MFUASI WA ZITTO AANZISHA CHAMA

  Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwigamba alisema mchakato wa kuandikisha wanachama mikoani kwa ajili ya kuomba usajili wa k...

 Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwigamba alisema mchakato wa kuandikisha wanachama mikoani kwa ajili ya kuomba usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria umeshakamilika.PICHA|MAKTABA 

Dar es Salaam. 
Chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) kimeanzishwa na kupewa usajili wa muda huku kikitamba kuwa mbadala wa vyama vyote vilivyopo sasa kwa maelezo kuwa vimekosa demokrasia ya kweli.
Miongoni mwa viongozi wa muda wa chama hicho ni Samson Mwigamba aliyetimuliwa uanachama wa Chadema kutokana na kuhusishwa na waraka uliotaka kumwandaa Zitto Kabwe kuwania uenyekiti wa chama hicho.
Mwigamba aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, alitimuliwa pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, huku uanachama wa Zitto aliyevuliwa nyadhifa zake zote zikiwamo za Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ukisubiri kesi aliyofungua mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwigamba alisema mchakato wa kuandikisha wanachama mikoani kwa ajili ya kuomba usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria umeshakamilika.
Alisema kimepata wanachama katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Hata hivyo, alisema kimechagua mikoa 10 ambayo Msajili wa Vyama vya Siasa atakwenda kuhakiki kama sheria inavyoeleza kabla ya kupewa usajili wa kudumu.
“Kama tutafanikiwa kupata usajili wa kudumu mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu zote katika chaguzi zote ndogo zitakazojitokeza, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani,” alisema Mwigamba.
Alisema bendera ya chama hicho itakuwa na rangi ya zambarau inayoashiria haki, heshima na uadilifu na rangi nyeupe inayonyesha uwazi na usafi.
“Katikati ya bendera inayozungukwa na rangi zambarau kuna nyota mfano wa chama kinachojitokeza katikati ya vyama vingi inayokuja kutatua matatizo ya wanyonge yaliyowakabili kwa kipindi kirefu,” alisema Mwigamba na kuongeza:
“Pembeni mwa bendera hiyo kuna misitari ya rangi ya dhahabu inayoonyesha rasilimali zetu, rangi nyeusi zinazoashiria sisi ni Waafirika.”
Alisema hivi sasa hakuna kiingilio katika kujiunga na chama hicho na kwamba mara baada ya kupatikana kwa katiba, ndipo suala hilo litakaposhughulikiwa sambamba na kiingilio.
Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu alisema ACT - Tanzania kinaamini katika demokrasia jamii na kina shabaha kuu ya kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi ambayo ni lazima jamii inufaike nayo.

Alisema ACT-Tanzania kinaongozwa na msingi mitano ambayo ni: uzalendo, usawa, uadilifu, demokrasia ya kweli, uwazi na uwajibikaji vitu ambavyo vyama vyote vya siasa nchini vimeshindwa kuvisimamia kwa vitendo.
“Hakuna chama hata kimoja chenye demokrasia ya kweli na hii inatokana na vyama kuanzishwa na watu kwa malengo yao. ACT-Tanzania inakuja kuwafuta machozi wanyonge wote kwani vyama 21 vilivyopo vimeshindwa,” alisema Limbu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) na kuongeza:
“Watu wameipora demokrasia, wanyonge wanahangaika kutafuta usawa katika huduma za jamii kama elimu, afya na nyinginezo. Sisi hatutakubali, tutahimiza usawa kwa kila kitu.”
Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi alithibitisha chama hicho kupata usajili wa muda na kusema kipo katika hatua za kusaka usajili wa kudumu.

MWANANCHI

Related

OTHER NEWS 3654200775035305893

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item