MAELEZO YA KATIBU MKUU WA CUF NA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWENYE MKUTANO NA VYOMBO VYA HABARI DAR ES SALAAM SERENA HOTEL, 10 MEI, 2015
Ndugu zangu Wahariri na Waandishi wa Habari, Assalam Alaykum. Awali ya yote, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtu...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2015/05/maelezo-ya-katibu-mkuu-wa-cuf-na-makamu.html
Ndugu zangu Wahariri na Waandishi wa Habari,
Assalam Alaykum.
Awali
ya yote, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia
kukutana wakati huu katika eneo hili kwa ajili ya mkutano huu maalum na
waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Ndugu
wanahabari, kama sote tujuavyo, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu
ambao umepangwa kufanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 kama ilivyokwisha
tangazwa na Tume za Uchaguzi.
Ndugu
wanahabari, Uchaguzi wa mwaka huu ni Uchaguzi wa aina yake na wa
kipekee kutokana na ukweli kwamba Watanzania sasa wameungana kutaka
mabadiliko ya dhati na ya kweli na wamejiandaa kukiondoa madarakani
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeisaliti dhamana kiliopewa
kuwaongoza na badala yake kujikita katika ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka huku wakijinufaisha wao, familia na marafiki zao. Kwa upande wa
Zanzibar, Wazanzibari wameamua kujiunga na wimbi la kihistoria la kudai
na kupigania kurejesha Mamlaka Kamili ya Zanzibar chini ya Chama Cha
Wananchi (CUF), kwa kuzingatia siasa za kistaarabu, demokrasia, umoja wa
kitaifa na kuweka mbele maslahi mapana ya Taifa letu.
Hata
hivyo, wakati nchi ikishuhudia vuguvugu hilo, Tume za Uchaguzi hapa
nchini kwa maana ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC) ambazo ndizo zilizopewa mamlaka kikatiba na kisheria
kubeba dhamana ya kuendesha na kusimamia chaguzi katika nchi zetu
zinaonekana bado zinashindwa kuachana na maradhi sugu yanayozikabili ya
kutumiwa na CCM na wao kukubali kutumika kukandamiza maamuzi huru ya
wananchi.
Leo
hii, tumeamua kuwaita hapa kuzungumzia hali halisi ya utendaji wa Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wakati tunaelekea katika uchaguzi mkuu wa
2015 na hasa tunapoelekea uandikishaji wa mwisho wa wapiga kura kabla ya
uchaguzi huo, uandikishaji ambao umepangwa kuanza tarehe 16 Mei na
kukamilika tarehe 28 Juni, mwaka huu.
Ndugu
wanahabari, mbali na ukweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa
ni wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini,
dalili zote zinaoenesha kuwa hakuna nia ya dhati ya kustawisha
demokrasia kupitia msingi wake muhimu, ambao ni uchaguzi, tulioamua
kufanyika kila baada ya kipindi cha miaka mitano. Tunasema hayo kutokana
na hadaa nyingi zilizojitokeza awali na wakati huu tunapojitayarisha
kuingia katika uandikishaji wa mwisho wa wapiga kura katika Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura (DKWK).
Mtakumbuka
kwamba chaguzi zote za Zanzibar kuanzia ule wa mwaka 1995, 2000, 2005
na ule 2010, ambao kwa kiasi ulikuwa huru lakini usio wa haki,
zilikabiliwa na kukumbwa na kasoro kadhaa kubwa kama vile uandikishwaji
wa wapiga kura zaidi ya mara moja, uandikishwaji wa wapiga kura wasio
wakaazi katika eneo la uandikishwaji hasa vikosi vya ulinzi na usalama
kwa upande wa Zanzibar, uandikishwaji wa wapiga kura walio chini ya umri
na kunyimwa kwa baadhi ya wapiga kura haki yao ya msingi ya
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. Pale yote haya
yaliposhindwa kufikia lengo lililokusudiwa la kuipa ushindi haramu CCM
kupitia wapiga kura haramu basi nguvu zilitumika na mwishowe matokeo ya
uchaguzi kubadilishwa na kumtangaza aliyeshindwa kuwa mshindi.
Ndugu
wanahabari, mnakumbuka vyema jinsi nchi yetu ilivyokumbwa na balaa na
maafa yaliyosababishwa na kasoro hizi za Uchaguzi ambazo kwa kiasi
kikubwa zinaratibiwa na wasaliti waliotanguliza mbele maslahi yao
binafsi na kufanikishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
iliyokubali kutumiwa kuhujumu, kudhalilisha na kukandamiza demokrasia
nchini.
Kutokana
na ukweli huo, ni vyema tukatambua kwamba mizozo yote ya kisiasa
Zanzibar huanzishwa na kuchochewa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za
Uchaguzi zilizowekwa hasa kuanzia hatua ya uandikishwaji wa wapiga kura,
uhesabuji wa kura hizo na utangazwaji wa matokeo ya uchaguzi
Matukio
ya vitisho, vipigo na mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia
yaliyotekelezwana Jeshi la Polisi tarehe 26 na 27 Januari, 2001 Unguja
na Pemba na hatimaye nchi kuzalisha wakimbizi katika kambi za Shimoni na
Dadaab, nchini Kenya ni sehemu ya matukio mabaya na kumbukumbu
inayoumiza katika historia ya nchi yetu inayotokana na ukiukwaji wa
Sheria za Uchaguzi hasa uandikishaji wa wapiga kura kunakofanywa kwa
makusudi na Tume ya Uchaguzi kwa lengo la kuibeba na kuisaidia CCM.
Sote
ni mashahidi wa jitihada kubwa zinazochukuliwa na zinazoendelea
kuchukuliwa na CUF kila baada ya Uchaguzi Mkuu ili kuiepusha nchi na
mawimbi mazito ya migogoro ya kisiasa, mipasuko ya kijamii na kuhuisha
mahusiano ya kidiplomasia na mataifa washirika wa maendeleo kama
ilivyoshuhudiwa miaka iliyopita kufuatia kuvurugwa kwa makusudi kwa
chaguzi.
Ndugu
wanahabari, kama nilivyokwisha kueleza, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
imetangaza kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura wapya katika
maeneo mbali mbali ya Zanzibar kuanzia tarehe 16 Mei, 2015 na
kumalizika tarehe 28 Juni, 2015. Hii ndio kusema kwamba hatua za awali
za matayarisho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 zimeanza.
Ni
katika muktadha huu, wa kuwa na Tume iliyoamua kuendelea kutumiwa
kuingiza nchi katika vurugu za makusudi kwa sababu tu ya kutaka
kukiridhisha Chama Cha Mapinduzi ambacho hakitakiwi tena na wapiga kura,
The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kimeamua kukuiteni
wanahabari kwa lengo la kukuelezeni, na kupitia nyinyi kuwaeleza
wananchi na dunia, juu ya mambo matatu yafuatayo:
1. Uchafu uliomo katika Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
Kitengo cha Sera, Utafiti na Mafunzo cha CUF.
2. Mipango ya uchafuzi inayofanywa sasa
ya kuyarudia yale yaliyofanywa katika uandikishaji wa wapiga kura
uliopita katika uandikishaji wa wapiga kura wapya unaotarajiwa kuanza
wiki ijayo.
3. Mpango wa kuchelewesha ukataji wa mipaka ya majimbo kwa shinikizo za Sekretarieti ya CCM Zanzibar.
4. Kutofanyiwa marekebisho Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Ndugu
wanahabari, kwa hili la kwanza linalohusu Uchafu uliomo katika Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar, ili muweze kujionea wenyewe na kwa
ushahidi na vielelezo yale niliyoyataja kabla, naomba nimpe nafasi Mkuu
wa Kitengo cha Sera, Utafiti na Mafunzo cha CUF, Mhe. Hassan Jani
Masoud, awasilishe matokeo ya utafiti waliyoufanya katika Daftari hilo
ambao unabainisha kuwepo kwa:
Wapiga Kura wenye Umri Mdogo;
Wapiga Kura walioandikishwa zaidi ya mara moja (Multiple Registration);
Wapiga Kura Waliokufa;
Wapiga kura ambao si wakaazi katika maeneo waliyojiandikisha (Mapandikizi);
Wapiga Kura waliotumia majina au picha ambazo sio zao;
Idadi ya wapiga kura iliyozidi katika utolewaji wa vipande vya Kura.
Ndugu
wanahabari, kuhusiana na suala la pili, ambalo ni Mipango ya uchafuzi
inayofanywa sasa ya kuyarudia yale yaliyofanywa katika uandikishaji wa
wapiga kura uliopita katika uandikishaji wa wapiga kura wapya
unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, hivi tunavyozungumza kunaendelea zoezi
kubwa la kuandaa wapiga kura haramu ili waweze kuja kuandikishwa.
Maandalizi
hayo yanahusisha Idara ya Usajili wa Wazanzibari ambayo ndiyo hutoa
Vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN IDs), Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya, Masheha, Sekretarieti ya ZEC na la kusikitisha zaidi , hata
Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama. Miongoni mwa mambo yanayofanyika ni
pamoja na:
1.
Kutumiwa Kambi ya JWTZ iliyopo Chukwani, kisiwani Unguja kuandikisha
mamia ya vijana wakiwemo wengi ambao si Wazanzibari na kuwapatia
Vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN IDs) kwa ajili ya kuja kuandikishwa
kama wapiga kura. Vijana hawa walikuwa wakipelekwa katika kambi hiyo kwa
magari maalum kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita na kuanza wiki
iliopita wameitwa na kuanza kupewa vitambulisho hivyo haramu. Miongoni
mwao wamepatiwa vitambulisho vinavyoonesha anuani zao ni eneo la
Darajani lakini wamepelekwa kambi ya JWTZ Chukwani kwenda kusajiliwa kwa
siri.
2. Katika majimbo mbali mbali ya visiwa
vya Unguja na Pemba kumeandikishwa vijana wanaofikia 20,000 na kupewa
ZAN IDs ambao wamepangwa kuja kuandikishwa kama wapiga kura. Wengi kati
ya vijana hawa wamehamishwa kutoka nje ya majimbo yao. Kwa mfano, kuna
vijana 700 waliochukuliwa katika maeneo mbali mbali ya jimbo la Uzini na
ambao wamepelekwa kusajiliwa katika jimbo la Bububu kisiwani Unguja,
vijana wapatao 10,000 waliohamishwa kutoka Wilaya ya Kati Unguja na
kusajiliwa katika majimbo ya Dimani na Mtoni katika Wilaya ya Magharibi
Unguja na majimbo ya Chumbuni na Kwamtipura katika Wilaya ya Mjini
Unguja. Pia kuna vijana 1,200 wamepatiwa ZAN IDs kwa ajili ya kuja
kuandikishwa katika jimbo la Chonga na wengine 1,000 katika jimbo la
Mkanyageni, kisiwani Pemba.
3. Katika Mkoa wa Kaskazini Unguja,
watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka 18 wengi wao wakiwa baina ya
miaka 14 hadi 17 wamekuwa wakichukuliwa na kupelekwa kituo cha kusajili
vitambulisho vya Mzanzibari kilichopo Gamba ambako wamepatiwa ZAN IDs na
sasa wanasubiri kuandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura. Jimbo la
Tumbatu limekuwa likiongoza katika suala hili.
Ndugu
wanahabari, suala la tatu linahusu ucheleweshaji wa ukataji wa mipaka
ya majimbo ya uchaguzi chini ya usimamizi wa Sekretarieti ya ZEC. Kazi
hii ilipaswa iwe imeshakamilika muda mrefu uliopita na Makamishna wa
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walizunguka katika majimbo yote ya Unguja
na Pemba na kuchukua maoni ya wananchi. Tunazo taarifa za kuaminika
kabisa kwamba Tume ilikwisha kamilisha kazi hiyo kwa kuzingatia maoni
yaliyotolewa na wananchi na ripoti ya mapendekezo kutayarishwa. Hata
hivyo, kwa sababu mapendekezo hayo hayakukiridhidha Chama Cha Mapinduzi,
mapendekezo hayo yaliwekwa upande na sasa CCM imeitumia Wizara ya
Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuandaa mapendekezo mengine
ambayo yameandaliwa kwa lengo la kupunguza majimbo katika maeneo yenye
wafuasi wengi wa CUF na kuongeza majimbo kwenye maeneo yenye wafuasi
wengi wa CCM. Hadi hii leo, Tume ya Uchaguzi imekuwa ikiahirisha kila
mara kutangaza majimbo hayo kwa kusubiri maelekezo hayo ya CCM kupitia
Wizara ya Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ.
Ndugu
wanahabari, suala la nne na la mwisho linahusu marekebisho ya
Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Mtakumbuka kwamba wakati
CUF ilipokubali kuridhia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010,
ilimtaka Dk. Ali Mohamed Shein kusimamia mambo mawili, ambayo ni
kuhakikisha Daftari la Wapiga Kura linahakikiwa na pia kufanya
marekebisho ya Sekretarieti ya ZEC. Dk. Ali Mohamed Shein katika hotuba
yake aliyoitoa wakati wa utangazwaji wa matokeo ya Uchaguzi, alikubali
kuyafanyia kazi mambo hayo yote mawili ili kuondoa kasoro zilizopo
katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo. Hadi hivi
tunavyozungumza, mabadiliko hayo hayajafanyika na Sekretarieti hiyo ya
ZEC sasa inajiandaa tena kututumbukiza katika vurugu nyengine za
uchaguzi mkuu wa 2015. Hata hizi hatua nilizozitaja hapo juu
zinategemewa kufanikishwa kwa kuitumia Sekretarieti hii ambayo ndiyo
imekuwa chanzo cha uchafuzi wa chaguzi zote za 1995, 2000, 2005 hadi
2010.
Kutokana
na hali hiyo, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kimeona
kuna haja ya kuyaeleza haya mbele ya wananchi kupitia kwenu waandishi wa
habari. Tukiwa ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar
tumekuwa tukiyawasilisha kwa wenzetu lakini hadi sasa hatujaona hatua za
maana na za dhati zenye lengo la kuyachukulia hatua. Tunaamini wakati
umefika masuala haya yajulikane na wananchi na jumuiya ya kimataifa kwa
ujumla na pia tunataka hatua zifuatazo zichukuliwe ili kuiepusha nchi na
vurugu zinazoweza kutokea kwa kukiuka misingi ya katiba na sheria
katika uendeshaji wa uchaguzi huru, wa haki na amani:
1.
Wapiga kura haramu wote waliopatiwa vitambulisho vya Mzanzibari kinyume
na sheria watakiwe kuvisalimisha vitambulisho hivyo na wasiandikishwe
katika Daftari la Wapiga Kura.
2. Watu wote wenye haki ya kupatiwa ZAN
IDs wapewe vitambulisho vyao kabla ya uandikishaji wa mwisho
unaotarajiwa kuanza tarhe 16 Mei ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba
kujiandikisha na kupiga kura.
3. Vikosi vya Ulinzi na Usalama vikiwemo
JWTZ na Idara Maalum za SMZ ziache kutumiwa kisiasa na kwenda kinyume
na sheria zinazoongoza kazi zao ambazo zinakataza kujiingiza katika
masuala ya kisiasa.
4. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala
za Mikoa na Idara Maalum za SMZ) awache kuwatumia Wakuu wa Mikoa, Wakuu
wa Wilaya na Masheha katika kusajili wapiga kura haramu kwa kuwapatia
ZAN IDs na wakati huo huo kuwakatalia wapiga kura halali haki ya
kusajiliwa na kupatiwa ZAN IDs.
5. Idara ya Usajili wa Wazanzibari iache
kutumika kisiasa kwa kusajili watu wasio Wazanzibari, watoto wadogo na
watu wanaotoka nje ya majimbo yao kwa lengo tu la kukisaidia CCM.
6. Jeshi la Polisi lisikubali kutumiwa kinyume na sheria kuwalinda wapiga kura hao haramu wanapopelekwa kwenda kujiandikisha.
7. Daftari la Wapiga Kura lifanyiwe
uhakiki kwa mfumo wa kielektroniki unaotumia bio-metric features ili
kuwafuta waliosajiliwa zaidi ya mara moja na pia kuwaondoa waliofariki
na watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
8. Sekretarieti ya ZEC ifanyiwe marekebisho ili iwe ni Sekretarieti huru isiyojiegemeza kwenye Chama cha CCM.
9. ZEC ikatae kutumiwa na CCM katika suala la ukataji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi.
Mwisho
kabisa, nitumie fursa hii kusema kwamba pamoja na matatizo ya uchaguzi
mkuu wa 2010, tuliweza kuvuka salama kupitia misingi madhubuti ya
maridhiano ambayo tuliyaasisi mimi na Rais mstaafu, Dk. Amani Karume.
Maridhiano yale yalipaswa kuendelezwa ili tufikie hatua ya kufanya
chaguzi huru, za haki na za amani na pia kujenga misingi madhubuti ya
umoja na maelewano katika nchi yetu. Sisi tulifanya wajibu wetu.
Ni
imani yangu kwamba Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein nao
watafanya wajibu wao ili kuepuka kuturudisha kule tulikotoka. Naamini
kwamba Zanzibar na Tanzania zinaweza kufikia mahala pa kufanya uchaguzi
ulio huru, wa haki na amani na kuwa mfano katika Bara la Afrika.
Niwakumbushe
tu wenzangu kwamba wimbi la mabadiliko linapofikia wakati wake huwa
halizuiliki tena. CCM isitarajie kuendelea kubakia madarakani kwa
kutumia njia za hadaa, udanganyifu, hujuma, nguvu, ubabe na vitisho.
Hii
ni nchi yetu sote na kama alivyowahi kusema Rais Mstaafu Benjamin
William Mkapa, CCM haina hatimiliki ya nchi hii. Hatuna budi kulitambua
hilo na tushirikiane kuivusha salama nchi yetu katika uchaguzi mkuu huu
na baada ya uchaguzi mkuu kwa kuheshimu matakwa ya wananchi.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
Ahsanteni sana.