MAMBO YANAYOHARIBU AFYA YA BINADAMU
Mazingira ni jambo linaloathiri afya. Iwapo maji tunayokunywa na kutumia n i safi na salama, iwapo hewa tunayovuta si chafu, maeneo tunay...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/mambo-yanayoharibu-afya-ya-binadamu.html
Mazingira ni jambo linaloathiri afya. Iwapo maji tunayokunywa na kutumia ni safi na
salama, iwapo hewa tunayovuta si chafu, maeneo tunayofanyia kazi ni salama na
pia nyumba tunazoishi, basi afya zetu huwa salama zaidi ikilinganishwa na watu
wanaoishi kwenye maeneo yasiyo na maji safi na salama au kuvuta hewa chafu na
kufanya kazi kwenye mazingira ya hatari.
Uchunguzi
uliofanywa na chuo kikuu cha Zuyd nchini Uholanzi umeonesha kwamba, kuvuta hewa
iliyochafuliwa kwa gesi za magari kwa lisaa limoja kunatosha kumpatia mtu
mfadhaiko wa kifikra au stress katika ubongo wake.
Utafiti mwingine
uliofanywa na chuo kikuu cha India cha Purdue umebainisha kuwa, sumu kali
inayotokana na sumu ya risasi, inayoweza kuiingia mwilini mwa binadamu kutokana
na kula vitu vilivyoingiwa na sumu hiyo, nchini Marekani huathiri maelfu ya
watoto kuliko kiwango dhaifu cha sumu hiyo kinachoweza kuwepo katika vifaa vya
kuchezea na mapambo yanavyosafirishwa.
Afya ya binadamu
pia huweza kuathiriwa na watu wanaomzunguka.
Iwapo una familia
unayoiangalia au marafiki katika jamii yako, basi una nafasi kubwa ya
kuimarisha afya yako kuliko mtu ambaye anaishi pekee au hana familia na
marafiki.
Uchunguzi uliofanywa na chuo kikuu cha
Washington nchini Marekani umegundua kuwa, ushirikiano wa kifamilia ni jambo
zuri kwa mtu na hupunguza kesi za watu kujiua, hasa wale wanaopatwa na matatizo
ya mfadhaiko wa kifikra au wanapokuwa na fikra ya kutaka kujiua.
Vilevile tamaduni,
mila na desturi za jamii na jinsi watu wanavyozithamini itikadi hizo, zina
mafasi kubwa katika afya zao ingawa matokeo yake huweza kuwa mazuri au mabaya.
Kwa mfano mazoea na
mila ya kuwakeketa au kuwatahiri watoto wa kike na wanawake ina madhara makubwa
kama vile kuongeza kiwango cha maambukizo ya magonjwa na hata matatizo ya
kiakili miongoni mwa wasichama na wanawake wanaofanyiwa jambo hilo.
Urithi wa jenetiki
ni suala jingine linaloathiri afya za watu. Kuishi muda mrefu, siha ya mwili
kwa ujumla na kupatwa na baadhi ya magonjwa na hata kuzaliwa nayo, ni masuala
yanayoainishwa na jinsi jeni zetu zilivyo mwilini tangu wakati tunapozaliwa.
Mambo mengine ni
pamoja na vyakula tunavyokula, harakati zetu kifizikia, tabia na mazoea tofauti
kama kuvuta sigara au kunywa pombe na kutumia madawa ya kulevya.
Pia jinsi
tunavyoweza kuvumilia mfadhaiko wa kifikra au stress yote hayo yana nafasi
muhimu katika uzima wetu kimwili na kiakili.
Suala jingine
tunaloweza kulitaja hapa ni matumizi ya vituo vya afya na hospitali. Jamii
ambayo ina vituo vya afya vya kutosha, vilivyo vizuri na vyenye kukidhi mahitaji
ya watu wa jamii hiyo, watu wake wana nafasi zaidi ya kuwa na siha nzuri kuliko
jamii au watu wanaoishi maeneo ambayo hayana vituo vya afya au hospitali.
Kwa mfano nchi
zilizoendelea zenye vituo vya afya na hospitali za kutosha na nzuri, watu wa
nchi hizo huishi maisha marefu zaidi ikilinganishwa na nchi masikini zenye
upungufu katika sekta hiyo.
Jinsia ya mtu pia huathiri afya yake. Kuna
magonjwa yanayowapata wanawake zaidi na kuna magonjwa yanayowapata wanaume
zaidi.
Hali ya miili ya wanawake hutofautiana na
wanaume na hata kazi na shughuli wanazozifanya pia huweza kuathiri afya zao kwa
ujumla. Kwa mfano, kubeba mimba na kujifungua, kansa ya ovari na kizazi
huathiri afya ya wanawake katika hali ambayo wanaume hupatwa na kansa ya tezi
kibofu na ya korodani.
Wakati wa vita
wanaume hushiriki kwa wingi kuliko wanawake na matokeo yake ni kuuawa au
kujeruhiwa. Wanawake na wasichana huenda wakawa wahanga wa vitendo vya utumiaji
mabavu dhidi yao na ukatili kuliko watoto wa kiume na wanaume.
Katika baadhi ya jamii
watoto wa kike na wanawake huwa hawapewi fursa ya kupata elimu na kujiendeleza
kama wanaume, suala ambalo huathiri afya zao pia. Tafiti nyingi zimeonyesha
ubaguzi wa kijinsia katika utoaji huduma za afya hata katika nchi
zilizoendelea.
Miongoni mwa mambo
muhimu yanayoijenga afya ya mwanadamu ni kula lishe salama na mlo uliokamilika.
Tunaposema lishe salama na mlo uliokamilika au healthy balanced diet kwa
kimombo, tunamaanisha masuala muhimu mawili.
Moja ni kula
kiwango kinachotakiwa cha chakula kwa mujibu wa harakati na hitajio la mwili
wako, na pili ni kula aina tofauti za vyakula vinavyotakiwa ili kuijenga siha
ya mwili.
Tunapaswa kufahamu
kwamba, kula lishe bora ni suala muhimu linalochangia kuimarisha afya ya mwili.
Lishe salama na iliyokami inamaanisha kula vyakula tofauti kutoka katika
mafungu manne makuu ya vyakula na kupunguza baadhi ya vyakula katika milo
tunayokula kila siku.
Aina ya vyakula
vinavyopaswa kuwepo kwenye milo yetu ni pamoja na matunda na mboga kwa
wingi. Kiwango cha kutosha cha wanga kama vile mkate, wali, viazi, pasta
na vinginevyo na ni bora viwe vinatokana na aina mbalimbali za nafaka kamili zisiokobolewa.
Maziwa na vyakula
vinavyotokana na maziwa kama mtindi na jibini. Vyakula vyenye protini kama
vyama, samaki, mayai, maharagwe na vinginevyo na vilevile kiasi kidogo cha
sukari , mafuta na chumvi.
Ufuatao ni ushauri au
vidokezo muhimu (tips) kuhusiana na namna ya kula vyema ili kuzilinda na
kuziimarisha afya zetu. Tunashauriwa mlo tunaokula uwe na kiasi cha
kutosha cha wanga, kwani aina hiyo ya chakula huipa miili yetu nguvu.
Tunashauriwa kula
matunda na mboga kwa wingi kila siku.
Baadhi wanasema, ni
bora kula aina 5 za matunda tofauti na mboga kwa siku.
Pia tunashauriwa
kula samaki kwa wingi kwa uchache mara mbili kila wiki na kama hatutoweza
kufanya hivyo au kwa wale ambao samaki wanawadhuru na wale wasiokula nyama,
wanapaswa kula virutubishi muhimu vinavyotupatia mada zinazopatikana kwenye
samaki kwa ajili ya afya ya miili yetu.
Tunashauriwa
kupunguza kwa kiasi kikubwa sukari na mafuta katika milo yetu.
Vilevile
tunashauriwa kula chumvi kwa kiwango kidogo, isizidi gramu 6 kwa siku kwa watu
wazima.
Tunapaswa kufahamu
kuwa, baadhi ya vyakula tayari vina kiwango cha chumvi ndani yake kwani karibu
theluthi moja ya chumvi katika milo yetu hutoka katika vyakula ambavyo tayari
vimeshatengeneza kama supu iliyo tayari, sosi, mikate, asusa (snacks), pai,
pizza vyakula vinavyosindikwa na kuhifadhiwa. Hivyo kuna umuhimu wa kula
vyakula hivyo kwa kiasi kidogo.
Hii ni kwa sababu
ongezeko la chumvi mwilini huweza kumfanya mtu apatwe na shinikizo la damu,
hali ambayo huweza kusababisha ugonjwa wa moyo na kiharusi.
Suala jingine
tunalopaswa kuzingatia ni kunywa maji ya kutosha, tunashauriwa kila siku kunywa
kiasi cha gilasi 6 hadi 8 za maji au vyakula vingine vya majimaji kama juisi na
kadhalika, ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.
Maji yana faida nyingi na baadhi yake ni
kuusaidia mwili kuondoa kwa urahisi sumu na mabaki yasiyotakiwa mwilini.
Kusaidia kulainisha
macho na maungio ya mwili na pia hutusaidia wakati wa kumeza.
Jambo jingine
tunaloshauriwa ni kuupa mwili harakati, mazoezi ya mara kwa mara na kuwa na
uzito unaotakiwa kiafya.
Jengine ni kutoacha
kula kifuangua kinywa.
Tunatakiwa
kustaftahi kila siku kwa sababu chakula hicho cha asubuhi huupa mwili nguvu ya
kuanzia siku na huamsha utendaji kazi wa mwili kwa ajili ya siku nzima.