KATIBA MPYA YAIPASUA CCM

  MAKUNDI YA URAIS YACHOCHEA MAANDAMANO KUPINGA SERIKALI TATU CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeweka mkakati wa kuipinga rasimu ya Katiba mpya...

 
MAKUNDI YA URAIS YACHOCHEA MAANDAMANO KUPINGA SERIKALI TATU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeweka mkakati wa kuipinga rasimu ya Katiba mpya, hususan pendekezo la muundo wa serikali tatu, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Mkakati huo umekuja baada ya kubaini kuwa rasimu ya Katiba mpya iliyopendekeza muundo huo imekipasua chama hicho katika makundi yanayohatarisha uhai wa chama.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kuzungumza na mawaziri, wabunge, viongozi na makada mbalimbali wa chama hicho tawala, umebaini kuwa makada wengi wameshangazwa na hatua ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Warioba kuruhusu pendekezo la kutaka muundo wa serikali tatu liingizwe kwenye rasimu.
Tayari Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye anatajwa kutaka kuwania urais amepinga pendekezo hilo, kwa madai kwamba hakuna nchi inayoongozwa na marais watatu duniani.
Makundi mengine ya urais yanadai kuwa rasimu hiyo ikipita itawaweka njia panda wasijue wagombee nafasi gani ifikapo mwaka 2015.
Baadhi ya vigogo wa chama hicho waliliambia gazeti hili kuwa lawama za kwanza wanazielekeza kwa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete, kwa madai kuwa aliiona rasimu hiyo kabla ya mtu mwingine yeyote na kuiacha kamati ya Jaji Warioba ikija na pendekezo la kutaka serikali tatu.
“Kwanza Ilani yetu inazungumzia serikali mbili, kule Zanzibar Rais Ali Mohamed Shein na Naibu Katibu Mkuu Visiwani wanagombana na Wazanzibari wa CUF kila siku kuhubiri serikali mbili, leo rasimu inakuja na serikali tatu na rais anaiona na anaipitisha ije kwa wananchi. Hatumuelewi,” alisema mmoja wa viongozi wa chama hicho, mjumbe wa NEC kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kigogo huyo alisema chama kinasubiri kwa hamu kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC), inayotarajiwa kukutana Jumatatu ijayo jijini Dar es Salaam, maalumu kwa ajili ya kujadili rasimu hiyo ya Katiba na kutoka na msimamo wa chama.
Kada mwingine ambaye ni mwenyekiti wa CCM kwenye moja ya mikoa ya Kanda ya Kati, alilieleza gazeti hili kuwa kilichotokea ndani ya chama hicho kuhusu pendekezo la serikali tatu ni kama bomu lililolipuka ghafla.
“Mimi nakuambia kilichotokea ni kama bomu vile, sasa kila mtu amenyanyuka, anakung’uta vumbi na kuanza kuvuta fikra nini kimetokea. Nadhani kikao cha CC kesho kutwa ni muhimu sana na lazima tuwe na NEC kabla ya Bunge kumalizika tukawekane sawa,” alisema mwenyekiti huyo wa CCM mkoa.
Kabla ya chama hicho kuitisha kikao cha CC ya dharura, baadhi ya makundi ya urais yalielezwa kuanza kupanga njama na mikakati ya kuwachonganisha baadhi ya wafuasi wao kuitisha maandamano kupinga pendekezo la serikali tatu.
 
Mikakati ya kuzima serikali tatu
Wakati Wana CCM wengi wamegawanyika kutokana na rasimu ya pendekezo hilo, upande wa pili wanajipa moyo kwamba hoja hiyo haitapita kuwa sheria ndani ya Katiba mpya.
Moja ya mikakati inayofanywa na chama hicho kwa sasa ni kuhakikisha nakala ya rasimu hiyo inawafikia wanachama ngazi ya tawi ili wailewe na kuwataka wawe makini wakati wa upigaji kura kupinga baadhi ya mambo wasiyoyataka, ikiwamo hoja ya kutaka kuwa na serikali tatu.
Pia chama hicho kimeanzisha mabaraza ya Katiba ya chama ili kuwapa fursa zaidi wanachama wao kuijua rasimu hiyo na kushiriki kikamilifu kuipitisha.
Wabunge Viti Maalumu wacharuka
Baadhi ya wabunge wa Viti Maalumu waliliambia gazeti hili kuwa pendekezo hilo linaonesha wivu wa wajumbe wa tume hiyo kwa wabunge hao.
“Umoja wa wanawake (UWT) ulishapitisha azimio kwamba ukomo wa Viti Maalumu ni awamu mbili. Lakini kusema viti hivyo viondoke, havina maana, ni uamuzi uliotokana na wivu,” alisema mbunge mmoja wa Viti Maalumu ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mbunge huyo ambaye aliungwa mkono na wenzake, alisema watahakikisha hoja hiyo haipiti na kuingizwa kwenye Katiba mpya.
Wiki iliyopita, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa rasimu ya mapendekezo ya katiba mpya ambayo imesheheni masuala mazito ambayo kama yatapitishwa yataleta mabadiliko makubwa ambayo yamekuwa yakipiganiwa kwa zaidi ya miaka 20.
Miongoni mwa mambo makuu yaliyoingizwa katika rasimu hiyo ni mfumo mpya wa Muungano wa serikali tatu; serikali ndogo ya mawaziri 15; Tume Huru ya Uchaguzi; spika na naibu wake wasio wabunge wala viongozi wa vyama vya siasa.
Mengine yaliyoingizwa ni kumnyang’anya rais madaraka ya kuteua peke yake viongozi wa ngazi za juu. Tume inapendekeza kwamba rais adhibitiwe katika kuteua mawaziri na manaibu wao, majaji na manaibu wao, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na makatibu wakuu na manaibu wao.
Imependekeza rais asaidiwe na vyombo kadhaa katika uteuzi huo. Mawaziri watakaoteuliwa na rais hawatashika nyadhifa zao hadi waidhinishwe na Bunge. Vile vile, rais atateua majaji kutoka miongoni mwa majina yatakayopendekezwa kwake na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tume imependekeza liundwe Baraza la Ulinzi na Usalama litakalomshauri rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Zaidi ya hayo, kinga ya rais kutoshitakiwa imependekezwa ibaki pale pale, ingawa Bunge lina mamlaka ya kumshitaki kama ilivyo sasa.
Rasimu pia imependekeza umri wa mgombea urais ubaki miaka 40 ya sasa. Katika uchaguzi, rais atatangazwa mshindi iwapo atakuwa amepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote; na matokeo yake yatahojiwa mahakamani ndani ya mwezi mmoja tangu yalipotangazwa.
Mbali na kurejeshwa kwa taifa la Tanganyika, tume imependekeza pia mgombea binafsi aruhusiwe katika ngazi zote, kuanzia kitongoji hadi Ikulu.
Akisisitiza umakini uliotumika kuchakata mapendekezo yaliyokusanywa kwa wananchi tangu Aprili mwaka jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Warioba alisema wamezingatia masilahi ya taifa na mahitaji ya wakati katika kila eneo.
 
Source: Chadema Social Media

Related

OTHER NEWS 3810854511496366674

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item