WABUNGE WATAKA UWAZI MALI ZA VIONGOZI
KAMATI za Bunge zinazosimamia fedha za umma zimeazimia kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki w...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/wabunge-wataka-uwazi-mali-za-viongozi.html
KAMATI za
Bunge zinazosimamia fedha za umma zimeazimia kuwa Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki wa mali za viongozi.
Hali hiyo inasababisha viongozi kutoweka wazi mali wanazozimiliki na ni rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa kweli.
Katika
maazimio yao 22 yaliyofikiwa siku ya mwisho wa mafunzo, juzi, kamati
hizo za Hesabu za Serikali (PAC), Serika za Mitaa (LAAC) na ile ya
Bajeti zimependekeza kuwa ni vema sekretarieti ikafanya utafiti wa
umiliki wa mali kwa viongozi wa umma na kuweka taarifa hizo katika
tovuti yake.
Lengo la
kufanya hivyo ni kuwawezesha wananchi kuziona mali zinazomilikiwa na
viongozi wao na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa taarifa ya umiliki
huo basi taarifa hiyo itolewe kwa tume.
Katika
maazimio mengine kamati zimekubaliana kuwa kutokana na kutokuwepo na
taarifa sahihi kuhusu deni la taifa, kuna umuhimu wa kuwakutanisha wadau
wakuu wanaohusika hususan Benki Kuu (BoT), Hazina, Kamati za Bunge na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG).
Hatua hiyo
itawawezesha kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa deni hilo. Vilevile
imeamuliwa kuwa serikali ishauriwe kuunda chombo huru kitakachosimamia
deni la taifa.
“Kamati za
Bunge zinazoshughulikia usimamizi wa fedha na rasilimali za taifa
zishughulikie zaidi maafisa masuuli hatarishi (risk based) ili kuleta
thamani ya fedha katika utendaji wao. Kamati zishirikiane na CAG katika
kuamua ni afisa masuuli yupi aitwe kukutana na Kamati,” walisema.
Serikali
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge na Tamisemi
imetakiwa kuanzisha utaratibu wa kuratibu mikutano na mafunzo ya
wakurugenzi wa halmashauri kwa pamoja kuliko kila wizara kuwaita
watendaji hao katika sehemu mbalimbali kwa muda tofauti na kuwafanya
kutokuwepo ofisini kwa kipindi kirefu.
“Taarifa za
mwaka za Kamati za Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha utekelezaji
wa mapendekezo ya kamati yaliyotolewa awali. Kamati ziwezeshwe kifedha
ili ziweze kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yao.
“Kanuni za
Bunge zieleze utaratibu wa ufuatiliaji wa maazimio ya Bunge na namna
utekelezaji wake utavyowasilishwa bungeni. Vilevile Bunge litenge siku
ya kuijadili serikali ilivyoshughulikia hoja za kamati za Bunge. Spika
ashauriwe kuhusu umuhimu wa kuunda kamati ya Bunge ya kufuatilia ahadi
za serikali,” alisema mjumbe mmoja na kuungwa mkono na wenzake.
Serikali
iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo
vya rushwa na mmomonyoko wa maadili vinavyoongezeka kwa kasi hapa
nchini.
Vilevile
viongozi wa umma na watendaji waongoze kwa mfano kwa kutojihusisha na
vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.
“Sheria ya
“Anti Money Laundering” ya 2006 irekebishwe ili iweke viwango vya fedha
ambavyo mtu anaweza kuingia au kutoka nazo nchini bila kuziweka wazi.
Kuna umuhimu wa Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni za kutekeleza sheria
hiyo.
“Benki Kuu
iandae mfumo thabiti wa usimamizi wa maduka ya fedha na kuhakikisha
kutungwa kwa sheria inayozuia matumizi ya fedha za kigeni katika
shughuli za kibiashara hapa nchini,” alisema mjumbe akiungwa mkono na
wenzake.