ZANZIBAR YATIA SAINI NA KAMPUNI YA SHELL KATIKA KUSHIRIKI KUENDELEZA SEKTA YA MAFUTA NA GESI
Na Said Ameir, Uholanzi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Mafuta ya Shell ya Uholanzi zimetia saini Makubaliano ya Ushir...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/zanzibar-yatia-saini-na-kampuni-ya.html
Na Said Ameir, Uholanzi
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Mafuta ya Shell ya Uholanzi
zimetia saini Makubaliano ya Ushirikiano katika kuendeleza sekta ya
mafuta na gesi.
Makubaliano
hayo yametiwa saini juzi tarehe 28 Agosti, 2013 mjini The Hague ambapo
Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban
alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na Mwakilishi wa Kampuni Shell Tanzania Axel Knospe alitia
saini kwa niaba ya Kampuni hiyo.
Makubaliano
hayo yamefikiwa mjini The Hague wakati wa ziara ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed inayoendelea nchini
humo.
Kabla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo Dk. Shein alifanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa kampuni ya Shell yaliyojielekeza katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Zanzibar na Kampuni hiyo.
Kwa
mujibu wa makubaliano hayo Kampuni ya Shell itaisaidia Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kujenga uwezo wa kitaalamu, katika hatua za awali za
uendelezaji wa sekta hiyo.
Sambamba
na hatua hiyo Kampuni ya Shell itasaidia pia shughuli za maendeleo ya
vijana katika kuwajengea uwezo kwa kuwapatia elimu na mafunzo mbalimbali
yakiwemo ya stadi za ujasiriamali.
Akizungumza
mara baada ya kutia saini makubaliano hayo Waziri wa Ardhi, Makazi,
Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban alisema “kutiwa saini kwa
makubaliano hayo ni hatua moja kubwa na mwelekeo sahihi katika jitihada
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza sekta ya nishati
Zanzibar”
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Shell Tanzania Bwana Axel Knospe
alieleza kuwa wakati mashauriano yakiendelea kati ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya
kuliondoa suala la mafuta na gesi katika mambo ya muungano, Kampuni hiyo
itaendelea na dhamira yake ya ushirikiano na Zanzibar hadi hapo muda
utakapokuwa tayari kuanza kazi ya shughuli za uchimbaji mafuta na gesi
ambapo itaifanya kazi hiyo kwa kuzingatia uwajibikaji kiuchumi, kijamii,
kimazingira na kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu
“wakati
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zikishughulikia kwa pamoja suala la kisheria na kisera
kuipatia Zanzibar haki pekee ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi
Zanzibar, Kampuni ya Shell itaendelea na dhamira yake ya kushirikiana na
Zanzibar hadi hapo muda muafaka utakapofika kuanza shughuli za
uchimbaji wa mafuta na gesi” alieleza bwana Axel Knospe.
Wakati
akizungumza na Rais wa Zanzibar mjini hapa juzi Waziri wa Biashara ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Uholanzi Bibi Lilianne Ploumen
alimueleza Rais kuwa Serikali ya nchi hiyo iko tayari kutumia utaalamu
na uzoefu wake katika sekta ya mafuta na gesi kuisaidia Zanzibar
kuendeleza sekta hiyo.
Bibi
Ploumen alieleza kuwa Serikali ya nchi hiyo iko tayari kutoa fursa za
mafunzo kwa watumishi wa Serikali ya Zanzibar katika sekta ya nishati
ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uzoefu katika kusimamia rasilimali
hizo, utunzaji wa mazingira na ushiriki wa wananchi katika matumizi ya
rasilimali hiyo kuepusha migogoro.
“Mambo
ya msingi ya kupewa kipaumbele ni pamoja na namna ya uendeshaji,
usimamizi na matumizi bora ya rasilimali hizo, ushirikishwaji wananchi
na utunzaji mazingira”alieleza bibi Ploumen na kusisitiza haja ya
Zanzibar kujifunza kutoka nchi nyingine kuepuka makosa yaliyofanywa na
baadhi ya nchi ikiwemo Uholanzi yenyewe.
Dr. Shein anamaliza ziara yake ya siku tano nchini Uholanzi leo na anatajiwa kurejea nyumbani Jumapili ijayo.
Katika ziara hiyo Dk Shein amefuatana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Mshauri wa
Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed
Ramia.