NAIBU WAZIRI WA MAJI ATEMBELEA MIRADI YA MAJI MIKOA YA PWANI NA DAR ES SALAAM

  Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiambatana na wakandarasi wa kampuni ya WABAG pamoja na Meneja Mradi DAWASA, Inj. Romanus Mwang’...

 Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiambatana na wakandarasi wa kampuni ya WABAG pamoja na Meneja Mradi DAWASA, Inj. Romanus Mwang’ingo (mwisho kulia) wakikagua mradi wa maji wa Ruvu
 Ujumbe ulioongozana na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla ukiwa ndani ya tenki la maji lililopo Chuo Kikuu cha Ardhi.
 Meneja Mradi DAWASA, Inj. Romanus Mwang’ingo akimuonyesha Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla ramani ya mpango wa ujenzi wa matenki ya mradi wa maji Ruvu Juu mkoani Pwani unaoendelea kujengwa
 Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiwa na Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa wakiwa katika ‘kijiko’ katika eneo la ujenzi wa mradi wa maji Ruvu Juu, Pwani.
  Ramani ya mpango wa ujenzi wa mradi wa maji Ruvu Juu, Pwani.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla ameanza ziara yake ya siku nne ya kukagua miradi ya maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam leo, kwa kutembelea tenki la maji la Chuo Kikuu cha Ardhi na mradi wa maji Ruvu Juu.
“Serikali hailengi tu kuleta maji, ila pia kutatua tatizo la upotevu wa maji. Bali, tumejiandaaje kupokea maji ya kutosha kutokana na mradi mkubwa unaoendelea Ruvu Juu. Hivyo, hatuna budi kukarabati au kujenga kabisa upya matenki yote mabovu kabla ya kuanza kupata maji tunayotegemea’’, alisema Naibu Waziri akiwa katika mradi wa maji wa tenki la Chuo Kikuu cha Ardhi. 
Naibu Waziri aliendelea kwa kusema upotevu wa maji ambao ni asilimia 53 na hii inachangiwa na miundombinu mibovu na chakavu, na pia wizi wa maji uliokithiri. Nia kubwa ya Serikali ni kuhakikisha tatizo hilo linapungua kama sio kwisha kabisa.
Pia, Naibu Waziri alitembelea mradi wa Ruvu Juu kuangalia maendeleo ya upanuzi wa mradi huo, ambao unahusisha ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba mapya katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, ambao unafanywa na kampuni mbili kutoka India na mojawapo ikiwa ni WABAG ukisimamiwa na DAWASA.
Mhe. Makalla alisema kuwa mtambo wa Ruvu Juu ulijengwa miaka ya 70 na kwa sasa unahitaji ukarabati. Na ameridhishwa na matengenezo yanayoendelea katika mtambo huo, ambao unategemewa kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita za ujazo 82 mpaka 196.
Aidha, aliwahakikishia wakazi wa Pwani na Dar es Salaam kuwa Serikali iko makini na mradi huu na wategemee kero ya maji kutatuliwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.
Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa aliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kutatua kero ya maji katika mkoa wa Pwani na vitongoji vyake na kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo.
Ukarabati wa tenki la maji la Chuo Kikuu cha Ardhi unategemewa kukamilika baada ya siku 90 na sio 120 kama ilivyokua ikitegemewa hapo awali kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kryton inayosimamia ujenzi wa tenki hilo, Inj. Denis Kapella.
Aidha, ujenzi wa chujio la maji unategemewa kukamilika mwezi Agosti na ulazaji wa mabomba, mwezi Septemba katika mradi wa Ruvu Juu.

Related

OTHER NEWS 6112378510431697547

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item