Taarifa ya Serekali Kuhusiana na Tukio la Kumwagiwa Tindi Kali Raia wa Uingereza huko Zanzibar
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUMWAGIWA TINDIKALI WATALII RAIA WA UINGEREZA 08/08/2013 Ndugu Wananchi, Jana m...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/taarifa-ya-serekali-kuhusiana-na-tukio.html
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUMWAGIWA TINDIKALI WATALII RAIA WA UINGEREZA
08/08/2013
Ndugu Wananchi,
Jana majira ya saa moja usiku, nchi yetu imekutwa na tukio la
kusikitisha sana la kushambuliwa kwa kumwagiwa tindi kali watalii vijana
wawili raia wa Uingereza Kate Gee na Kirstie Trup wwote wakiwa na umri
wa miaka 18. Shambulizi hilo lilifanyika katika eneo la Shangani. Tukio
hilo ni kubwa na linashitua sana kwani limeanza kuchukua sura mpya
kutokana na tindi kali kuanza kumwagiwa wageni.
Kumwagiwa vijana hao tindikali hakuwezi kuachiwa hata kidogo kwani
kitendo hicho kinajaribu kuiondoshea nchi sifa iliyojijengea ya Zanzibar
kuwa ni eneo la Amani na Utulivu. Mbali hayo, tendo hilo halikubaliki
katika mazingira ya kibinadamu kwani kila binadamu ana uhuru wa kuishi
na kutembea akiwa ana uhakika na usalama wake. – Sisi wenyewe
Wazanzibari, tunatembea na kuishi nchi mbali mbali za kigeni.
Kuachwa kuendelea kwa vitendo vya aina hii kunaweza kuwajengea hofu
wageni na raia wetu. Aidha, kitendo hicho kinaweza kuathiri sana sekta
ya utalii ambayo ni sekta kiongozi katika muhimili wa uchumi wetu.
Katika kuhakikisha jambo hilo halipewi nafasi kuendelea tena, serikali
imekusudia kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuendesha uchunguzi mkali wa
kuwasaka wahusika ili kuweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.Vyombo
vya ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi kwa pamoja kuwatafuta
wahal;ifu hao na mara watakapokamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya
sheria. Katika kufanya kazi hiyo Serikali inawaomba wananchi kutoa
ushirikiano utakaopelekea kuwakamata na kuwafikisha katika vyumba vya
sheria wote waliohusika na tukio hilo. Serikali ya Zanzibar kwa upande
wake inaahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni 10 kwa yeyote
atakayesaidia kukamatwa kwa watu waliofanya uhalifu huo.
Ndugu Wananchi,
Kwa vile bidhaa ya tindikali katika siku za hivi karibuni imeanza
kutumika vibaya, Seikali inachukua kila hatua kudhibiti matumizi ya
bidhaa hiyo kwa kudhibiti uingizaji, usambazaji, upatikanaji na utumiaji
wa tindikali na inazitaka taasisi zote zinazohusika zitimize wajibu
wake kwatika matumizi ya tindikali kwa kutumia sheria iliyopo na kwa
haraka kutunga kanuni za kuthibiti uuzaji na matumizi ya tindikali.
Katika kuhakikisha vitendo vya uhalifu haviendelei na hasa katika maeneo
ya utalii yakiwemo maeneo ya Mji Mkongwe na kwenye maeneo ya fukwe,
Serikali inachukua hatua za makusudi za kuweka ulinzi utakaosaidia
wageni wetu kuja nchini na kutembea bila ya bughudha.
Kupitia kauli hii, Serikali inaomba wananchi wote kutoa ushirikiano
mkubwa katika kulinda sekta ya utalii kama ndio chanzo kikubwa cha
uchumi wa nchi yetu.
Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunatoa pole kwa
waliojeruhiwa na familia zao na tunawaombea waliojeruhiwa wapate nafuu
haraka. Aidha, tunatoa pole kwa ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania na
kuuomba watupelekee masikitiko ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
Serikali ya Uingereza kwa tukio hilo na kwamba tutafanya kila jitihada
matukio kama haya yasitokee tena.
Ahsanteni