TAARIFA KUTOKA SEKRETARIETI YA AJIRA: UBORA WA WAHITIMU

UBORA WA WAHITIMU   Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichopewa jukumu la kuhakikisha kuwa Utumishi wa ...


UBORA WA WAHITIMU
 
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichopewa jukumu la kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unakuwa na watumishi wenye weledi wa hali ya juu kupitia mchakato wa ajira. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa inapata waombaji wenye sifa kitaaluma, uwezo na ujuzi ili kuufanya Utumishi wa Umma kuendeshwa na watumishi wenye weledi na maadili mema katika kuiwezesha Serikali kutimiza malengo yake kwa ufanisi.

Kwa kuwa nchi nyingi duniani na hususan kwenye Utumishi wa Umma zimeweza kuendelea kwa kasi kubwa kutokana na kuwa na rasilimaliwatu wenye kukidhi viwango na weledi wa hali ya juu.  Rasilimaliwatu yenye sifa ni nguzo muhimu katika utendaji kazi uliobora na wenye kufikia malengo katika sehemu yeyote iwe ya huduma au uzalishaji.

Upatikanaji wa rasilimali watu bora inategemea sana uwepo wa wahitimu bora toka kwenye vyuo au taasisi za elimu na elimu ya juu zilizopo katika nchi husika. Ndio maana Serikali ya Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikitilia mkazo suala zima la elimu ikiwemo kuwekeza katika sekta hiyo pamoja na kutoa fursa kwa watu binafsi, Mashirika na Taasisi mbalimbali kuanzisha Shule na Vyuo ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kutoa wahitimu wenye ubora wanaoweza kukabiliana na ushindani ulioko kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Pamoja na mikakati hiyo bado kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wahitimu kumaliza ngazi mbalimbali za elimu wakiwa wamemaliza na kupata vyeti lakini hawana uelewa wa kutosha wa kile walichokisomea (taaluma husika)kutokuwa na ufahamu wa kutosha wa mambo yanayoendelea kwenye mazingira husika. Maana ni matarajio ya wahitimu walio wengi pindi wamalizapo masomo wawe na uwezo wa kujiajiri ama kuajiriwa katika sekta binafsi au za Umma kutokana na weledi wa kitaaluma pamoja na uelewa mpana wa mambo yanayowazunguka ili kuweza kuendana na soko la ajira katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

Katika kipindi cha miaka minne ya kutekeleza jukumu hilo Sekretarieti ya Ajira imekabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ubora wa wahitimu wanaowasilisha maombi ya kazi Serikalini kuanzia waombaji wenye elimu ya ngazi ya sekondari, astashahada, stashahada, stashahada ya juu, shahada, shahada ya uzamili, pamoja shahada ya uzamivu.

Sekretarieti ya Ajira katika tathmini yake imebaini mapungufu mbalimbali yatokanayo na ubora wa wahitimu wanaoomba kazi kupitia chombo hiki ambao wamehitimu ngazi mbalimbali za elimu ikiwemo wanaotokea kazini.

Aidha, tofauti ya  mapungufu yao hutofautiana kutoka ngazi moja na nyingine, uwezo wa kitaaluma, ufahamu, Kuamini vyeti peke yake vinaweza kuwapa kazi pasipokuwa na uelewa mpana wa kile walichoombea kazi, kutotilia maanani sifa/vigezo na masharti ya tangazo husika, kutokujiamini, kukosa uzoefu kwa kazi inayohitaji uzoefu, uwezo mdogo wa mawasiliano ikiwemo matumizi ya lugha sahihi, uwezo mdogo wa kutumia nyenzo za utendaji kazi hususan vifaa vya kielekroniki, kutokujiandaa vya kutosha, kukosa mbinu za usaili na kutozingatia muda.

Changamoto nyingine ni kutokujitambua, kusoma kwa kufuata mkumbo, kukosa sifa halali za kitaaluma, kutokujua namna ya kuandika barua za maombi ya kazi, namna ya kuandika wasifu wao(CV), kutokuwa na maandalizi sahihi pamoja na kughushi baadhi ya sifa kwa lengo la kujipatia ajira.

Kwa upande wa wahitimu wanaoomba kazi wakitokea kazini baadhi yao wameonyesha udhaifu wa kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto hivyo kuona ni bora atafute kazi nyingine, kutokupitisha barua kwa waajiri, kukosa uelewa mpana unaoendana na uzoefu wake kazini ili kuweza kuonyesha tofauti yake na waajiriwa wapya, kukimbilia serikalini ili kupata fursa ya kusomeshwa lakini si kwa lengo la kwenda kuongeza tija kiutendaji.

Hali hii inadhihirisha kwamba wapo waombaji kazi ambao wanasoma ili kuhitimu au kufaulu na sio kuelewa kwa ufasaha fani wanazosomea ili kuweza kuleta utaalamu wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Jambo ambalo limekuwa likichangia wengi wao kushindwa kufikia hatua ya kuitwa kwenye usaili kutokana na kukosa baadhi ya vigezo na wengine kufikia hatua ya usaili na kushindwa kufaulu usaili husika kutokana na kutojiandaa ipasavyo.

Sekretarieti ya Ajira katika kukabiliana na changamoto ya upungufu unaotokana na ubora wa wahitimu kabla ya kuingia katika mfumo wa kutuma  maombi kwa njia ya Kielektroniki imeamua kuweka mapungufu haya kwa uwazi ili kusaidia wahitimu husika na wadau mbalimbali wa elimu katika kuzitatua changamoto hizo.

Aidha, Chombo hiki kitaendelea kutembelea sekta za elimu ikiwemo kushauriana na mamlaka na wadau mbalimbali wa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja ikiwemo kuandaa programu ya elimu kwa umma ili kuwawezesha waombaji wa kazi kuweza kutimiza vigezo vinavyohitajika ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata kazi husika wanazoomba.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma  +255-687624975.

Related

KAZI 281197305496359230

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item