hatua
za kuchukua pale wanapokuwa wanamtafuta mtu.
Alisema hata yeye wakati anatafutwa na polisi
alipelekewa barua akitakiwa kuripoti kituoni lakini si kupitia vyombo
vya habari na kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa Serikali imeshindwa
kuwahakikishia raia usalama wao.
“Mbaya zaidi, wao ambao wanataka watu wasichukue
sheria mkononi ndiyo hao wa kwanza kufanya hivyo jambo ambalo sidhani
kama litatufikisha pazuri,” alisema Kundecha.
Aliitaka Serikali kufuata sheria na kufuata
taratibu husika katika kushughulikia masuala yanayowahusu makundi
mbalimbali katika jamii badala ya inavyofanya sasa akisema hiyo
inachangia chuki kati ya Waislamu na Serikali.
Profesa Lipumba atoa tamko
Mwenyekiti wa (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba
amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati suala la kupigwa risasi kwa
Sheikh Ponda ili nchi isije kuingia kwenye machafuko yenye mrengo wa
kidini.
Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini
kwake Dar es Salaam kuwa chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na
kutaka polisi kuwakamata waliompiga risasi.
“Nimetoka kumjulia hali muda mfupi uliopita,
nimemkuta akiwa katika hali mbaya japo anaweza kuzungumza na kutambua
watu wanaokwenda kumwona... kwa kweli tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh
Ponda linaweza kusababisha nchi kuingia kwenye machafuko ya kidini kama
hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tukio la Sheikh Ponda kupigwa risasi tena na watu wanaodhaniwa kuwa ni polisi, limeleta sura mbaya kwa taifa,” alisema Lipumba.
Rufaa ya wafuasi wake leo
Wakati hayo yakitokea, rufaa ya wafuasi 52 wa
Sheikh Ponda waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela inatarajiwa
kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo hicho, Machi 21,
mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa
makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama,
kutenda makosa, kukaidi amri ya polisi kabla na baada ya kufanya
maandamano yaliyozuiwa na polisi, kufanya mikusanyiko haramu na
kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa Wakili wao, Mohamed Tibanyendera walikata rufaa wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa.
Rufaa hiyo itasikilizwa leo na Jaji Salvatory Bongole.
Kwa mujibu wa hati ya rufani waliyoiwasilisha
mahakamani hapo, wafuasi hao, pamoja na mambo mengine, wanadai kuwa
hakimu alikosea kisheria katika kuchambua ushahidi wa pande zote
uliowasilishwa mahakamani.
Pia wanadai kuwa katika hukumu hiyo, hakimu
alijikanganya kwa kumwachia huru mmoja wa washtakiwa na kuwatia hatiani
washtakiwa wengine.
Watu hao walikamatwa na Polisi Machi 15, mwaka
huu, wakiandamana kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa
lengo la kumshinikiza kumpa dhamana Sheikh Ponda na mshtakiwa mwenzake
Mukadam Swalehe na Machi 18, mwaka huu walipandishwa kizimbani na
kusomewa mashtaka.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi