MDEE: JIANDIKISHENI KATIKA DAFTARI KUEPUSHA WIZI WA KURA

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee Wakati miezi tisa ikiwa imebaki Tanzania kufanya uchaguzi mkuu, Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa ...

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee


Wakati miezi tisa ikiwa imebaki Tanzania kufanya uchaguzi mkuu, Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kuepuka vitendo vya wizi wa kura.

Rai hiyo ilitolewa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuwapongeza viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kata ya Makongo, jana jijini Dar es Salaam.
Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema Taifa (Bawacha), aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwani kwa kutokufanya hivyo kutatoa mwanya wa kuibiwa kura na hivyo kuwapata viongozi ambao hawakuwachagua katika uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika nchi nzima Oktoba mwaka huu.

Alisema Tanzania siyo mali ya viongozi wa siasa bali ya Watanzania na ndiyo wenye uwezo wa kufanya mabadiliko na kwamba kura ndiyo suluhisho kubwa dhidi ya matatizo mengi yanayojitokeza nchini yakiwamo ya ufisadi wa uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

“Nchi hii siyo ya Mbowe, Lipumba, Mbatia au Makaidi. Nchi hii ni ya kwetu Watanzania. Wananchi ndiyo wenye wajibu wa kuibadilisha nchi hii,” alisema Mdee.

Kauli hiyo ni moja ya tahadhari kuepuka dosari ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati chaguzi ukiwamo wa serikali za mitaa Desemba 14, mwaka jana kutokana na kujitokeza kwa idadi ndogo ya wananchi kupiga kura kutokana na kutojiandikisha katika daftari.

Aidha alieleza kutoridhishwa kwake na maamuzi yaliyotolewa dhidi ya waliohusika kwenye kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, akisema kwamba haiwezekani watu wachote fedha hizo na kuzijaza kwenye ‘mapipa’ halafu wanaambiwa warudishe bila hatua zingine zozote.

Alisema, zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilizochotwa kwenye akaunti hiyo ni nyingi kwani mtu anaweza kuzitumia kwa matumizi ya kawaida ya Shilingi 20,000 kila siku kwa miaka 50 ijayo.

Naye Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Edward Simbei, alisema, chama hicho hakitawavumilia viongozi ambao watakiuka maadili ya chama na kushindwa kuwatumikia wananchi na kujifanya miungu watu.

Related

TUJUZANE 8654427989170157478

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item