WALIOTUPA VIUNGO VYA BINADAMU HADHARANI KUKIONA CHAMOTO
Tukio la utupaji wa viungo vya binadamu jalalani, linalodaiwa kufanywa na Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/07/waliotupa-viungo-vya-binadamu-hadharani.html
Tukio la utupaji wa viungo vya binadamu jalalani, linalodaiwa
kufanywa na Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) cha
Dar es Salaam, linadaiwa kuandika historia mbaya nchini.
Wakati serikali ikiendelea kuchunguza tukio hilo, ikiwemo kuunda tume
nyingine chini ya Wizara ya Afya na Ustawi, kujiridhisha kabla ya hatua
kuchukuliwa, Baraza la Madaktari limetwishwa mzigo wa kuhakikisha
linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho.
Imeeleza kwamba katika miaka yote, tangu mafunzo ya udaktari yaanze kutolewa nchini, halijawahi kutokea tukio kama hilo.
Serikali imetumia nafasi hiyo kuonya vyuo vingine, kwa kusema jambo
hili ni la kusikitisha, la aina yake katika historia ya mafunzo ya
udaktari tangu yaanze nchini takribani miaka 40 sasa.
"Pia tunatoa onyo kwa vyuo vingine, mafunzo haya tumeanza miaka 40
iliyopita lakini haijawahi kutokea kitu cha aina hii, ni mara ya kwanza
ni jambo la kusikitisha sana," alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na
Ustawi, Dk Steven Kebwe.
Naibu Waziri aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo hicho cha
kutupa viungo vya binadamu hadharani, si jambo la kawaida, ni la
uvunjifu wa haki za kibinadamu.
Alisema tangu Tanzania ipate uhuru wake, haijawahi kutokea tukio kama hilo, ambalo linatia hofu miongoni mwa wanajamii.
Katika kile kinachodhihirisha chuo hicho kung’ang’aniwa, kabla ya
kuamua hatua za kuchukua dhidi yake, Wizara hiyo yenye dhamana ya afya,
pia imeunda kamati ya watu 15 kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.
Kamati hiyo ya wizara iliyopewa siku saba kukamilisha kazi, imeundwa
kukiwa na tume nyingine iliyoundwa na Polisi Kanda ya Dar es Salaam,
kuchunguza sakata hilo la kutupwa viungo katika maeneo ya Bonde la
Mbweni Mpiji, Bunju jijini Dar es Salaam.
Dk Kebwe aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati hiyo ya wizara
itafanya kazi yake kwa siku saba kuanzia juzi. Inajumuisha wataalamu
mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Polisi na Wizara ya Afya na
Ustawi.
Aidha, alisema zipo sheria zinazoelekeza namna ya kuteketeza miili hiyo baada ya kumalizika kwa kazi yake.
“Lakini inasikitisha kuona miili hiyo ilitelekezwa na watu wanaojua maadili ya kazi ya udaktari,” alisema.
Alisema kwa kuwa madaktari huwa wanakula viapo baada ya kumaliza
mafunzo yao, Baraza la Madaktari nchini linatakiwa kuhakikisha
linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho.
Timu iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
imejielekeza kuja na majibu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufahamu idadi
kamili ya watu wenye viungo hivyo.
Ikiwa na watu saba akiwemo Mkemia Mkuu wa Serikali, itakuja na
majibu yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika
kemikali gani kuvikausha.
Pia, jopo hilo litabaini kama ipo sheria na ni ipi inavunjwa.
Wataalamu hao wanalenga kubaini, pia kama upo uzembe katika kulinda
viungo vya binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya mazoezi.
Katika sakata hilo, lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani
na kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo madaktari wa IMTU,
walikamatwa na Polisi kwa mahojiano, wakituhumiwa kuhusika katika
utupaji viungo vya binadamu jalalani.
Kwa mujibu wa Polisi, mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono,
moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa
maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.