ZITTO KABWE NJIA PANDA, CHADEMA WAMFUKUZA

Zitto Kabwe Dar es Salaam. Hali ya kisiasa ya mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe imewekwa njiapanda baada ya Chadema kutanga...

Zitto Kabwe

Dar es Salaam. Hali ya kisiasa ya mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe imewekwa njiapanda baada ya Chadema kutangaza kumvua uanachama saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyofungua dhidi ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Zitto, ambaye amedumu kwenye nafasi ya ubunge kwa takriban mwaka mmoja kutokana na amri ya mahakama, sasa atalazimika kuamua kutangaza rasmi kujiunga na chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT) kama alivyokuwa amepanga kufanya wiki ijayo, au kukata rufaa mahakamani ili aendelee na majukumu yake ya kibunge hadi hapo muda muafaka utakapowadia.
Lakini mbunge huyo mwenye umri wa miaka 36, aliiambia Mwananchi muda mfupi baada ya kutangazwa kutimuliwa kwake kuwa hakuwa na taarifa za kuwapo kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu jana na kwamba leo ataendelea kuchapa kazi za Bunge wakati atakapoiongoza Kamati ya Hesabu za Serikali kupitia matumizi ya Shirika la Umeme (Tanesco).
Akitangaza kutimuliwa kwa Zitto, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa kufungua kesi mahakamani, naibu katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema alikiuka katiba ambayo hairuhusu migogoro ya ndani ya chama kupelekwa mahakamani.
Alinukuu Sehemu ya Kwanza ya Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chadema, kipengele cha 8 (a) (X), inayosema: “Chadema itashughulikia matatizo ya viongozi na wanachama kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama, wala hata siku moja haitashughulikia mambo kama hayo mahakamani. Mwanachama atakayeshindwa kufuata taratibu na ngazi za chama hatavumuliwa na atafukuzwa uanachama.”
Lissu alisema Zitto alikiuka kipengele hicho kutokana na kufungua kesi Mahakama Kuu kushughulikia matatizo yake ndani ya chama.
Katika kesi yake Zitto, ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, alikuwa anataka mahakama hiyo imwamuru katibu mkuu wa Chadema ampe mwenendo na taarifa za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama.
Mbunge huyo pia aliomba na kufanikiwa kupata amri ya muda ya kuizuia Chadema, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote wala kumjadili kuhusu uanachama wake, hadi hapo rufaa aliyokuwa anakusudia kukata Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia amri hiyo ilizuia walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Zitto alifungua kesi hiyo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema.
Katika uamuzi wake jana, Jaji Richard Mziray ilitupilia mbali kesi hiyo na kumwamuru Zitto akilipe chama hicho gharama za kesi hiyo.
Jaji Mziray alijikita katika hoja mbili tu za pingamizi, akieleza kuwa kesi ilitakiwa kufunguliwa kwenye Masjala ya Wilaya ya Mahakama Kuu badala ya Masjala Kuu ya Mahakama Kuu.

Kwa hoja hizo mbili, Jaji Mziray alisema kuwa hoja hizo zinatosha kutupilia mbali shauri hilo na kwamba hakuwa  na haja ya kuendelea na hoja nyingine za pingamizi.
Jaji Mziray alisema kuwa mlalamikaji alipaswa kufungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na si Mahakama Kuu.
Pia alisema kuwa hata kama alikuwa na uhalali wa kufungua kesi hiyo Mahakama Kuu, basi alipaswa kuifungua katika Masjala ya Wilaya na si Masjala Kuu.
Wakati uamuzi huo unatolewa, Zitto na Wakili wake hawakuwepo mahakamani hapo.
Akifafanua kutimuliwa kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, Lissu alisema kuwa kwa sasa hakuna sababu ya kuitisha kikao cha Kamati Kuu kwa ajili ya kumtimua Zitto kwa sababu alikimbilia mahakama kuzuia vikao vya juu kumjadili tofauti na Katiba inavyoeleza.
Alirejea sehemu hiyo ya kusimamia shughuli, mienendo na maadili ya wabunge wa Chadema, kipengele cha tisa kinachosema: Mkutano Mkuu utakuwa na maamuzi ya mwisho kwa jambo lolote na pande zinazohuika ni lazima ziti maamuzi ya mkutano mkuu. Mtu yeyote atakayeshindwa kutii uamuzi wa Mkutano Mkuu atakuwa ametofautiana na Chama na kuanzia saa hiyo uanachama wake utakuwa umekoma.”
“Kama (aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Arusha, Samson) Mwigamba na (mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Kitila) Mkumbo, wangeenda mahakamani kama Zitto, wangekuwa wameshafukuzwa kabla ya kujadiliwa na Kamati Kuu. Lakini Zitto alikimbilia mahakama kuizuia Kamati Kuu kumjadili na hivyo ilikuwa automatic,” alisema Lissu.
“Kitakachofanyika kwa Kamati Kuu ni ku-take note tu (kuchukua taarifa) kwamba Zitto amefukuzwa, hakuna haja ya kuitisha kikao cha Kamati Kuu kwa ajili ya kumjadili na kumtimua.”
Lissu alisisitiza kuwa Zitto alikuwa akilijua hilo kwa kuwa wakati Katiba hiyo inaandaliwa alishiriki kwa kuwa alikuwa ni kiongozi na kama hakulijua basi alipaswa kulijua.
“Kitendo cha Zitto kufungua kesi katika mahakama za kisheria amekiuka Katiba. Kwa kuwa amefanya hivyo kinachofuata ni malipizo ya ukiukwaji wa masharti ya chama.
Lissu alisema kuwa baada ya uamuzi huo wa mahakama sasa vyombo rasmi vya chama vitakaa na kufanya uamuzi na kuchukua hatua.
Alibainisha hatua hizo kuwa ni pamoja kuitaarifu Mahakama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa kwa sasa Zitto si mwanachama tena wa Chadema.

 “Katiba ya nchi inasema kuwa mbunge akikosa uanachama wa chama kilichomdhamini, anapoteza sifa ya kuwa mbunge,” alisema Lissu.

 “Hivyo tutapeleka taarifa kwa Nec ili wamweleze spika kuwa jimbo la Kigoma Kaskazini liko wazi kwa kuwa aliyekuwa mbunge wake si mwanachama wa chama kilichomdhamini.”
Uamuzi wa Mahakama Kuu na wa Chadema unaonekana umekuja wakati ambao Zitto alikuwa amepanga kuachia ubunge na kutangaza uamuzi wake wa kujiunga na ACT.
Zitto amekuwa akihusishwa na ACT tangu kuibuka kwa mgogoro huo baina yake na viongozi wa Chadema, ikielezwa kuwa yeye ndiye aliyesuka mipango ya kukianzisha, ingawa amekuwa haielezi bayana.
Habari kutoka kwa watu walio karibu naye zinaeleza kuwa Zitto alikuwa amepanga kuagana na wanachama wa Chadema wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na baadaye kwenda kuhudhuria kikao cha Bunge mjini Dodoma kinachoanza Jumanne, lakini siku inayofuata Jumatano au Alhamisi atangaze rasmi kujiondoa Chadema.
“Huyu bwana anachangia bungeni tarehe 18 au 19 mwezi huu, atatumia nafasi hiyo kutangaza kujiondoa Chadema,” alisema mmoja wa marafiki wa Zitto.
Hata hivyo, Zitto alisema kwa ufupi kuwa msimamo wake kuhusu kubaki au kujiondoa Chadema utajulikana mwezi huu.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa ambaye alikuwa ni mmoja wa wadaiwa katika kesi ya Zitto alisema kuwa amefurahishwa na uamuzi huo wa mahakama, akisema msimamo wake kuhusu hatima ya Zitto ni kama ilivyoelezwa na Lissu.
Hoja za pingamizi la Chadema
Katika kesi hiyo, mawakili wa Chadema, Peter Kibatala, ambaye pia ni mkurugenzi wa sheria wa chama hicho na John Mallya, walitoa hoja kadhaa za kutaka mahakama itupilie mbali kesi hiyo.
Pamoja na mambo mengine walidai kuwa kesi hiyo imekosewa kwa kufunguliwa Mahakama Kuu badala ya kufunguliwa katika mahakama ya chini. Pia walidai kuwa kesi hiyo imefuguliwa kimakosa katika Masjala Kuu ya Mahakama Kuu, badala ya kufunguliwa  Masjala ya Wilaya ya  Mahakama Kuu.
Uamuzi wa mahakama
Wakili wa mlalamikaji, Albert Msando alidai kuwa Zitto ana uhuru wa kufungua kesi katika masjala yoyote, lakini mahakama katika uamuzi wake ilikubaliana na hoja za pingamizi la walalamikiwa.
Zitto anena
Akizungumzia uamuzi huo wa mahakama, Zitto alisema: “Mimi kwanza sikuwa najua kama hukumu hiyo inatolewa leo (jana) na nimepata taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii. Lakini nilichokuwa najua mimi kesi hiyo ilikuwa isikilizwe Machi 12 na si leo kama ilivyokuwa.”
Zitto, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema: “Nimemtuma mwanasheria wangu kwenda mahakamani kupitia uamuzi huo wa mahakama na kujua kwa nini imekuwa leo (jana) kwani hata jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo kahamishiwa Tabora na tulikuwa tunasubiri kujua ni nani atakayeisimamia.
 “Naendelea na majukumu yangu kama kawaida, kamati inaendelea na vikao vyake (ofisi ndogo za Bunge) na kesho (leo) tutakuwa na Shirika la Umeme (Tanesco) kupitia matumizi yao.
“Keshokutwa (kesho) tutashughulikia mabilioni ya Uswisi na tayari tumewaita Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kamishna ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili waje watueleze walipofikia kuhusu fedha hizo.”
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando alisema awali kesi hiyo ilikuwa isikilizwe Novemba 11 mwaka jana, lakini Jaji aliyekuwa anaisikiliza alikuwa jijini Mwanza katika mkutano wa majaji hivyo iliahirishwa hadi Machi 12 mwaka huu.
“Nimefuatilia mahakamani na imeonekana tena Februari 25 mwaka huu na katika rekodi za mahakama zinaonyesha sisi hatukuwa na taarifa na kama kulikuwa na mabadiliko ya tarehe, basi mahakama ilitakiwa kutoa hati ya wito, lakini yote hayo hayakufanyika,” alisema Msando.

MWANANCHI.

Related

OTHER NEWS 4852667796682311080

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item