ZANZIBAR INA MWELEKEO MZURI WA KUIMARISHA AFYA
Na Khamis Haji, OMKR Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema mafanikio yaliyoweza kupatikana ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/11/zanzibar-ina-mwelekeo-mzuri-wa.html
Na Khamis Haji, OMKR
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema
mafanikio yaliyoweza kupatikana katika sekta ya afya miaka ya hivi
karibuni ni ishara kuwa Zanzibar ina mwelekeo mzuri wa kuimarisha afya
za wananchi na kukuza maendeleo yao.
Maalim
Seif amesema hayo (27 Novemba) wakati alipokuwa akifungua mkutano wa
nane wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mikakati ya Sekta ya Afya Zanzibar,
unaofanyika hoteli ya Ocean View mtaa wa Kilimani mjini Zanzibar.
Amesema
ni dhahiri hatua ya Zanzibar kuelekea kutokomeza maradhi ya Malaria,
kupungua kwa asilimia kubwa vifo na matatizo yanayo wakumba akinamama
wakati wa kujifungua na mengineyo, zimeibua matumaini makubwa kuimarika
afya na maisha bora zaidi.
Aidha,
Maalim Seif amesema mafanikio hayo yanaleta matumaini kuwa Zanzibar
itamudu au kukaribia kabisa kutimiza malengo yaliyowekwa ya Milenia
katika sekta ya Afya, ifikapo mwaka 2015.
Makamu
wa Kwanza wa Rais alitoa mfano vifo vya akinamama wakati wa kujifungua
mwaka 2008 vilikuwa 422 kati ya watu 100,000, lakini kutokana na juhudi
kubwa zilizoweza kuchukuliwa vimeweza kupungua hadi kufikia 221 kati ya
watu 100,000, punguo ambalo ni wastani wa asilimia 50.
Aliwapongeza
watendaji na wataalamu wa Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na washirika
wa maendeleo kutokana na juhudi kubwa na moyo wa dhati wanao uonesha
katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuimarisha afya bora za
wananchi wa Unguja na Pemba.
Maalim
Seif, hata hivyo alisema kwa upande wa maradhi ambayo hadi sasa
yanaendelea kuwa changamoto kubwa, juhudi zaidi za kuwaelimisha wananchi
namna ya kujikinga nayo ziendelezwe.
Ameahidi
kwa upande wa Serikali itaendelea kuchukua juhudi kubwa zaidi katika
kujenga mazingira yatakayoweza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto
hizo. Alisema juhudi hizo zinajumuisha kuwapatia wananchi huduma bora,
ikiwemo maji safi na salama.
Amesema
bado changamoto zipo katika baadhi ya maeneo, kama vile kudhibiti
maradhi ya kichocho na Kifua Kikuu, ambayo pamoja na juhudi hizo kubwa
zinazoendelea kuchukuliwa kote Zanzibar, bado hali sio ya kuridhisha.
“Bado
hatua za upimaji wananchi Kifua Kikuu hazitoshi, bado kuna changamoto
ya wagonjwa kutomaliza dawa, maradhi ya kichocho pia ni tatizo,
changmaoto hizi zinapaswa kushughulikiwa ipasavyo, ili tuweze kuondokana
nazo”, alihimiza Maalim Seif.
Waziri
wa Afya, Mhe. Juma Duni Haji akizungumza katika mkutano huo alisema
juhudi za kuelimisha wananchi njia bora kulinda afya zao na jamii kwa
jumla zitaendelezwa, sambamba na kuhakikisha kunakuwepo wataalamu wa
kutosha katika Sekta ya Afya Zanzibar.
Alizitaja
miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa kutatua changamoto ya uhaba wa
wataalamu wa Kada hiyo, kuwa ni Serikali kusomesha wananchi katika vyuo
vya ndani na nje ya nchi, juhudi ambazo zimeanza kuzaa matunda kutokana
na kupatikanwa wahitimu ambao wanaendelea kutoa huduma Unguja na Pemba.
Amesema
mwelekeo wa Wizara ni kuwahamaisha wananchi kujikinga zaidi na maradhi
mbali mbali kuliko kusubiri kujitibu. “Tunahimiza Kukinga ni rahisi
kuliko kutibu”, alisema Waziri Duni.
Akiwasilisha
mada katika mkutano huo, Aisha A. Mohammed kutoka Wizara ya Afya
Zanzibar, amesema mkazo zaidi uwekwe na Serikali pamoja na washirika wa
Maendeleo katika kuhakikisha vifaa, wataalamu na mafunzo yanatolewa, ili
kuhakikisha utoaji wa huduma za afya unazidi kuimarika.
Mkutano
huo ambao hufanyika kila mwaka uliwashirikisha wadau mbali mbali,
wakiwemo wataalamu wa Afya, Washirika wa Maendeleo, Wawakilishi kutoka
Wizara ya Fedha, Jumuiya zisizokuwa za Kiserikali (NGOs) na baadhi ya
watendaji kutoka taasisi nyengine za Serikali.
Credits: ZanziNews