BUNGE LA KATIBA VIPANDE VIPANDE
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakijiandikisha bungeni mjini Dodoma, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa vikao vya bunge hilo. Pich...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/02/bunge-la-katiba-vipande-vipande.html
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakijiandikisha bungeni mjini Dodoma,
ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa vikao vya bunge hilo. Picha na Silvan
Kiwale
Dodoma.
Bunge Maalumu la Katiba, linaanza leo mjini hapa, huku kukiwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa wajumbe, unaotokana na misimamo tofauti.
Kipengele kinachowagawa wajumbe hao ni Muundo wa Serikali uliopendekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyokutana kwa siku
mbili Mjini Dodoma imeondoka na msimamo wa kutaka wajumbe wake wa bunge
hilo kutetea hoja ya Serikali mbili huku Chadema na CUF vinataka
Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila
hivi karibuni alikaririwa akitishia kwenda mahakamani kuzuia mchakato
mzima wa Katiba hadi iundwe Serikali ya Tanganyika.
Msimamo wa CCM
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja
vya CCM Mjini Dodoma jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho,
Nape Nnauye alisema msimamo wa chama chake haujabadilika na kwamba
wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki na mfumo
wa Serikali mbili.
“Hatuwezi kukataa mawazo ya watu wengine, lakini
kikubwa ambacho tunakisimamia ni kuhakikisha kuwa tunabaki na Serikali
mbili na ndiyo maana tumezungumza na wajumbe wa NEC na leo (jana),
tunakutana na wabunge wetu wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi
la Zanzibar,” alisema Nape.
Kuhusu kero zinazolalamikiwa na pande zote,
alisema CCM inafahamu kero nyingi na kwamba upande wa Bara kuna kero
nane na Zanzibar idadi kama hiyo.
“CCM imetengeneza mfumo mzuri wa kuziondoa kero
hizo ndani ya Serikali mbili siyo kama wenzetu ambao wamebuni Serikali
tatu eti iwe dawa ya kumaliza kero hizo kitu ambacho hakiwezekani,”
alisema huku akiwataka wajumbe na Watanzania kwa jumla, kulumbana kwa
hoja badala ya kupiga kelele.
Malecela aipinga CCM
Hata hivyo, kada mkongwe aliyewahi kuwa Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela alitofautiana na msimamo huo
akisema si sahihi kwa viongozi kuwatungia wananchi Katiba kama
inayoonekana kufanywa na baadhi yao.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Kenya,
Malecela alisema: “Kama tuliona inafaa kuwatungia wananchi Katiba,
hakuna ulazima wa kuwataka maoni yao. Mimi ni kiongozi na Katiba hii ni
ya wananchi, nisingependa kutoa maelekezo ya nini kifanyike, kama
viongozi wengine wanavyofanya.
“Ushauri wangu ni kwamba viongozi tusiwawekee wananchi misimamo. Tuwaache wafanye uamuzi kwa kuwa katiba hiyo ni yao.”
MWANANCHI
“Ushauri wangu ni kwamba viongozi tusiwawekee wananchi misimamo. Tuwaache wafanye uamuzi kwa kuwa katiba hiyo ni yao.”
Mnyika ataka mawazo ya umma
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema
anakusudia kuwasilisha mapendekezo kwamba ratiba ya Bunge ifanyiwe
mabadiliko ili kuwe na kikao cha kusikiliza mawazo ya umma.
Alisema kwa kusikiliza mawazo hayo juu ya kanuni
hizo, kutawezesha maoni ya Watanzania wengi kusikilizwa wakati wa
maandalizi ya kanuni kabla ya Bunge kupitisha azimio la kuridhia kanuni
hizo.
Pia alisema atawasilisha hoja kwa Katibu wa Bunge
na Katibu wa Baraza la Wawakilishi ambao ndiyo waitishaji wa mkutano huo
ili kanuni hizo zisitolewe kwa wajumbe wa Bunge hilo tu, bali ziwekwe
pia kwenye tovuti za Bunge, Baraza la Wawakilishi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dodoma, (Udomasa), Paul Losulite alisema anaamini kuwa mwafaka
utapatikana katika majadiliano ya bunge hilo. “Wajadiliane lakini ifike
sehemu wafahamu kuwa maoni ya wananchi lazima yaheshimiwe,” alisema.
Aliwataka wajumbe kukubaliana katika mambo
yanayohusu masilahi ya taifa akisema si dhambi kutofautiana lakini ni
vizuri kufikia mwafaka.
MWANANCHI