SERIKALI HAIWEZI KUTAJA MAJINA YA VIGOGO WA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA, WABUNGE WAMO KATIKA ORODHA HIYO

DODOMA.  WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa m...

DODOMA. 
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.

Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya wabunge kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha. “Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna vithibitisho.

“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse.

Katika swali lake ambalo lilisababisha kelele za kuzomea, Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo lazima mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini mtindo huu si mzuri...”
Patashika hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na kama haioni kama kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege na juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.

Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.
Alisema Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo la matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini na alitaja takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi Machi, 2012.

Alisema pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.

Hata hivyo, katika swali lake la nyongeza, Magige alisema uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa siri kiasi cha kutiliwa shaka kuwa huenda zinachukuliwa na maofisa waliozikamata ndiyo maana hakuna uwazi.
Kuhusu hilo, Waziri Lukuvi alisema suala la uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi kutokana na sheria zilizopo kutotoa nafasi ya kuteketezwa mapema kwa kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi akisema wakati mwingine hukaa zaidi ya miaka 10.
SOURCE:  MWANANCHI

Related

CAR BOMB BLAST KILLS 6 IN SOMALIA

 Somali soldiers`walk near the car wreckage of a suicide bomber in Mogadishu, Somali , Thursday Feb,1 3 2014, Somali police say the car bomb exploded near the gate of Mogadishu airport Thurs...

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AFUNGUA KONGAMANO LA UHAMASISHAJI NA UWEKEZAJI KANDA YA ZIWA JIJINI MWANZA.

   Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la siku tatu la Uwekezaji na Uhamasishaji Kanda ya Z...

KAMATI KUU CHADEMA KUKUTANA KWA DHARURA

    TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KAMATI KUU YA CHADEMA KUKUTANA KWA DHARURA   Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) itakutana kwa ajili ya kikao ch...


LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

904746
item