SHERIA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA, MNYIKA AWASILISHA MUSWADA BINAFSI
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amewasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa ya muswada binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la T...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/11/sheria-baraza-la-vijana-la-taifa-mnyika.html
Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amewasilisha kwa Katibu wa Bunge
taarifa ya muswada binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa.
Kwa
mujibu wa Mnyika, taarifa hiyo inaeleza madhumuni na sababu za muswada.
Mbali na taarifa hiyo, Mnyika pia amewasilisha nakala ya muswada husika
na hivyo kukidhi matakwa ya kanuni ya Bunge ya 81 (2).
Mnyika
alisema baada ya kuwasilisha vitu hivyo, hatua inayopaswa kufuatwa ni
Katibu wa Bunge kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni ya Bunge ya 81
(3), kutangaza muswada huo kwenye Gazeti la Serikali ili usomwe kwa
mara ya kwanza kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge unaoendelea.
Alisema
amechukua hatua hiyo baada ya ratiba ya mkutano wa sasa wa Bunge
kuonyesha kwamba Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa haupo
katika orodha ya miswada ambayo serikali inakusudia kuiwasilisha,
kinyume cha ahadi za mara kwa mara zilizotolewa za kuuwasilisha.
Kwa
mujibu wa Mnyika, alitarajia kwamba tarehe ya juzi ambayo ilikuwa ni
Siku ya Vijana wa Afrika, serikali ingetumia nafasi hiyo kutoa taarifa
ya utekelezaji wa mkataba wa vijana wa Afrika ambao uliridhiwa na Bunge
mwaka 2011.
Alisema
kifungu cha 11 cha mkataba huo ambao Rais Jakaya Kikwete alishiriki
katika mkutano wa kuuandaa mwaka 2006, kinataka nchi wanachama wa Umoja
wa Afrika (AU) kuhakikisha ushiriki wa vijana kwa pamoja na mambo
mengine kuwezesha kuundwa kwa mabaraza ya vijana.
Alisema
mkataba huo unaelekeza kwamba mabaraza yaundwe kuanzia kwenye ngazi ya
mitaa mpaka taifa kuwezesha vijana kushiriki katika maamuzi na
kutekeleza kikamilifu kazi mbalimbali za maendeleo.
“Katika
muktadha huo sehemu ya nne ya muswada huo, hususan vifungu vyake vya 27
na 28 vimewekwa utaratibu wa kuundwa kwa majukwaa (mabaraza) ya vijana
kwenye ngazi za vijiji/mitaa, kata na wilaya,” alisema Mnyika.
Pia
alisema sehemu ya sita ya muswada ina vifungu vinavyohusu Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana hususan kifungu cha 31 (1) kinachoeleza kwamba mfuko
huo utaundwa kwa ajili ya kuliwezesha baraza kutekeleza miradi ya
vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Vilevile, kuwezesha utekelezaji wa mipango ya baraza na kugharimia shughuli za baraza hilo.