MAALIM SEIF ATEMBELEA ENEO LA JENGO LILILOANGUKA JANA MJI MKONGWE ZANZIBAR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akimsikiliza Kamanda Ame Ali ambaye ni kiongozi wa shughuli za ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/11/maalim-seif-atembelea-eneo-la-jengo.html
Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akimsikiliza
Kamanda Ame Ali ambaye ni kiongozi wa shughuli za usafishaji wa eneo
lilipoanguka jengo la ghorofa huko Shangani mjini Zanzibar.
Na Khamis Haji , OMKR
Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amezitaka
Mamlaka zinazosimamia majengo katika enelo la Mji Mkongwe Zanzibar kuwa
na utaratibu mzuri wa kuyakagua ili kuhakikisha uimara wake na kuepusha
maafa kwa watumiaji na jamii nzima.
Maalim Seif
amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za uondoaji
kifusi katika jengo lililoanguka jana katika eneo la Shangani mjini
Zanzibar, zoezi linalofanywa na askari wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa
pamoja na wananchi wa Mji Mkongwe.
Makamu wa
Kwanza wa Rais amesema nyumba zilizopo katika Mji Mkongwe zinasimamiwa
na Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya Mji Mkongwe au Kamisheni ya Wakfu na Mali
ya Amana, hivyo taasisi hizo ni jukumu lao kuzigagua uimara wake na
kuhakikisha ni madhuti.
Amesema pale
ambapo taasisi hizo zitabaini kuna nyumba ambazo zimechakaa zinazoweza
kuanguka na kuhatarisha maisha ya watu na mali zao ni vyema kuwataka
watumiaji wake wahame, ili kuepusha kuangukiwa na nyumba hizo na
kuhatarisha maisha yao.
Katika ziara
hiyo, ambapo alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla
Mwinyi Khamis na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Mhe. Ismail Jusa
Ladhu alivipongeza vikosi vinavyoendesha shughuli za Uokoaji na wananchi
wa Mji Mkongwe kwa kazi kubwa ya uokozi wanayoifanya.
Naye Mkuu wa
Kituo cha Zimamoto na Uokozi Makao Makuu, Ame Ali ambaye anaongoza
shughuli za uokozi na usafishaji wa eneo hilo amesema kazi hiyo
inaendelea vizuri na walitarajia kuikamilisha leo.
Amesema jengo
hilo lililoanguka jana asubuhi lilikuwa halikaliwi na watu kutokana na
kukabiliwa na uchakavu na hakuna mtu aliyepoteza maisha au kujeruhiwa
kufuatia tukio hilo.