Hospitali ya AMI kufurushwa kwa kutolipa kodi ya pango ya bilioni tatu

Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara imeamuru kufurushwa kwenye jengo hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama ...




Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara imeamuru kufurushwa kwenye jengo hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Center ya Msasani Jijini Dar es Salaam, baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi 26, inayofikia zaidi ya dola za kimarekani milioni 1.6 (zaidi ya Shilingi Bilioni tatu za Kitanzania).
Hatua hii imefikiwa baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria baina ya AMI na mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki wa jengo hilo, Bw. Navtej Singh Bains.
Akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zimekutwa zikiwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.
Amri hiyo iliyotolewa wiki iliyopita (tarehe 7 Mei, 2015) na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, imeipa mamlaka kampuni ya mnada ya MEM (MEM Auctioneers and General Brokers Limited) kuifurusha Hospitali ya AMI kutoka kwenye jingo ambapo kampuni hiyo inafanya biashara yake.
Amri hiyo ya kutoka kwenye jengo itaanza mara baada ya kuisha kwa kipindi cha notisi cha siku kumi na nne ambacho kimeshatumiwa na AMI.
“Ikiwa mdeni aliyetajwa katika hukumu hapo juu (African Medical Investment Limited –AMI) ameamuriwa kwa amri ya mahakama hii ya tarehe 9 mwezi Septemba, 2014 kuondoka na kukabidhi jengo, na ikiwa bado hajaondoka na kukabidhi jengo lenyewe.
“Unaelekezwa kumwondoa mdaiwa/wadaiwa au mtu yeyote anaefanyakazi chini yake atakayekataa kuondoka kwenye jengo na kumuweka anaemiliki amri hii ya mahakama (Navtej Singh Bains- Mwenyenyumba) kwenye nyumba yake,” inasomeka sehemu ya amri ya mahakama iliyoelekezwa kwa kampuni ya mnada ya MEM (MEM Auctioneers).
Amri hii sasa inapelekea kufungwa kwa Hospitali ya AMI, licha ya rufaa zake za kujaribu kuzuia kufukuzwa, imefikiwa baada ya hospitali hiyo kushindwa kutimiza amri ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania iliyoamuru kulipwa kwa dola za kimarekani milioni 1.514 mahakamani pamoja na kodi ya kila mwezi ya kiasi cha dola za kimarekani 64,000 kila mwezi kufuatia mgogoro wa kodi ya jengo.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Mbarouk, Salum Massati na Katherine Oriyo waliiamuru Hospitali ya AMI kufanya malipo hayo ndani ya mwezi mmoja baada ya hukumu iliyotolewa Februari 12, 2015, agizo ambalo halijatekelezwa.
Mahakama ilitoa uamuzi huo kwenye kesi No. 185 ya mwaka 2014 iliyofunguliwa na AMI kupinga utekelezaji wa amri iliyotolewa kwenye kesi No. 104 ya mwaka 2013 ambapo ilishindwa kesi na mwenye nyumba wao (Mfanyabiashara wa ndani Navtej Singh Bains) iliyohusiana na jengo ambalo kampuni hiyo inaendesha biashara yake.
Hospitali ya AMI ilishindwa katika kesi iliyofunguliwa na mwenye nyumba wao baada ya kushindwa kulipa kodi kwa kipindi cha miezi 26 iliyopita katika malumbano/mabishano ya kisheria kwenye Mahakama ya Biashara ya Tanzania Novemba 2014 na walipewa notisi ya kuhama na mwenye nyumba huyo.
Kufuatia hukumu hiyo, AMI ilipeleka ombi la kuwa imefilisika katika Mahakama Kuu ya Tanzania ikieleza kuwa imekuwa ikijiendesha kwa madeni baada na kupata hasara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa AMI Plc, Bw. Theunis Peter Botha, ambaye pia ni Mkurugenzi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya AMI Tanzania, aliwasilisha ombi hilo kuwa imefilisika katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Katika shauri hilo la ufilisi lililofunguliwa wiki iliyopita kwa Msajili wa Mahakama Kuu, kampuni hiyo inadai kuwa imekuwa ikikumbana na hasara za mabilioni ya shilingi jambo lililopelekea kuwepo kwa madeni yaliyokithiri ambayo kwa sasa yako nje ya uwezo wa kampuni kulipa.
“Mlalamikaji (AMI) anadai kuwa alipata hasara halisi ya Dola za kimarekani 1.146 katika mwaka uliomalizika Februari 28, 2013, huku kwa mwaka uliomalizika Februari 28, 2014, mlalamikaji alipata hasara halisi ya Dola za Kimarekani 775,000,” inasomeka sehemu ya hati ya malalamiko.
AMI Tanzania inamilikiwa na Kampuni mama ya AMI Plc ya London ambayo iliondolewa kwenye Soko la Hisa la London mnamo Februari 2014 baada ya jaribio la kuuza mali zake zilizopo nchini Maputo bila kibali kutoka kwa wanahisa.
Inaelezwa kuwa kampuni hiyo ilitakiwa pia kufanya malipo kwa taasisi mbalimbali, zikiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na watu na makampuni binafsi.
Kwa mujibu wa shauri hilo, ukichukulia thamani ya mali za kampuni na kiasi cha fedha zinazodaiwa na wadai, kulikuwa hakuna njia ya kuweza kupata fedha za kutosha kuwalipa sambamba na kutekeleza majukumu yake.
Pia kuna kumbukumbu zinazoonyesha kuwa Lancet Laboratory (T) Ltd iliwasilisha ombi la dharura dhidi ya kufungiwa kwa Hospitali ya AMI ikiwa inaidai hospitali hiyo zaidi ya Shilingi Milioni 150.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa wadai mbalimbali wako njia panda kutokana na deni kubwa la Dola za Kimarekani Milioni 4 wanaloidai hospitali hiyo. Wadai wakubwa ni pamoja na mmiliki wa jengo Bw. N Bains, Madaktari, Wafanyakazi, TRA, Wasambazaji wa madawa na Wasambazaji wengine. 



Source:  dewjiblog

Related

OTHER NEWS 1425974709276087306

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item