BARAZA LA MITIHANI LABADILI MFUMO MZIMA WA KUPANGA MADARAJA YA UFAULU KIDATO CHA NNE NA SITA 2016.
Matokeo ya Mtihani wa Majaribio (Mock) kwa mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu na Kidato cha Sita mwakani, yatachangia alama 10 za Al...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/06/baraza-la-mitihani-labadili-mfumo-mzima.html
Matokeo ya Mtihani wa Majaribio (Mock) kwa mtihani wa Kidato cha Nne
mwaka huu na Kidato cha Sita mwakani, yatachangia alama 10 za Alama
Edelevu (CA).
Kwa utaratibu huu, matokeo ya mwisho ya mtahiniwa,
yatatokana na asilimia 30 ya Alama Endelevu na asilimia 70 ni mchango wa
Alama za Mtihani wa Taifa.
Asilimia 30 za Alama Endelevu, zitapatikana kutokana na mitihani
mbalimbali. Kwa Kidato cha Nne mwaka huu, alama hizo zitatokana na
matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili ambao utakuwa na alama
10, matokeo ya kidato cha tatu muhula wa kwanza na wa pili alama tano,
matokeo ya mtihani wa majaribio (mock) wa Kidato cha Nne ni alama 10 na
majaribio ya kazi alama tano.
Utaratibu huu umetokana na viwango vipya vya ufaulu, vilivyoainishwa
na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kwenye kitabu cha Mwongozo wa
Matumizi ya Viwango vya Ufaulu na utaratibu wa kutunuku matokeo ya
kidato cha nne na sita.
Kwa Kidato cha Sita, zitatokana na matokeo ya mtihani wa Kidato cha
Tano muhula wa kwanza na pili alama 15, matokeo ya 'mock' alama 10 na
kazi mradi itakuwa ni alama tano.
“Katika somo ambalo mtahiniwa hakufanyia Kazi za majaribio, alama za
matokeo ya Mitihani ya 'Mock' ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita,
itachangia alama 15 badala ya 10 zilizoainishwa,” imefafanua sehemu ya
mwongozo huo.
Hata hivyo, katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana na Kidato
cha Sita mwaka huu, mchanganuo wa alama 30 za Alama Endelevu ni alama 15
zinazotokana na matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili,
asilimia 10 ilitokana na maendeleo ya mitihani ya kidato cha Tatu muhula
wa Kwanza na Pili na matokeo ya muhula wa Kwanza Kidato cha Nne na kazi
za majaribio asilimia tano.
Kwa Kidato cha Sita, alama endelevu ni matokeo ya Kidato cha Tano
kwa mihula yote miwili ni alama 15, muhula wa kwanza wa Kidato cha Sita
ni asilimia 10 na kazi za majaribio ni asilimia tano.
Aidha, Baraza limebadili utaratibu wa kupanga madaraja ya kufaulu, kutoka mfumo wa Pointi na kuwa wa Wastani wa Alama za Mtahiniwa (GPA).
Mfumo unaotumiwa sasa wa pointi, huonesha wastani wa pointi
alizopata mtahiniwa kwa masomo aliyofaulu zaidi, na kupanga madaraja
kuanzia la kwanza hadi la nne.
Madaraja ya mfumo wa GPA, hupangwa katika utaratibu wa Distinction, Merit, Pass na Fail. Daraja la Distinction ni la ufaulu wa juu zaidi na daraja Pass ni ufaulu wa chini.
Mtahiniwa hutunukiwa madaraja A, B+, B, C, D, E au F kutegemeana na
ufaulu wake katika somo ambapo uzito wa alama katika madaraja A = 5, B+=
4, B = 3, C=2, D = 1, E = 0.5 na F = 0.
Mtahiniwa atahesabiwa kuwa amefaulu somo, endapo atapata Daraja D
ambayo ni sawa na uzito wa alama moja. Ukokotoaji wa jumla ya GPA ya
mtahiniwa hufanyika kwa kuzingatia masomo, ambayo mtahiniwa amefaulu
angalau kwa daraja D na kuendelea (D, C, B, B+ na A).
GPA anayopata mtahiniwa hutokana na wastani wa pointi alizopata
katika masomo saba aliyofanya vizuri zaidi kwa Mtihani wa Kidato cha Nne
au masomo matatu ya mchepuo kwa Mtihani wa Kidato cha Sita.
Aidha, GPA ya mtahiniwa huandikwa katika nafasi moja ya desimali
ambapo nafasi ya pili ya desimali hukadiriwa katika makumi yaliyokaribu.
Mfano, mtahiniwa mwenye GPA ya 3.15 itakuwa sawa na 3.2 na mtahiniwa mwenye GPA ya 3.14 itakuwa sawa na 3.1.
Muundo wa madaraja ya GPA kwa kidato cha nne, Distinction ni
3.6-5.0, Merit 2.6 -3.5, Credit 1.6-2.5, Pass 0.3-1.5, Fail 0.0-0.2
wakati Kidato cha sita ni Distinction 3.7-5.0, Merit 3.0-3.6, Credit
1.7-2.9, Pass 0.7-1.6, Fail 0.0-0.6.