NAIBU WAZIRI HASUNGA: WANANCHI WAPEWE ELIMU KUHUSU HIFADHI ZA WANYAMAPORI

    Serikali imewataka Maafisa Wanyamapori  nchini  kujikita zaidi  katika kutoa elimu kwa wananchi hususani wakulima na wafugaji wa...

 
 
Serikali imewataka Maafisa Wanyamapori  nchini  kujikita zaidi  katika kutoa elimu kwa wananchi hususani wakulima na wafugaji wanaozunguka maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini ili kuepusha migogoro kati yao na mamlaka za hifadhi zinazosimamia maeneo hayo.
 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga alipotembelea hifadhi ya pori la akiba la Mkungunero kwa ajili ya kutatua mgogoro wa wafugaji wa vijiji vinavyo zunguka pori hilo na mamlaka ya hifadhi ya pori la Mkungunero, ambapo zaidi ya ngombe mia mbili hamsini wanashikiliwa kwa uvamizi.
 
“Wekezeni nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka pori hili ili wafahamu umuhimu na manufaa ya kutunza hifadhi badala ya kusubiri ng’ombe waingie kwenye hifadhi ili muwakamate, kazi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori siyo kuwafilisi wananchi,” amesema Naibu Waziri Hasunga.
 
Ameeleza kuwa jukumu kubwa la maafisa hifadhi ni kuwaelimisha wananchi ili waweze kuzijua taratibu na sheria zinazosimamia hifadhi za wanyama pori hapa nchini jambo litakalo punguza kwa kiasi kikubwa migogoro. 
Aidha amewataka maafisa hifadhi wa pori la akiba la Mkungunero kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu, kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na unyanyasaji wa wananchi  kwani vinaichafua Mamlaka  ya Usimamizi wa Wanyamapori na kujenga sifa mbaya kwa askari wake. 
 
“Serikali haitosita kumchukila hatua kali za kinidhamu Afisa yoyote atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa na unyanyasaji, hivyo hakikisheni mnafanya kazi kwa weledi mkizingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kuongeza ufanisi wa Mamlaka hii,” aliongeza Hasunga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Sezaria Makota ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia kwa karibu Mamlaka ya Usimamizi wa Pori la akiba la Mkungunero. 
“Ninapenda kuishukuru Wizara kwa juhudi zake za dhati za kufuatilia na kusimamia kwa karibu shughuli za pori hili, tunaomba muendelee na juhudi hizi za kutoa elimu kwa maafisa hifadhi wa wanyamapori na kutatua migogoro ya pori hili,” alisisitiza Bi. Sezaria .
 
Akitoa maelekezo kwa maafisa hifadhi wa pori la akiba la Mkungunero, Kaimu Mkurugenzi – Usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. David Kanyata amesema wamepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na watahakikisha wanayafanyia kazi kwa wakati muafaka. 
“Tunaahidi kuyatekeleza kwa haraka maagizo yote ya Mhe. Naibu Waziri ili kwenda na kasi ya awamu ya tano,” alifafanua Kanyata.
 
Meneja wa pori la akiba la Mkungunero Bw. Emmanuel M. Birasso ameeleza kuwa pori hilo lina faida kubwa kiuchumi na kiikolojia ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu muhimu ya mazalia ya wanyamapori ambao wako hatarini kutoweka kama tembo, chui na duma.
Aliongeza kuwa, pamoja na umuhimu wa pori hilo bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka ya pori hilo kama ujangili, uvamizi wa hifadhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji na uchimbaji madini na  migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
“Kumekuwa na changamoto kubwa ya uvamizi wa hifadhi kwa ajili ya shughuli za ufugaji ambapo mifugo 1320 na watuhumiwa 12 wamekamatwa hadi sasa  kwa makosa ya uvamizi” aliongeza Bw. Birasso.
 
Pori la akiba la Mkungunero lililopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, linazungukwa na vijiji vipatavyo 11 na lina ukubwa wa kilomita za mraba 743.95.
 
Na Octavian Kimario, Maelezo

Related

OTHER NEWS 7300799926236061722

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item